Arusha. Licha ya kukabiliwa na changamoro nyingi, Sekta ya mifugo nchini inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi kutokana na mchango wake katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kutoa ajira, kuongeza kipato cha kaya, kuchochea maendeleo ya viwanda na kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Hata hivyo, sekta hiyo bado inakabiliwa na magonjwa mbalimbali yanayoathiri uzalishaji, biashara ya mifugo na maendeleo ya wafugaji.

Miongoni mwa magonjwa yanayoisumbua sekta hiyo ni sotoka ya mbuzi na kondoo (PPR), ugonjwa wa midomo na miguu (FMD), ugonjwa wa kutupa mimba (Brucellosis) na homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP).

Mbali na hayo, sekta ya mifugo inaendelea kuathiriwa na magonjwa mengine yanayovuka mipaka, hali inayosababisha hasara kwa wafugaji, kupunguza uzalishaji na kudhoofisha ushindani wa bidhaa za mifugo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya ya wanyama kupitia maboresho ya sera, kuimarisha utoaji wa huduma za mifugo, ufuatiliaji wa magonjwa na utekelezaji wa programu za kitaifa za chanjo.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Fabian Madele jijini Arusha jana, wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta hiyo nchini kuhusu chanjo na uchanjaji wa mifugo.

Amesema hatua hizo zinalenga kulinda rasilimali za mifugo, kuongeza uzalishaji na kuboresha fursa za biashara ya mifugo na bidhaa zake ndani na nje ya Tanzania.

Dk Madele amesema licha ya umuhimu mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa, uwezo wake kamili bado unakwamishwa na ukosefu wa mikakati ya pamoja ya kudhibiti magonjwa ya mifugo, mengi ambayo yanaweza kuzuilika kwa matumizi sahihi ya chanjo.

“Sekta ya mifugo inaendelea kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania. Hata hivyo, uwezo wake bado unakwamishwa na kutokuwepo kwa mikakati ya pamoja katika kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mifugo,” amesema.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha afya ya mifugo na ndiyo sababu imeendelea kuwekeza katika programu za kitaifa za chanjo na utambuzi wa mifugo.

Kwa mujibu wa Dk Madele, Juni mwaka 2025 Serikali ilizindua Kampeni ya Taifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ambayo itatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2025/26 hadi 2029/30 kwa gharama ya Sh216 bilioni.

Amesema katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, Serikali imejikita katika kudhibiti magonjwa ya CBPP, PPR, Ndui ya mbuzi na kondoo, Newcastle (ND) pamoja na mafua ya kuku, huku ikiboresha mfumo wa utoaji wa chanjo katika mamlaka 184 za Serikali za Mitaa nchini.

Aidha, amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 Serikali itaendelea na awamu ya pili ya kampeni hiyo kwa kuongeza chanjo ya homa ya mapafu kwa mbuzi, kupanua ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za mifugo na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kudhibiti magonjwa yanayovuka mipaka.

Katika mkutano huo, Serikali pia ilikaribisha utekelezaji wa Programu ya VITAL 2(ubunifu wa mifugo unaobadilisha afya ya wanyama na maisha ya jamii) iliyolenga kuimarisha soko la chanjo, kuongeza upatikanaji wake na kumarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika utoaji wa huduma za afya kwa wanyama.

Amesema programu hiyo ya miaka mitano itatekelezwa Tanzania, Kenya na Nigeria na kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za afya ya mifugo zinawafikia wafugaji wengi zaidi.

Mkurugenzi wa  Chama cha Afya ya Wanyama Tanzania (TAHO) , Dk Daniel Dulla amesema sekta binafsi itashirikiana na Serikali katika uandaaji wa mipango na sera katika kuhakikisha taarifa mbalimbali za mlipuko wa magonjwa ya wanyama zinapatikana kwa haraka na Serikali kuchukua hatua.

Amesema hali ya chanjo ni nzuri, lakini sasa ni wakati wa Serikali kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kudhibiti ubora wa chanjo ya mifugo ili kupata wanyama bora na masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi.

Awali, Katibu  Mkuu wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) , Mathayo Daniel amesema uwekezaji katika chanjo za mifugo ni nguzo muhimu katika kujenga sekta ya mifugo yenye afya, tija na uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti, washirika wa maendeleo, watengenezaji na wasambazaji wa chanjo pamoja na vyama vya wafugaji kwa lengo la kujadili njia bora za kuongeza matumizi ya chanjo kwa afya na uzalishaji endelevu wa mifugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *