Kigoma. Serikali Mkoa wa Kigoma imezindua Mkakati wa Usafi wa Mazingira wa miaka mitatu unaolenga kudumisha mazingira safi na salama pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za usafi katika kaya, taasisi za umma, shule na vituo vya afya.

Mkakati huo, utakaoanza kutekelezwa kuanzia Juni 2026 hadi Juni 2029, unalenga kupunguza na kudhibiti magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama na usafi duni, kama vile kipindupindu, kuhara, homa ya matumbo (typhoid) na magonjwa mengine ya mlipuko.

Malengo mengine ya mkakati huo ni kutokomeza vitendo vya kujisaidia haja kubwa ovyo, kuboresha usalama wa maji ya kunywa kupitia ulinzi wa vyanzo vya maji, usimamizi wa ubora wa maji na matumizi salama ya maji katika ngazi ya kaya.

Aidha, mkakati huo unalenga kuhamasisha unawaji wa mikono kwa sabuni, kuimarisha usimamizi wa taka ngumu na majitaka pamoja na kuboresha hali ya usafi wa mazingira kwa ujumla.

Mkakati huo uliozinduliwa Alhamisi Juni 18, 2026,  pia unatarajiwa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi, mashirika ya kiraia na jamii katika utoaji na usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro (wa nne kutoka kushoto), akiwa na baadhi ya Wakuu wa Wilaya pamoja na wakuu wa idara mkoani humo wakionesha mkakati wa usafi wa mazingira uliozinduliwa kwa lengo la kutokomeza magonjwa yatokanayo na usafi duni na matumizi ya maji yasiyo salama.

Vilevile, utaimarisha ufuatiliaji na uwajibikaji wa wadau wa sekta ya maji na usafi katika ngazi ya mkoa na halmashauri.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amesema utekelezaji madhubuti wa mkakati huo utasaidia kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, kuboresha matumizi ya vyoo bora na vya kudumu pamoja na kuhakikisha maeneo ya mijini na vijijini yanakuwa safi wakati wote.

Amesema mafanikio ya mkakati huo yatategemea ushirikiano wa viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali katika kusaidia wataalamu wa afya kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira.

Ofisa Usafi na Mazingira Mkoa wa Kigoma, Nesphory Sungu, amesema licha ya asilimia 65 ya wakazi wa mkoa huo kutumia vyoo bora, bado wananchi wengi wanatumia maji yasiyo safi na salama, hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa magonjwa ya tumbo.

“Kwa takwimu tulizonazo, ni asilimia 34 pekee ya wakazi wa Mkoa wa Kigoma wanaozingatia utaratibu wa kutibu maji kwa njia mbalimbali kabla ya kuyatumia. Hivyo, mkakati huu unalenga kutoa hamasa na kubadilisha tabia za wananchi ili waanze kutumia maji safi na salama,” amesema Sungu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Mkoa wa Kigoma, Justus Ndenzako amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika kila hatua ya utekelezaji wa mkakati huo ili kuhakikisha unakuwa endelevu na wenye matokeo chanya.

“Napenda kusisitiza kuwa dhamira ya UNICEF ni kuendeleza mpango huu kwa kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mamlaka za Serikali za mitaa, sekta binafsi na wananchi wa Kigoma ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Ndenzako.

Mkakati huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na UNICEF, na unahusisha wilaya zote za Mkoa wa Kigoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *