Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amemteua Mansura Mossi Kassim kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Kabla ya uteuzi huo, Mansura alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Katiba,  Sheria Utumishi na Utawala Bora. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Juni 22, 2026 ikiwa imesainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Saleh Juma Mussa, uteuzi huo unaanza rasmi leo na anatarajiwa kuapishwa Jumatano Juni 24, 2026 Ikulu, Zanzibar.

Mansura anachukua nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said ambaye aliteuliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia.

Zena aliteuliwa kushika nafasi ya ukatibu mkuu kiongozi mwaka 2021 baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi kuingia madarakani hadi Machi mwaka huu alipoteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika nafasi ya ubalozi Saudi Arabia.

Katika utumishi wake Mansura alikuwa mfanyakazi wa kawaida katika Wizara ya Killimo na Mifugo ambapo baadaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa wizara katika wizara hiyo wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Saba, Dk Mohamed Shein.

Baada ya Rais Mwinyi kuingia madarakani, alimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara Katiba , Sheria Utumishi na Utawala Bora mpaka mwaka jana alipomteua kuwa katibu mkuu kamili wa Wizara hiyo nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Seif Shaaban ambaye alihamishiwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Umwagiliaji hadi alipostaafu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *