
Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na wasimamizi wa mirathi ya marehemu mfanyabiashara Zacharia Hans Poppe, pamoja na kampuni ya ZH Poppe Limited.
Wasimamizi hao walikuwa wakiomba zuio la muda dhidi ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kuzuia kuchukuliwa na kuuzwa kwa mali zilizowekwa rehani kwa ajili ya kurejesha mkopo wa zaidi ya Sh7.4 bilioni.
Maombi hayo ya Madai Na. 11792/2026 yaliwasilishwa na Angel Zacharia na Abel Zacharia, ambao ni watoto wa marehemu na wasimamizi wa mirathi yake, pamoja na kampuni ya ZH Poppe Limited.
Wajibu maombi walikuwa TCB, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali.
Uamuzi huo ulitolewa Juni 15, 2026 na Jaji Arnold Kirekiano, aliyesikiliza maombi hayo. Nakala ya hukumu imewekwa katika mfumo wa mtandao wa Mahakama.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia nyaraka zilizowasilishwa, Mahakama ilihitimisha kuwa waombaji hawakutimiza vigezo vya kisheria vinavyohitajika ili kupewa amri ya muda ya kuzuia benki kuendelea na hatua za kurejesha mkopo wake.
Kutokana na hilo, ombi hilo lilitupiliwa mbali kwa gharama, huku TCB ikiachiwa kuendelea na utekelezaji wa dhamana zake kwa mujibu wa sheria.
Chanzo cha mgogoro
Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, mgogoro huo unatokana na mkopo uliotolewa na TCB kwa kampuni ya ZH Poppe Limited, ambao benki ilidai haukulipwa kwa mujibu wa makubaliano ya mkopo.
Baada ya deni hilo kufikia zaidi ya Sh7.4 bilioni, TCB ilitoa notisi ya mwisho ya kudai malipo na kuanza taratibu za kurejesha fedha zake kupitia mali zilizowekwa rehani.
Hatua hiyo iliwafanya waombaji kufungua maombi ya zuio la muda wakitaka Mahakama iamuru hali ibaki kama ilivyo na kuzuia kukamatwa au kuuzwa kwa malori ya mizigo, malori ya mafuta, trela na mali nyingine hadi muda wa notisi ya kisheria ya siku 90 utakapomalizika.
Waombaji walieleza kuwa kupitia barua ya Machi 25, 2026, walitoa notisi ya nia ya kuishtaki Serikali, wakitarajia kufungua kesi ya msingi dhidi ya TCB baada ya kipindi hicho cha siku 90 kumalizika. Hivyo waliomba Mahakama izuie kwa muda utekelezaji wa dhamana hadi taratibu hizo zikamilike.
Katika viapo vyao, waombaji walidai kuwa kulikuwa na vitendo vya udanganyifu vilivyoathiri umiliki wa hisa, usimamizi na uendeshaji wa kampuni ya ZH Poppe Limited. Walidai kuwa hisa 4,500 za marehemu Zacharia Hans Poppe zilihamishwa isivyo halali kwa Aldo Hans Poppe kupitia nyaraka za ridhaa zinazodaiwa kuwa na kasoro, jambo lililomwezesha kuwa mbia mkuu wa kampuni na kuidhinisha mkopo husika.
Kwa msingi huo, walidai kuwa wanakusudia kufungua kesi ya msingi kupinga uhalali wa mkopo huo mara baada ya muda wa notisi ya siku 90 kuisha.
Hoja za pande zote
Wakili wa waombaji aliiambia Mahakama kuwa maombi hayo yalikuwa na msingi wa kisheria kwa kuwa tayari walikuwa wametoa notisi ya kushtaki Serikali na walikuwa wakisubiri muda wa kisheria kuisha kabla ya kufungua kesi kuu.
Alieleza kuwa iwapo benki ingeruhusiwa kuuza mali hizo kabla ya kesi ya msingi kuwasilishwa, waombaji wangepata hasara kubwa ambayo isingeweza kurekebishwa kwa urahisi.
Alisisitiza kuwa mali zinazokusudiwa kuuzwa ni muhimu kwa shughuli za kampuni, na kwamba mauzo yake yangesababisha kesi inayotarajiwa kufunguliwa baadaye kupoteza maana.
Aidha, alidai kuwa kusimamisha kwa muda hatua za benki kusingeisababishia TCB madhara makubwa zaidi ya kuchelewesha urejeshaji wa mkopo kwa kipindi kifupi.
Kwa upande wao, mawakili wa wajibu maombi waliomba Mahakama ikatae ombi hilo wakieleza kuwa waombaji hawakukidhi masharti ya kisheria yanayohitajika ili kupewa amri ya muda ya kuzuia utekelezaji wa dhamana.
Walisisitiza kuwa madai ya kughushi nyaraka na migogoro ya uongozi ndani ya ZH Poppe Limited hayajawahi kuthibitishwa na Mahakama yoyote na hayahusiani moja kwa moja na TCB.
Mawakili hao walieleza kuwa benki ilitoa mkopo huo kwa kutegemea taarifa rasmi za BRELA zilizowaonyesha wakurugenzi halali wa kampuni, hivyo ilikuwa na haki ya kuamini kuwa taratibu zote za ndani za kampuni zilifuatwa kwa mujibu wa kanuni ya Turquand Rule.
Pia, walirejea uamuzi uliotolewa katika kesi za Royal British Bank dhidi ya Turquand na Freeman & Lockyer dhidi ya Buckhurst Park Properties, wakisisitiza kuwa mtu wa tatu anayefanya biashara na kampuni kwa nia njema hawezi kuwajibishwa kwa migogoro ya ndani ya kampuni hiyo.
Kuhusu madai ya hasara isiyoweza kurekebishwa, walidai kuwa waombaji hawakueleza kwa kina aina ya madhara ambayo hayawezi kufidiwa kwa fedha.
Waliongeza kuwa kwa kuwa mgogoro unatokana na mkataba wa mkopo, fidia inaweza kutolewa iwapo upande wowote utashinda katika kesi ya msingi.
Aidha, walionya kuwa kusimamishwa kwa utekelezaji wa dhamana kungeendelea kuongeza deni ambalo tayari limefikia zaidi ya Sh7.4 bilioni na kuathiri shughuli za benki pamoja na uwezo wake wa kuwahudumia wateja wengine.
Uamuzi wa Mahakama
Katika uamuzi wake, Mahakama ilibainisha kuwa ingawa waombaji walikuwa wametoa notisi ya siku 90 ya nia ya kufungua kesi, hawakuonyesha kwa kiwango kinachohitajika kisheria kuwa wana kesi yenye msingi wa kutosha dhidi ya TCB.
Mahakama ilieleza kuwa madai ya udanganyifu yaliyowasilishwa yanahusu zaidi migogoro ya ndani ya kampuni ya ZH Poppe Limited kuliko uhusiano wa moja kwa moja kati ya waombaji na benki.
Aidha, Mahakama ilisema kuwa licha ya waombaji kudai kuwepo kwa uchunguzi wa jinai kuhusu umiliki wa hisa na uongozi wa kampuni, hawakuwasilisha ushahidi wa ziada kuthibitisha madai hayo baada ya kupingwa na wajibu maombi.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama iliona kuwa madai hayo hayakuonyesha kwa dhahiri uwepo wa kesi yenye nafasi kubwa ya kufanikiwa dhidi ya benki.
Mahakama pia ilikubaliana na hoja ya TCB kwamba benki ilikuwa na haki ya kutegemea taarifa rasmi za BRELA wakati wa kuidhinisha mkopo huo.
Kwa mujibu wa kanuni ya Turquand Rule, taasisi inayofanya biashara na kampuni kwa nia njema inaweza kuamini kuwa taratibu za ndani za kampuni zimefuatwa ipasavyo isipokuwa ithibitishwe vinginevyo.
Kuhusu hoja ya hasara isiyoweza kurekebishwa, Mahakama ilisema waombaji hawakuonyesha jinsi watakavyopata madhara ambayo hayawezi kufidiwa kwa fedha endapo mali zilizowekwa rehani zitauzwa.
Mahakama ilibainisha kuwa mgogoro huo unatokana na mkataba wa mkopo, hivyo fidia inaweza kutolewa kwa upande utakaoonekana kuathirika iwapo utashinda katika kesi ya msingi.
Pia imezingatia uwiano wa usumbufu kati ya pande zote mbili na kubaini kuwa kusitisha utekelezaji wa dhamana kungeendelea kuongeza deni ambalo tayari limefikia zaidi ya Sh7.4 bilioni, jambo ambalo lingeweza kuathiri shughuli za kifedha za benki na uwezo wake wa kuwahudumia wadai na wakopaji wengine.
Kwa sababu hizo, Mahakama ilihitimisha kuwa waombaji hawakukidhi masharti muhimu ya kisheria ya kupewa amri ya muda ya kuzuia benki kuendelea na hatua za kurejesha mkopo wake.
Hivyo, ombi hilo lilitupiliwa mbali kwa gharama, na TCB inaendelea kuwa huru kutekeleza dhamana zake kwa mujibu wa sheria.