
Ugonjwa wa sasa wa Ebola, ambao ulizuka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda mwezi uliopita, ni matokeo ya kuenea kwa wanyamapori. Haya yameelezwa na wanasayansi kutoka nchi hizo mbili jana Alhamisi.
Wanasayansi hao wamepinga uvumi kwamba aina ya sasa ya Ebola inaweza kuhusishwa na mlipuko wa zamani ambao ulikuwa haujajitokeza au ambao unaendelea kusambaza maamukizi bila ya kutambuliwa.
Wanasayansi kutoka Idara ya Maabara ya Taifa ya Afya na Huduma za Uchunguzi ya Wizara ya Afya ya Uganda na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba ya Kongo wamesema kuwa matokeo ya uchunguzi wao yameonyesha kuwa virusi vya ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo vinatofautiana kwa upande wa vinasaba na milipuko ya awali.
Kongo imeripoti zaidi ya kesi 800 zilizothibitishwa za Ebola, ikiwa ni pamoja na vifo vya 196, tangu mlipuko uliosababishwa na aina ya Bundibugyo ya Ebola ilipotangazwa, Mei 15 mwaka huu.
Uganda kwa upande wake imeripoti kesi 19 zilizothibitishwa, ikiwa ni pamoja na vifo vya watu wawili.
Wanasayansi hao wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano, wakisema kazi ya pamoja ya kuvuka mipaka inawasaidia wafanyakazi wa sekta ya afya kufuatilia harakati za virusi, kuandaa hospitali na kulinda jamii za watu wanaoishi katika maeneo ya mpakani ambapo wanaingia na kutoka kila siku.
Imeelezwa kuwa nchini Kongo, virusi vinaenea katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, huku Ituri ikiwa na karibu asilimia 95 ya kesi za maambukizi ya Ebola.