
Walinzi wa mpaka wa pamoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Iraq wamefanya vikao vya pamoja katika mpaka wa eneo la Mehran katika mkesha wa kuanza rasmi wimbi kubwa la mazuwwar wa Muharram na Arbaeen.
Brigedia Jenerali Ali Nadarkhani, Kamanda wa Walinzi wa Mpakani katika Mkoa wa Ilam, amesema leo Ijumaa katika kikao na Kamanda wa Walinzi wa Mipaka ya Eneo la Tatu la Iraq, kufuatia kuongezeka kiwango cha uratibu wa usalama kati ya Iran na Iraq katika mkesha wa Arbaeen, kwamba: Kupiga doria za pamoja na kushirikiana nyanjani kati ya askari wa nchi mbili kutatayarisha uwanja salama wa ushirikiano wa nchi mbili hizi katika kuaanda mazingira ya kufanyika vyema safari za marasimu ya Muharram na Arbaeen kupitia mpaka wa Mehran.
Brigedia Jenerali Nadarkhani amesema: Ushirikiano wa pande mbili kati ya vikosi vya mpakani vya nchi hizi mbili umekuwa ukiongezeka katika miezi ya hivi karibuni, na kwamba utekelezwaji wa doria zilizoratibiwa katika ukanda wa mpakani umekuwa na taathira inayofaa katika kuimarisha usalama na udhibiti bora wa mipaka.
Akiashiria umuhimu wa kuwepo uratibu wa kudumu baina ya walinzi wa mpaka wa Iran na Iraq amesema: Kuwepo uwanjani na kupiga doria za pamoja katika maeneo ya mipakani mbali na kuboresha kiwango cha usalama kumeharakisha upashanaji habari na kuongeza utayarifu wa kioperesheni wa pande mbili.
Kamanda wa walinzi wa mpaka wa mkoa wa Ilam amesema Muharram na Arbaeen ya Imam Hussein (as) ni matukio makubwa ya kidini katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza: “Mpaka wa Mehran, ikiwa njia kuu ya mazuwwar, unahitajia mipango makini na uratibu wa kina baina ya vyombo husika katika nchi mbili hizi.”