DODOMA: MGANGA Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) na Waganga Wakuu wa Wilaya (DMOs) kuhakikisha wanaendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia Programu ya Kukuza Huduma za Uzazi wa Mpango (SuFP) hata baada ya kufungwa rasmi kwa mradi huo.
Dk Magembe alitoa maelekezo hayo juzi Jijini Dodoma wakati wa kongamano la kujifunza na kutathmini mafanikio ya miaka tisa ya utekelezaji wa programu hiyo iliyolenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango nchini.
Alisema viongozi hao wa sekta ya afya hawakualikwa kushiriki hafla hiyo kwa ajili ya kushuhudia kufungwa kwa mradi pekee, bali kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaingizwa katika mipango na bajeti za mikoa na halmashauri ili huduma ziendelee kutolewa bila kukwama.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Will Guest alisema Serikali ya Uingereza itaendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha afya ya uzazi na haki za wanawake na wasichana.
Alisema kupitia SuFP, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 5.2 walifikia huduma za uzazi wa mpango, hatua iliyosaidia kuzuia zaidi ya vifo vya wajawazito 6,500 na mimba zisizotarajiwa milioni 8.3.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa MSI Tanzania, Dk Stephen Mutegeki alisema programu hiyo imeonyesha kuwa maendeleo makubwa yanawezekana pale wadau mbalimbali wanaposhirikiana katika kufikia malengo ya pamoja.
Alisisitiza kuwa MSI Tanzania itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelezwa na kwamba huduma bora na zenye usawa za afya ya uzazi zinaendelea kuwafikia wananchi wote.

Akizungumza kwa niaba ya washirika wa utekelezaji, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini, Mark Bryan Schreiner alisema mafanikio ya programu hiyo yamethibitisha kuwa maendeleo makubwa yanawezekana pale serikali, watoa huduma, washirika wa maendeleo na jamii wanaposhirikiana.
Programu ya SuFP iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2017 hadi 2026 kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia FCDO, ilitekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na taasisi za EngenderHealth, UNFPA, MSI Tanzania na Pathfinder International.