Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Morogoro, imewaachia huru Thomas Komba na Clarence Francis waliokuwa wakitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la wizi wa kutumia silaha, baada ya kubaini upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yao kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Katika kesi ya msingi, warufani hao walidaiwa Julai 6, 2024 katika Kitongoji cha Mbegesela, kilichopo Kijiji cha Ikombe, Kata ya Mikumi wilayani Kilosa, kutenda kosa la wizi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu.

Walidaiwa siku ya tukio waliiba Sh8 milioni mali ya Hamis Ndemeka na kabla ya wizi huo walimtishia mwathirika wa tukio hilo kwa kutumia panga ili kupata fedha hizo.

Mahakama ya Wilaya ya Kilosa iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo ya jinai, iliwatia hatiani watu hao wawili na kuwahukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.

Hukumu iliyowaachia huru ilitolewa Juni 19, 2026 na Jaji Stephen Magoiga aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyokuwa imekatwa na warufani hao wakipinga adhabu hiyo na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Jaji Magoiga amesema baada ya kupitia mwenendo na kusikiliza pande zote mbili za rufaa, Mahakama imebaini mbali na dosari za ushahidi, pia kuna makosa ya kisheria yaliyofanyika wakati wa kusikilizwa kwa utetezi katika Mahakama ya Wilaya.

Mahakama ilieleza kuwa, warufani na mashahidi wao walitoa ushahidi bila kula kiapo au kuthibitisha kauli zao kama sheria inavyotaka.

Katika rufaa hiyo, warufani hao walipinga hukumu hiyo kwa sababu nane, wakiomba Mahakama Kuu kufuta hukumu ya kifungo cha miaka 30 wakidai kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwa mlalamikaji walikuwa na fedha hizo zinazodaiwa kuibiwa siku ya tukio.

Walidai hakuna ushahidi wa kutosha ulioonesha fedha hizo zilikuwepo wala namna zilivyochukuliwa.

Pia, walidai Mahakama ya Wilaya ilishindwa kuchambua ipasavyo ushahidi wa utetezi wao, hususan nyaraka zilizoonesha kuwapo kwa mgogoro wa ardhi kati yao na mlalamikaji.

Kwa mujibu wao, mgogoro huo uliibua shaka kuhusu uhalali wa tuhuma zilizokuwa zikielekezwa dhidi yao.

Aidha, warufani walipinga kutegemewa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka wakisema ulikuwa na mapungufu na tofauti katika maelezo muhimu ya tukio.

Walidai baadhi ya maelezo yaliyotolewa na mlalamikaji hayakuungwa mkono na mashahidi wengine waliodaiwa kuwapo eneo la tukio.

Sababu nyingine ni kuwa uchunguzi wa kesi haukufanyika kwa umakini kwa kuwa, tukio liliripotiwa awali kama shambulio kabla ya kubadilishwa na kuwa wizi wa kutumia silaha.

 Walibainisha kuwa, hakuna fedha, silaha wala mfuko uliodaiwa kubeba fedha hizo uliowahi kupatikana au kuwasilishwa mahakamani kama vielelezo vya kuthibitisha shtaka hilo.

Uamuzi wa Mahakama

Katika uchambuzi wake, Jaji Magoiga amesema moja ya masuala makubwa yaliyoibua shaka ni namna tukio hilo lilivyoripotiwa awali polisi kama shambulio na baadaye kubadilishwa kuwa kesi ya wizi wa kutumia silaha karibu mwaka mmoja baada ya tukio kutokea.

Mahakama imebaini kuwa, ofisa mpelelezi wa kesi hiyo, ambaye pia alikuwa ofisa wa kwanza kumpokea mlalamikaji siku ya tukio na kumpeleka hospitalini, hakueleza kwa nini mwanzoni hakukuwa na taarifa yoyote kuhusu madai ya kuibwa fedha.

Jaji Magoiga amesema ushahidi wa ofisa huyo ulionesha kuwa wakati mlalamikaji alipofika kituoni alipewa fomu namba tatu ya Polisi (PF3) na kupelekwa hospitalini kutokana na jeraha la kichwa, lakini hakuna maelezo kwamba aliripoti kuibiwa fedha.

“Kutokuwepo kwa maelezo ya namna madai ya wizi wa fedha hizo yalivyojitokeza baadaye kunazua shaka kubwa kuhusu uhalali wa shtaka la wizi wa kutumia silaha,” amesema jaji huyo katika hukumu yake.

Mahakama pia iliona dosari katika kucheleweshwa kwa kufunguliwa kwa kesi hiyo ambapo rekodi zilionesha warufani walikamatwa Julai 6, 2024 na kupewa dhamana ya polisi lakini walifikishwa mahakamani Juni 25, 2025, karibu mwaka mmoja baadaye.

Kwa mujibu wa Jaji Magoiga, upande wa mashtaka haukutoa maelezo yoyote ya kuridhisha kuhusu kuchelewa huko, hali iliyodhoofisha zaidi kesi yao.

Alinukuu maamuzi mbalimbali ya Mahakama za juu yaliyoeleza kuwa kila kipindi cha kucheleweshwa kwa kufikishwa kwa mtuhumiwa mahakamani lazima kielezwe kwa sababu za msingi, vinginevyo haki ya mtuhumiwa inaweza kuathiriwa.

Mahakama pia ilichunguza suala la ushahidi wa mali zinazodaiwa kuibwa na silaha iliyotumika katika tukio hilo.

Ingawa upande wa mashtaka ulieleza kuwa si lazima kila wakati silaha au mali iliyoibwa iwasilishwe mahakamani kama kielelezo, Jaji Magoiga amesema mazingira ya kesi hiyo yalihitaji maelezo ya kina zaidi.

Amesema hakuna ushahidi ulioonyesha kuwapo panga lililotajwa, mfuko uliodaiwa kuwa na fedha hizo wala fedha zenyewe ziliwahi kupatikana au kufuatiliwa na polisi.

Aidha amesema hakuna ushahidi ulioonesha kuwa warufani walikamatwa wakiwa na mali hizo au kwamba walifanyiwa upekuzi uliobaini vitu vinavyohusishwa na kosa hilo.

“Katika mazingira ya kesi hii, kushindwa kufuatilia au kueleza hatima ya vitu muhimu vinavyodaiwa kuhusika katika tukio kunatia doa kesi ya upande wa mashtaka,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Suala jingine lililojadiliwa ni chanzo cha majeraha aliyopata mlalamikaji ambapo upande wa mashtaka ulidai jeraha hilo lilitokana na kukatwa kwa panga, lakini Mahakama ilibaini kuwa ofisa aliyefika eneo la tukio aliona pia vipande vya kioo vilivyovunjika pamoja na damu katika eneo hilo.

Kutokana na ushahidi huo, Jaji amesema haiwezekani kuhitimisha kwa uhakika kuwa majeraha hayo yalitokana na panga pekee kama ilivyodaiwa.

Mahakama pia iliona kuwepo kwa tofauti kadhaa katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka shahidi aliyedai kumwona mmoja wa warufani akimpiga mlalamikaji, jambo ambalo mlalamikaji mwenyewe hakulieleza katika ushahidi wake.

Kwa mujibu wa Jaji Magoiga, tofauti hizo hazikuwa ndogo kwa kuwa zilihusu mambo muhimu yaliyoweza kusaidia kuthibitisha au kukanusha tukio lilivyotokea huku Mahakama ikitilia mkazo pia uwepo wa mgogoro wa ardhi kati ya pande hizo mbili.

Jaji amesema mazingira hayo yaliongeza uwezekano kwamba tuhuma za wizi wa kutumia silaha zingeweza kuhusishwa na mgogoro huo wa muda mrefu.

Mbali na dosari za ushahidi, Mahakama Kuu ilibaini pia makosa ya kisheria yaliyofanyika wakati wa kusikilizwa kwa utetezi katika Mahakama ya Wilaya ambapo warufani na mashahidi wao walitoa ushahidi bila kula kiapo au kuthibitisha kauli zao kama sheria inavyotaka.

Jaji Magoiga amesema sheria inataka kila shahidi katika kesi ya jinai kutoa ushahidi kwa kiapo au uthibitisho, isipokuwa katika mazingira maalumu yanayotambuliwa na sheria na Mahakama hiyo ya chini ilishindwa kuwaeleza warufani kikamilifu haki zao kabla ya kuanza kujitetea, jambo ambalo lilikiuka masharti ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Hata hivyo, licha ya dosari hizo za mwenendo wa kesi, Jaji amesema hakuna sababu ya kuamuru kesi isikilizwe upya kwa kuwa hata ushahidi wa upande wa mashtaka wenyewe haukufikia kiwango cha kuthibitisha kosa bila kuacha shaka.

“Baada ya kupitia ushahidi wote kwa jumla wake, nimefikia hitimisho kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi ya warufani bila shaka yoyote,” amesema.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu iliruhusu rufaa hiyo, ikafuta hatia na hukumu ya kifungo cha miaka 30 iliyotolewa dhidi ya warufani hao na kuamuru waachiliwe huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *