
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mzambia Joshua Mutale ‘Budo’ amebakia njia panda baada ya Klabu ya Al Adalah Club ya Saudi Arabia aliyokuwa akicheza kwa mkopo msimu wa 2025-2026, kudaiwa haina mpango pia wa kumsajili nyota huyo moja kwa moja.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 1, 2024, akitokea Power Dynamos ya kwao Zambia, ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo waliotolewa kwa mkopo dirisha dogo la Januari 2026, ili kupisha wengine kwa ajili ya kuongezea nguvu kikosini humo.
Hatua ya mchezaji huyo kujiunga na Al Adalah Club ya Saudi Arabia ilijiri baada ya dili lake la kujiunga na Kenya Police FC ya Kenya ili kuungana na nyota mwenzake, Awesu Awesu aliyejiunga na kikosi hicho Januari 2026, kushindwa kukamilika.
Hata hivyo, baada ya dili la nyota huyo kwenda Kenya kuonekana gumu, Al Adalah Club iliyoanzishwa mwaka 1984, ikiwa na miaka 42, ilionyesha nia ya kumsajili ili kuitumikia kwa mkopo, huku pia kukiwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja.
Baada ya Budo kuichezea Al Adalah Club kwa miezi sita taarifa zinaeleza uongozi wa timu hiyo hauna mpango wa kumsajili tena moja kwa moja, huku kwa Simba ikiwa haina nia ya kumrudisha jambo linalompa nafasi ya kutufata sehemu nyingine.
Wakati nyota huyo anajiunga na Simba alisaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwingine mmoja zaidi, japo hadi sasa vigogo hao hawana tena mpango naye, jambo linalomfungulia mlango wa kutafuta timu nyingine ya kuichezea.
Katika Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia msimu wa 2025-2026, Al Adalah Club imemaliza nafasi ya 14 na pointi 33, kati ya timu 18, baada ya kikosi hicho kushinda mechi nane tu, sare tisa na kupoteza 17, kikifunga mabao 44 na kuruhusu 70.