Mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Israel, pamoja na watu mashuhuri kutoka Israel na Marekani, wakuu wa zamani wa mashirika ya usalama, na maafisa kadhaa wa zamani katika taasisi mbalimbali za usalama, wamesaini barua iliyoelekezwa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu jana Jumatano, wakiitaka serikali na mashirika yake kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na kile walichokiita “ugaidi wa Kiyahudi” katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu huko Palestina.

Barua hiyo, iliyoandaliwa na wakili Shmuel Berkowitz, imejumuisha maelezo ya kina kuhusu ukiukwaji wa sheria na mashambulizi yaliyofanywa na Wayahudi wenye msimamo mkali dhidi ya Wapalestina katika miaka ya hivi karibuni, pamoja na mapitio ya kile ambacho waliotia saini wamekitaja kama ongezeko la kutia wasiwasi la kasi ya vitendo hivyo.

Nakala za barua hiyo pia zimetumwa kwa Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Usalama wa Taifa, mawaziri wengine kadhaa, Mkuu wa Wafanyakazi, mkuu wa Shin Bet (Shirika la Usalama la Israel), Inspekta Jenerali wa Polisi, na maafisa wengine wakuu wa utawala huo ghasibu.

Berkowitz ameandika kwa niaba ya waliotia saini kwamba barua hiyo ni “kengele ya hatari na onyo la mwisho. Tunawataka mchukue hatua zote muhimu ili kukomesha mara moja ugaidi wa Kiyahudi ambao umeenea katika Ukingo wa Magharibi katika miaka ya hivi karibuni, na ambao umesababisha mauaji na kujeruhi wanavijiji na wachungaji wa Kipalestina, uharibifu wa kikatili na uporaji wa mali wa mamia ya wahalifu na vijana wa Kiyahudi.”

Waliotia saini barua hiyo wamesema: “Aghlabu ya wahalifu hawa wanaishi katika mashamba na vitongoji vya walowezi, ambavyo vingi havijaidhinishwa na mamlaka husika.” Vitongoji hivyo vilianzishwa karibu na vijiji vya Wapalestina kwa lengo la kuwadhuru na kuwafukuza kwenye makazi yao, kupitia kile kinachoitwa kuliyahudisha eneo la Ukingo wa Magharibi.

Mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Israel, pamoja na watu mashuhuri kutoka Israel na Marekani, wakuu wa zamani wa mashirika ya usalama na taasisi nyingine muhimu za Israel, wanamtaka Netanyahu, Waziri wa Ulinzi, na maafisa wakuu katika taasisi ya usalama na mahakama, kuwaondoa mara moja Wayahudi wote wanaohusika na vitendo vya kigaidi kwenye mipaka ya Ukingo wa Magharibi, na kuwafungulia mashtaka ya kesi ya jinai.

Wito huu ndiyo wenye nguvu zaidi wa aina yake kuhusu suala la ugaidi wa Kiyahudi, na umesainiwa na idadi kubwa ya watu, wakiwemo maafisa kadhaa wa zamani wa ngazi za juu katika serikari ya Israel.

Ujumbe huu unakuja huku kukiwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ugaidi vinavyofanywa na Wayahudi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, hasa unyanyasaji wa kimfumo na ukatili ambao umelazimisha idadi kubwa ya Wapalestina kuhama makazi yao na kutelekezwa jamii nzima, hasa katika Bonde la Jordan.

Miongoni mwa waliotia saini barua hiyo ni pamoja na Mawaziri Wakuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak na Ehud Olmert, wakuu wa zamani wa wafanyakazi Moshe Ya’alon na Dan Halutz, mkuu wa zamani wa Mossad Tamir Pardo, wakuu wa zamani wa Shin Bet Carmi Gillon na Yaakov Peri, mkuu wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa Uzi Arad, Jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Israel, Yoram Danziger, majenerali wa zamani Nitzan Alon, Avi Mizrahi na Gadi Shamni, Mwanasheria Mkuu wa zamani Moshe Lador, pamoja na marabi na wasomi mashuhuri na washindi sita wa Tuzo ya Israel, akiwemo mwandishi David Grossman.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *