KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema ushindi walioupata dhidi ya Yanga kwenye nusu fainali ya Kombe la CRDB haujafunga hesabu dhidi ya wapinzani wao hao, kwani bado wanakutana tena kwenye mechi muhimu ya Ligi Kuu Bara.

Azam imetinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga Yanga kwa mabao 3-2 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Lakini, Ibenge amesema kikosi chake hakina muda wa kusherehekea kwa sababu kinapaswa kujiandaa kwa pambano jingine kubwa litakalopigwa Juni 24, Zanzibar.

Kocha huyo raia wa DR Congo amesema nguvu zote  wanazielekeza katika kuhakikisha wachezaji wanarejea kwenye kiwango bora cha utimamu kabla ya mchezo huo ambao unaweza kuamua mbio za ubingwa na nafasi za juu za msimamo wa ligi.

“Tumepata ushindi muhimu na tumefuzu fainali, lakini kazi bado haijaisha,” amesema Ibenge na kuongeza:

 “Tunakutana tena na Yanga baada ya siku chache, hivyo tunapaswa kurudidha utimamu na kujiandaa vizuri.”

Mchezo huo wa ligi ni muhimu zaidi kwa Yanga ambao wanaongoza msimamo kwa pointi 66, wakifuatiwa na Simba wenye pointi 64 huku Azam wakiwa nafasi ya tatu na pointi 58.

Yanga inahitaji matokeo mazuri ili kuendelea kujihakikishia nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa ligi, wakati Azam ikisaka kumaliza katika nafasi za juu zitakazoipa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Ushindi wa Azam dhidi ya Yanga umefuta matumaini ya mashabiki  waliokuwa wakisubiri uwezekano wa kushuhudia dabi ya tano ya Kariakoo msimu huu katika fainali ya Kombe la CRDB.

Katika mchezo huo, Azam imeonyesha uimara wa kiufundi na kimbinu huku ikifanikiwa kushinda licha ya kumaliza sehemu ya mchezo ikiwa na mchezaji mmoja pungufu kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa beki Yoro Diaby.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *