Chanzo cha picha, Reuters
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Makamu wa rais wa Marekani JD Vance, amekuwa mstari wa mbele kutetea makubaliano ya Marekani na Iran na kupuuzia swali kuwa Rais Donald Trump amemweka kuwa mbeba lawama katika makubaliano hayo ambayo hayaungwi mkono na baadh ya viongozi wa chama cha Republican.
“Nadhani rais alikuwa anatania tu” Vance alijibu kuhusu semi za Trump ambapo alisema atamlaumu yeye iwapo makubaliano kati yao na Iran yataporomoka.
Vance amekuwa mstari wa mbele wiki nzima kutetea hati hiyo ya makubalino kati ya Marekani na Iran.
Ingawa Trump amekuwa akitoa semi kinzani kuhusu mkataba huo, kuhairisha safari yake ya kwenda Uswizi kwa sherehe za kutia Saini mkataba huo, kunaashiria kuwa Vance hana udhibiti wowote kuhusu swala hilo.
Ikulu ya White House alhamisi, ilitangaza kuwa Vance hatasafiri kuelekea Uswizi.
Licha ya hilo, Vance bado alitetea makubaliano ya Marekani na Iran.
Ila wakati huu si rahisi kwa Vance ambaye ameonyesha dalili ya kuwania Urais mwaka wa 2028.
Imekuwa vigumu kwake kuwarai watu kuunga mkono makubaliano haya ya muda kwa chama ambacho kimegawanyika kati ya wafuasi wa MAGA wanaopinga uingiliaji wa kijeshi na ambao walipinga vita tangu mwanzo, na wahafidhina wenye msimamo mkali dhidi ya Iran wanaoamini kuwa Ikulu ya White House imesalimu amri ya Tehran.
Chanzo cha picha, GETTY
Maafisa wengine katika serikali ya Trump, hawakabiliwi na shinikizo kama lile analokumbana nalo Vance kuhusu Iran.
Waziri wa Mambo ya Kigeni, Marco Rubio, ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wanaoweza kuwania uongozi wa chama cha Republican mwaka wa 2028, amejitahidi kujiepusha na mjadala kuhusu vita hivi.
Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, amekuwa mtetezi mkubwa wa operesheni ya kijeshi, lakini hajahusika kwa kina katika mazungumzo ya kidiplomasia ya kumaliza mzozo huo. Pia si sura ya makubaliano haya kama alivyo Vance.
Baadhi ya wanachama wa Republican wanasema jukumu la Vance katika suala la vita vya Iran limegeuka kuwa kazi isiyo na shukrani kutoka kwa rais ambaye kwa muda mrefu amejulikana kwa kuwatupia lawama wasaidizi wake pale sera zake zisipopokelewa vizuri na umma.
“Si kawaida ya rais kuachia wengine nafasi ya kung’ara, lakini amefanya hivyo katika suala hili,” alisema mwanamikakati wa Republican, Matt Mackowiak. “Hilo linaonekana kuwa uamuzi wa maksudi.”
Mwanaharakati mmoja mkongwe wa Republican na mkosoaji wa rais alisema kuwa Donald Trump anajaribu kumbebesha Vance jukumu la mafanikio au kushindwa kwa makubaliano hayo.
Chanzo cha picha, EPA
Huenda uhusiano wa J. D. Vance na vita vya Iran vitamgharimu kisiasa.
Iwapo nchi husika zitafikia makubaliano ya mwisho ya amani yatakayodhibiti mpango wa nyuklia wa Iran, Vance atakuwa amechangia kwa kiwango kikubwa kufanikisha lengo ambalo Marekani na washirika wake wa Mashariki ya Kati wamekuwa wakilifuatilia kwa miaka mingi.
Hata hivyo, hakuna uhakika kwamba pande hizo mbili zitafanikisha makubaliano ya mwisho kuhusu masuala mbalimbali ya kiufundi ndani ya siku 60 zijazo, au kwamba makubaliano ya muda mrefu yatatosheleza matamanio ya wakosoaji wa ndani na wa kimataifa.
“Kumtwika Vance jukumu la vita vya Iran ni njia nyingine ambayo wakosoaji watatumia kumwajibisha kwa sera na siasa za Trump,” alisema mshauri mkongwe wa Republican, Terry Holt.
Utawala wa Donald Trump ulitangaza kwamba Iran ilikuwa imekubali hati ya makubaliano ya awali siku ya Jumapili, lakini haukuweka hadharani maelezo ya makubaliano hayo.
Kutokuwepo kwa ufafanuzi wa kutosha kulisababisha mkanganyiko kuhusu kile kilikuwa kimeandikwa katika makubaliano hayo.
Kufuatia hali hiyo, J. D. Vance alijaribu kuondoa mkanganyiko huo kupitia mahojiano kadhaa.
Katika mahojiano na shirika la habari la CBS News siku ya Jumatatu, Vance alisema kwamba Iran fursa inaweza kunufaika na mfuko wa dola bilioni 300 za Marekani kwa ajili ya ujenzi upya wa nchi hiyo, ikiwa itaheshimu masharti ya makubaliano yake na Marekani.
Hata hivyo, saa chache baadaye, Donald Trump alitoa tafsiri tofauti. Kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, aliita madai ya mfuko huo wa dola bilioni 300 kuwa “habari za uongo” na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, “hatutatoa hata senti 10.”
Baadaye, maandishi ya makubaliano yalipotolewa rasmi na maafisa wa Marekani, yalijumuisha kifungu kinachoeleza kuwa Marekani itashirikiana “na washirika wa kikanda kuandaa mpango wa mwisho uliokubaliwa na pande zote wenye thamani ya angalau dola bilioni 300 za Marekani” kwa ajili ya ujenzi upya wa Iran. Hata hivyo, kifungu hicho hakikusema wazi kwamba fedha hizo zingetolewa moja kwa moja na Marekani.
Kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, J. D. Vance alirudia kauli ya Donald Trump kwamba makubaliano ya muda yalikuwa hatua muhimu ya kwanza kuelekea kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.
Wakati Vance anabishana na Whoopi Goldberg kwenye kipindi cha ABC The View, Donald Trump alikuwa akikutana na viongozi wa dunia katika mkutano wa G7 katika mji wa Évian-les-Bains Ufaransa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari siku ya Jumatano, Trump alirudia kauli kuwa angemlaumu J. D. Vance iwapo makubaliano ya Iran yatashindwa.
Maswali yaliibuliwa kuhusu kwa nini Vance alihitajika baadaye kufanya tukio tofauti la utiaji saini wake huko Geneva.
Swali hilo lilijibiwa baadaye pale Ikulu ya White House ilipotangaza kwamba Vance hataenda Geneva,angalau kwa sasa,wakati maandalizi ya mazungumzo na Iran bado hayajakamilika.
Wakati Trump akiwa bado nje ya nchi, Vance anaendelea kutetea makubaliano hayo huku wenzake wa zamani katika Seneti wakiyakosoa kwa madai kwamba inawanufaisha Iran.