Dar es Salaam. Ukiacha furaha iliyoigubika familia ya Simon Mkwizu baada ya mkewe Victoria Mkwizu kujifungua pacha watano kwa mpigo, mzigo wa majukumu ya malezi ni upande mwingine mgumu utakaoifanya familia hiyo iwe na mawazo.

Familia hiyo ya dereva wa bajaji na mama asiye na shughuli yoyote ya kuingiza kipato, wakazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, italazimika kutumia angalau Sh2 milioni kila mwezi, kumudu huduma za watoto hao watano, watatu wa kiume na wawili wa kike.

Katika simulizi yake, Mkwizu anasema mapokezi ya baraka ya watoto watano, yamekuja kwa mchanganyiko wa furaha na wasiwasi wa kumudu malezi ya familia hiyo, katika uzazi wao wa kwanza.

Victoria amejifungua watoto hao Jumamosi Juni 13, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakati ambao ujauzito wake haukuwa umekomaa vema, kama alivyoeleza Mkuu wa wadi ya watoto wachanga katika hospitali hiyo, Dk Martha Mkony.

Amesema watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito wa kati ya gramu 800 na kilo 1.7.

Kutokana na kuzaliwa kabla ya kukomaa kwa ujauzito, amesema kulihitajika uangalizi maalumu, hasa ukizingatia mmoja wao alipata changamoto ya kupumua.

“Akapewa dawa ya kukomaza mapafu Jumapili (Juni 14) na kuanzia hapo wamekuwa wakiendelea vizuri na wanaangaliwa kwa karibu na wauguzi na madaktari na hali zao za afya na mama yao zinaridhisha na wanaweza kutumia maziwa ya mama,” amesema.

Gharama za lishe

Akizungumzia hilo, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi wa MNH, Dk Living Colma amesema kwa wastani mtoto mmoja atahitaji makopo matano ya maziwa ya watoto kwa mwezi, kwa kuwa maziwa ya mama pekee huenda yasitoshe.

Ili kutosheleza mahitaji ya maziwa kwa watoto wote watano kwa mwezi, anasema familia italazimika kununua makopo 25, ambayo wastani wa bei ya kila kopo ni Sh30, 000 hivyo jumla zitatumika Sh750, 000.

Sambamba na hayo, Dk Colman anasema watoto hao wanaweza kuhitaji nepi takribani 300 kila mmoja kwa mwezi, sawa na nepi 1,500 kwa wote watano. Gharama ya nepi pekee inaweza kuzidi Sh500, 000 kwa mwezi.

Aidha, gharama za mavazi, makazi na kupata watu wa kusaidia malezi zinatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mahitaji ya kuwahudumia watoto hao.

Kuhusu pacha watoto, anasema kitaalamu hutokea mayai mawili au zaidi yanayotolewa katika mzunguko mmoja wa hedhi yanarutubishwa na mbegu za kiume kutokana na tendo la ndoa lililofanyika nyakati tofauti.

“Kupata ujauzito wa watoto watano kwa njia ya kawaida ni jambo nadra sana,” anasema Dk Colman.

Kwa teknolojia ya kisasa na utaalamu uliopo MNH, anasema vimewezesha madaktari kufanikisha kujifungua salama watoto hao katika wiki ya 32 ya ujauzito.

Kutokana na kuzaliwa kabla ya muda wao kutimia, watoto hao wanatarajiwa kubaki hospitalini kwa takribani miezi miwili chini ya uangalizi maalumu, kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Furaha, maumivu

Baba wa watoto hao, Simon Mkwizu anasema uzazi huo ni furaha, lakini ni changamoto kwa familia kwa upande mwingine, akisisitiza atahitaji msaada kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki.

“Tunashukuru Mungu kwa baraka hii, lakini kulea watoto watano kwa wakati mmoja kunahitaji msaada kutoka kwa ndugu, jamaa na watu wenye mapenzi mema,” amesema.

Anasema yeye ni dereva wa bajaji huku mkewe akiwa mama wa nyumbani na kwa hali yao ya kiuchumi hawatamudu gharama zote za kulea watoto hao peke yao.

Mkwizu, amesema mara ya kwanza waligundua kuwa Victoria alikuwa na ujauzito wa watoto wanne alipofikisha miezi mitatu ya ujauzito baada ya kuhudhuria kliniki katika Kituo cha Afya Malecela, Tabata.

“Baadaye tulipelekwa Hospitali ya Amana kwa ufuatiliaji zaidi kabla ya kuhamishiwa Muhimbili,” amesema.

Kwa upande wake, Victoria amesema alilazwa Muhimbili Mei 13 baada ya kuhamishwa kutoka Hospitali ya Amana na tangu wakati huo alikuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.

“Nawashukuru Muhimbili kwa huduma bora walizonipatia. Tangu nilipolazwa Mei 13 nimekuwa nikipata matibabu na uangalizi wa hali ya juu kwa ajili yangu na watoto wangu,” amesema.

Wanahitaji msaada

Akizungumzia hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu ameipongeza timu ya wataalamu wa Muhimbili kwa kufanikisha ujauzito huo kufika wiki ya 32 kabla ya kujifungua.

“Wataalamu wa Muhimbili wamefanya kazi kubwa. Mara nyingi ujauzito wa watoto wengi huishia kati ya wiki ya 27 na 29. Kufika wiki ya 32 kunawaongezea watoto nafasi kubwa ya kuishi na kukua vizuri,” anasema.

Dk Nkungu anasema familia hiyo inahitaji msaada mkubwa wa kifedha na kisaikolojia ili kukabiliana na changamoto za kulea watoto watano waliozaliwa kabla ya wakati.

“Mama anahitaji ushauri nasaha na uangalizi wa karibu. Mwili wake umepitia mabadiliko makubwa wakati wa ujauzito na sasa anakabiliwa na jukumu la kuwalea watoto watano huku akiendelea kupona mwenyewe,” anasema.

Anasema mama huyo anahitaji mwongozo kuhusu lishe bora, muda wa kupumzika na msaada wa kihisia, mambo ambayo yanahitaji rasilimali za kifedha pamoja na upendo kutoka kwa jamii.

“Ni wajibu wetu sote pamoja na Serikali kuisaidia familia hii ili iweze kukabiliana na changamoto za kulea baraka hii waliyopewa,” anasema.

Dk Nkungu anasema watoto hao wanaendelea kupata huduma maalumu Muhimbili wanahitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuepuka matatizo yanayoweza kuhusiana na kuzaliwa kabla ya muda, ikiwamo kutokwa damu kwenye ubongo, matatizo ya macho pamoja na changamoto za mfumo wa fahamu na upumuaji.

“Kutoa huduma za kiwango hiki kunahitaji gharama kubwa na msaada endelevu,” anasema.

Ni tukio la nadra

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk Rachel Mhaville anasema kuzaliwa kwa watoto hao ni tukio la nadra na kipekee lililohitaji usimamizi wa karibu kutoka kwa timu ya wataalamu wa fani mbalimbali, ili kuhakikisha usalama wa mama na watoto.

Alitangaza kuwa Muhimbili itagharamia huduma zote za matibabu kwa Victoria na watoto wake watano kuanzia siku ya kulazwa hadi watakapomaliza matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Pia, amewataka watoa huduma za afya nchini kuendelea kuwapeleka mapema wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa katika hospitali hiyo, kama ilivyofanyika katika tukio hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *