DODOMA; Wizara ya Afya imehimiza Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola huku ikisisitiza kuwa bado Tanzania ni salama na wageni kutoka mataifa mengine waje bila hofu.

Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa alibainisha hayo jijini Dodoma alipotoa taarifa kwa kikosi kazi cha wanahabari kuhusu mwenendo wa tishio la ugonjwa wa Ebola na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuzuia na kuimarisha utayari wa nchi kukabili ugonjwa huo.

Aidha, alisema hivi karibuni Tanzania ilitoa vifaatiba kusaidia mapambano dhidi ya Ebola kuungamkono mapambano katika nchi za DRC na Uganda.

“Napenda kuwafahamisha Watanzania kuwa, hadi sasa nchi yetu haina ugonjwa wala wagonjwa na hali ya usalama wa afya nchini iko vizuri,” alisema.

Mchengerwa alisema Serikali inaendelea kuimarisha uwekezaji katika mifumo ya afya yenye uwezo na endelevu ili kuimarisha utayari wa taifa kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa pamoja na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa salama wakati wote huku ikitoa taarifa za hali ya usalama wa afya nchini kwa mashirika ya kitaifa na kimataifa, wadau na balozi za nchi mbalimbali.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inazidi kutambulika kama nchi salama kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na utalii na kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na taharuki za usalama wa afya.

Aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari zaidi na kufuata kanuni za afya kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Ebola kama damu, mate, matapishi, jasho, mkojo, kinyesi cha mgonjwa au mwili wa mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo au vitu/vifaa alivyotumia.

“Aidha, Watanzania waendelee kuepuka kula mizoga ya wanyama, kutoa taarifa ya mhisiwa au msafiri mwenye dalili za ugonjwa huo kwa kupiga simu namba 199 bure na kuwahi katika kituo cha kutolea huduma endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huo,” alisema.

Akaongeza: “Hata hivyo, kutokana na mwingiliano wa watu na shughuli za kijamii na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani, Serikali imeendelea kuchukua hatua za mapema na za kina kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini na imejipanga kikamilifu kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti tishio lolote la kuhatarisha afya ya Watanzania kupitia mifumo yake ya kitaifa ya ufuatiliaji, utambuzi na udhibiti.”

Akizungumzia hatua na juhudi dhidi ya ugonjwa huo, Mchengerwa alisema Serikali imepeleka na kusimika maabara jongezi mbili zenye uwezo wa kupima sampuli za Ebola katika mikoa ya Kagera na Kigoma kusogeza huduma ya upimaji wa sampuli za wahisiwa katika maeneo yanayopakana na nchi zenye mlipuko na Serikali kuimarisha uchunguzi katika maeneo ya kuingilia nchini.

“Tangu kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola, vyombo vya usafiri 101,302 vimekaguliwa na wasafiri 155,897 wamechunguzwa katika mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege na bandari, wakiwemo raia 10,026 kutoka nchi zilizoathirika,” alisema Mchengerwa.

Akaongeza: “Vilevile, wasafiri 4,415 wa safari za kimataifa wamechunguzwa, ambapo 559 walitoka katika nchi zenye mlipuko. Kazi hii inaendelea kuimarishwa katika mipaka na maeneo yote ya kuingilia nchini.”

Kwa mujibu wa Waziri huyo, watoa huduma za afya nchini 45,000 wamejengewa uwezo kupitia mafunzo kwa njia mbalimbali.

Aidha, elimu kuhusu kinga dhidi ya Ebola imetolewa kwa wasafiri, watoa huduma na jamii za mipakani, sambamba na uhamasishaji wa umma kupitia njia na vyombo mbalimbali vya habari na mawasiliano;

“Nchi yetu inaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kikanda na za Bara la Afrika kupitia mikutano ya pamoja ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na wadau wa afya kuimarisha uratibu wa afua za kudhibiti ugonjwa huu. Aidha, tumeendelea kuonesha mshikamano kwa kusaidia juhudi za nchi zilizoathirika kupitia ushirikiano wa kitaalamu, ubadilishanaji wa taarifa na kuimarisha afua za kinga katika mipaka kwa kuwa tunatambua kuwa usalama wa afya wa nchi jirani ni sehemu ya usalama wa afya wa Tanzania,” alisema.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, mafanikio ya kulinda Tanzania dhidi ya Ebola hayategemei Serikali pekee, bali. yanahitaji ushirikiano wa kila mwananchi, viongozi wa jamii, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wote wa maendeleo.

“Huu ni wakati wa kuonesha uzalendo wetu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, kutoa taarifa mapema za wahisiwa na kupuuza taarifa za upotoshaji zinazoweza kuleta hofu au taharuki isiyo ya lazima. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kushiriki katika kulinda Tanzania dhidi ya tishio hili,” alisema.

Hatua nyingine kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, ni Serikali kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege kubaini mapema viashiria vya ugonjwa huo.

“Hadi sasa, jumla ya tetesi 63 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa. Kati ya hizo, wahisiwa 11 walikidhi vigezo, wakachukuliwa sampuli na baada ya kupimwa wakathibitika hawana maambukizi ya Ebola,” alisema.

Alisema na kuongeza kuwa, Serikali ya Tanzania imemarisha utayari wa wataalamu wa kitaifa na vituo vya huduma kote nchini na kuhakikisha kuna upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na tiba muhimu ili kutoa huduma kwa wagonjwa endapo ugonjwa utaingia nchini.

“Serikali imehakikisha kuna upatikanaji wa kutosha wa mavazi maalumu ya kinga, vifaatiba na vifaa vingine muhimu kwa watoa huduma wa afya waliopo mstari wa mbele. Hadi sasa, seti za kutosha za mavazi hayo zipo katika Bohari ya Dawa (MSD) na mikoa yote kwa ajili ya matumizi ya dharura,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri, hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha hakuna mhudumu wa afya anayepata maambukizi au kupoteza maisha akiwa katika jukumu la kuokoa maisha ya wengine.-

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *