Mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonya dhidi ya kuwa na matumaini kupita kiasi kuhusu mazungumzo na adui, akitaja historia yake ya kuvunja ahadi.

Jenerali mstaafu Mohsen Rezaei aliyasema hayo katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X siku ya Jumapili, wakati wawakilishi wa  ngazi ya juu kutoka Iran na Marekani wakiwa wamewasili Uswisi kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa Waraka wa Makubaliano (MoU) uliosainiwa hivi karibuni kati ya nchi hizi mbili. Mapatano hayo yanakusudia kumaliza kabisa vita haramu vya uchokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Rezaei, ambaye aliwahi kuwa kamanda mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), amesema: “Marekani ilipaswa kuilazimisha Iran isalimu amri kupitia mkakati wake wa ‘amani kupitia nguvu’.”

Ameongeza kuwa: “Sasa kwa kuwa wameshindwa, wanasisitiza kufanya mazungumzo kwa sababu ya kukata tamaa.”

Pia ameonya kuwa: “Adui ameonyesha kwamba ni mvunja ahadi. Ni lazima tuwe waangalifu; matumaini yoyote kupita kiasi yatatumiwa vibaya na adui.”

Wakati huo huo Spika wa Bunge la Iran amesisitiza tena kwamba atatetea haki za Wairani waliouawa shahidi wakati wa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu baada ya kuwasili Uswisi kufuatilia mkataba wa Hati ya Maelewano uliosainiwa na viongozi wa nchi mbili kwa lengo la kukomesha vita.

Mohammad Baqer Qalibaf amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X alipowasili Zurich akiongoza ujumbe wa Iran wa mazungumzo ya jinsi ya kutekeleza yaliyomo kwenye hati ya makubaliano hayo, ambayo yalitiwa saini hivi karibuni kati ya marais wa Jamhuri ya Kiislamu na Marekani.

Ujumbe huo, ambao unajumuisha Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araqchi, unatarajiwa kufanya majadiliano na Wamarekani kuhusu jinsi ya kutekeleza majukumu yaliyokubaliwa na pande hizo mbili kwenye Waraka wa Makubaliano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *