Marekani. Staa wa filamu kutokea Uingereza, Tom Holland (30), amethibitisha kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Zendaya (29), ikiwa ni baada ya miezi kadhaa ya tetesi kuhusu uwepo wa ndoa yao ya siri.
Ametoa uthibitisho huo katika mahojiano na Jarida la Esquire, wakati akizungumzia picha bandia zilizotengenezwa kwa teknolojia ya akili unde (AI), picha zilizodai wawili hao walifanya harusi yao huko Como, Italia.
Holland amesema bibi yake alipoona picha hizo alidhani hakualikwa kwenye harusi. Lakini ukweli ni kwamba picha hizo hazikuwa halisi ila tukio lenyewe lilifanyika na wanafamilia wote walishiriki.
Hata hivyo, awali Zendaya wakati akiitangaza filamu yake, The Drama kwenye kipindi cha Jimmy Kimmel Live!, alikwepa kutoa majibu ya moja kwa moja kuhusu uvumi wa wao kufunga ndoa.
Kauli ya Holland imekuja takribani miezi mitatu baada ya mbunifu wa mitindo wa muda mrefu wa Zendaya, Law Roach kudai kwamba mastaa hao walifunga ndoa na kufanya harusi kabisa.
Ingawa Holland hakutoa maelezo zaidi kuhusu harusi yao, alizungumza kwa furaha kubwa jinsi Zendaya alivyoleta mabadiliko chanya katika maisha yake.
Alisema kuwa na uhusiano imara na mtu anayeelewa maisha yao ya umaarufu ni jambo la thamani kubwa, na kwamba Zendaya ni mtu anayemuunga mkono na kumpa usalama katika kazi zake za sanaa.
Vilevile Holland alitoa sifa nyingi kwa Zendaya akisema amempata mwenza sahihi kabisa wa maisha ambaye pia ni rafiki yake mkubwa kiasi kwamba hajawahi kuwa na furaha kama aliyonayo kwa sasa.
“Kwa upande wangu, nimempata mtu ambaye nimeridhika naye. Yeye ni rafiki yangu wa karibu zaidi, na sijawahi kuwa na furaha kama ninavyokuwa ninapokuwa naye,” alisema Tom na kuongeza.
“Tunaweza kusaidiana kwa namna ambazo ni sisi tu ndio tunaweza, kwa sababu ni sisi tu tunaelewa namna ya kuishi katika haya maisha yetu. Na nafikiri hilo ni jambo la kipekee sana, kwa sababu sijui ningewezaje kupata kitu kama hicho na mtu mwingine,” alieleza.
Wawili hao waliotangaza kuchumbiana mnano Januari 2025, kwa sasa wapo katika ziara ya kuzitangaza filamu zao mpya zijazo, The Odyssey na Spider-Man: Brand New Day, ambazo zinatarajiwa kuanza kuonyeshwa katika kundi za sinema hapo Julai.
Mbali na hayo, Zendaya na Holland walionekana pamoja kwenye zulia jekundu huko Madrid, Hispania mapema wiki hii ikiwa ni mara ya kwanza baada ya takribani miaka mitano.
Hadi sasa filamu ambazo Holland amecheza kama mwigizaji mkuu zimeingiza mapato ya zaidi ya Dola9.9 bilioni, wastani wa Sh25.9 trilioni, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa waigizaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani.
Naye Zendaya kutokea Marekani ambaye alianza kujulikana tangu akiwa mdogo kupitia vipindi vya Disney, hadi sasa filamu zake zote alizocheza kama mwigizaji mkuu zimeingiza zaidi ya Dola3.9 bilioni, wastani wa Sh10.1 trilioni.