Dar es Salaam. Ni takribani miaka 10 sasa tangu msanii wa Bongo Movie, Riyama Ally afunge ndoa na Leo Mysterio. Kumekuwa na tetesi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai wawili hao wameachana.

Hata hivyo Riyama amevunja ukimya baada ya kutafutwa na Mwananchi.Amesema jambo hilo halimshangazi kwani tangu walipofunga ndoa kumekuwa kukiibuka tetesi kama hizo mara kwa mara.

Pia amezungumzia safari ya miaka 10 ya ndoa yao, changamoto walizopitia na matumaini yake ya kupata mtoto siku moja na mume huyo.

“Huo ni uzushi wa kawaida ambao nimeuzoea. Mimi na mume wangu tupo pamoja, tunaendelea vizuri na maisha yetu. Watu wamekuwa wakiifuatilia ndoa yetu tangu siku ya kwanza tuliyofunga ndoa. 

“Hivyo sikushangazwa kuona tena habari za kututenganisha. Ukweli ni hatujaachana na tunaendelea kujenga familia yetu kwa amani,amesema Riyama

Mwigizaji huyo ameeleza kinachofanya ndoa yake kuingia kwenye midomo ya watu mara kwa mara

“Nadhani ni kwa sababu tangu mwanzo watu walikuwa na maoni yao kuhusu sisi. Wapo waliokuwa wakisema nimeolewa na mwanamume mdogo kuliko mimi.

“Wengine wakasema ndoa haitadumu. Lakini leo hii tunatimiza miaka 10 tangu tufunge ndoa na bado tupo pamoja. Hivyo naamini watu wengi walikuwa wakisubiri kuona kile walichokitabiri kinatokea,”amesema

Amesema wao kufikisha miaka kumi ya ndoa ni jambo kubwa sana na siyo rahisi.

“Siyo rahisi kwa wanandoa wowote kufikisha miaka 10. Tumepitia mengi, mazuri na magumu, lakini bado tumeshikamana. Ninamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa tulipo. Miaka 10 ni ushahidi upendo wetu haukujengwa kwa maneno ya watu bali kwa uamuzi wetu wenyewe,”amesema 

Amesema mwanzoni kulikuwa na maneno mengi sana kuhusu utofauti wa umri kati yake na mume wake lakini hilo halikumkatisha tamaa

“Tulijifunza mapema, ukisikiliza sana maneno ya watu huwezi kuishi maisha yako. Leo Mysterio ni mume wangu na nimekuwa nikimheshimu kama mume wangu. Naye ameniheshimu kama mke wake. Hicho ndicho kilichotusaidia kuvuka changamoto zote.

Licha ya kutopata mtoto na mumewe Riyama amesema hilo wala halimpi presha kwani anaamini kila kitu kina wakati wake.

“Mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kama Mungu ameandika tutapata mtoto, tutampata. Mimi bado nina matumaini makubwa sana. Sijakata tamaa hata kidogo. Japo mimi nina mtoto wa kike ambaye nilizaa kabla sijaingia kwenye ndoa na Mysterio,”amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *