Shirikisho la Soka la Iran limetangaza kuwa limewasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kufuatia kukataliwa kwa mara ya pili mfululizo kwa mipango ya maandalizi ya Timu ya Taifa ya Iran, Team Melli.

Malalamiko hayo yanakuja baada ya maafisa wa Iran kusema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Marekani vimezuia tena timu ya taifa kusafiri kwenda mji mwenyeji wa mechi kulingana na ratiba iliyokuwa imeidhinishwa mapema. Kombe la Dunia la FIFA la mwaka 2026 linaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico.

Iran ilikuwa imeiarifu FIFA mapema kuhusu mpango wake wa maandalizi kabla ya mashindano hayo. Kwa mujibu wa mpango huo, benchi la ufundi lilipendekeza timu ifike katika kila mji wa mechi siku mbili kabla ya mchezo na irejee kambini siku inayofuata baada ya mechi, ili kuhakikisha maandalizi bora ya kimwili na kiufundi.

Hata hivyo, shirikisho hilo linasema mpangilio huo haukuheshimiwa katika mechi ya ufunguzi ya Iran dhidi ya New Zealand. Badala ya kufika siku mbili kabla ya mchezo, timu iliruhusiwa kusafiri siku moja tu kabla, na ikaamriwa kurejea makao yake huko Mexico mara tu baada ya kumalizika kwa mechi.

Kwa mujibu wa shirikisho hilo, vikwazo hivyo hivyo sasa vimewekwa tena kabla ya mechi ya pili ya Iran dhidi ya Ubelgiji.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa Los Angeles siku ya Jumapili saa sita mchana saa za huko. Ili kuwapa wachezaji muda zaidi wa kuzoea mazingira ya eneo hilo, kufanya mazoezi ya mwisho na kukamilisha maandalizi, maafisa wa Iran waliomba timu iruhusiwe kusafiri kwenda Los Angeles siku mbili kabla ya mchezo kuanza.

Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa licha ya kuwepo kwa sababu za wazi za kiufundi zilizounga mkono pendekezo hilo.

Kutokana na hali hiyo, Team Melli italazimika kusafiri kwenda Los Angeles siku ya Jumamosi, siku moja tu kabla ya mechi.

Shirikisho la soka la Iran limesema hatua hizo hazilingani na kanuni ya kutoa mazingira sawa kwa timu zote zinazoshiriki, na zinaweza kuathiri maandalizi ya kiufundi ya timu za taifa.

Shirikisho la soka la Iran limeongeza kuwa haliridhishwi na uamuzi huo na litaendeleza suala hilo kupitia njia rasmi ndani ya FIFA.

Mvutano huu wa karibuni unafuatia ukosoaji uliotolewa mapema na kocha mkuu wa Iran, Amir Ghalenoei, ambaye alisema kuwa Marekani imekuwa ikiibagua timu ya taifa ya Iran na kuweka vikwazo vya ziada katika kipindi chote cha mashindano.

Akizungumza baada ya mechi ya kwanza ya Iran dhidi ya New Zealand mapema wiki hii, Ghalenoei alisema: “Team Melli iko katika hali ngumu sana. Hatukupewa muda wa kutosha wa maandalizi na kutulia, na hata baada ya mechi tunalazimishwa kurejea mara moja Tijuana, Mezico. Hali hii iinatuweka chini ya shinikizo kubwa.”

Kocha huyo alibainisha kuwa awali Iran ilikuwa imepanga kuweka kambi yake ya mazoezi mjini Tucson, jimbo la Arizona, lakini ililazimika kuhamia Tijuana nchini Mexico kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani

Aliongeza kusema: “Wamechelewesha nyakati za kuwasili kwetu, na sasa wanatulazimisha kurejea mapema bila muda wa kutulia. Wanazidi kufanya hali iwe ngumu zaidi kwa kutuwekea vikwazo zaidi. Lakini hatutaruhusu hilo lituzuie kufanya kila tuwezalo.”

Ghalenoei alisisitiza pia kuwa: “Ndiyo maana ninaamini sisi ndio timu inayodhulumiwa zaidi katika Kombe la Dunia hili.”

Licha ya changamoto hizo za karibuni, Shirikisho la Soka la Iran limesema timu ya taifa itaendelea na maandalizi yake huku ikibaki makini kikamilifu kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Ubelgiji mjini Los Angeles.

Katika mechi yake ya kwanza ya Kundi G, Iran ilitoka sare ya mabao 1–1 dhidi ya New Zealand.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *