Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imeitaka Serikali na makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuhudhuria bila kukosa mwenendo wa shauri la kupinga uteuzi wa makamishna hao kesho Jumanne, Juni 23, 2026.

Shauri hilo la mapitio ya kimahakama limefunguliwa na mwanaharakati Buberwa Ephraim Buberwa na mwenzake Joseph Daud Mabugo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila na makamisha wake watatu.

Makamishna hao ambao pia ni walalamikiwa katika shauri hilo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.

Buberwa na mwenzake walifungua shauri hilo la kupinga uteuzi wa makamishna hao, Juni 18, 2026 kwa njia ya mtandao, baada ya kupata kibali cha Mahakama hiyo.

Uamuzi wa Mahakama hiyo kuridhia kufunguliwa kwa shauri hilo ulitolewa Juni 8, 2026 na Jaji Agustine Rwizile kufuatia maombi ya kibali hicho cha walalamikaji hao baada ya kuridhika kuwa wamekidhi matakwa ya kisheria kuruhusiwa kufungua shauri hilo.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa na Jaji Wilbert Chuma, kesho Jumanne, Juni 23, 2026, kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa hati za taarifa ya usikilizwaji wa shauri hilo zilizosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo kwenda kwa walalamikaji na walalamikiwa wote ambazo Gazeti la Mwananchi imeziona, limepangwa kutajwa saa 5:30 asubuhi.

“Unatakiwa kuhudhuria kwa njia ya mtandao kupitia kiungo (link): https://virtualcourt.judiciary.go.tz/hc023 kwa tarehe iliyopangwa bila kukosa,” zinasomeka hati hizo za taarifa ya usikilizwaji wa shauri hilo kwenda kwa wadaawa wote.

Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wake ukitangazwa Mei 18, 2026.

Rais Samia ameunda tume kufuatia Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Awali, kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa maeneo mbalimbali nchini na kuwafungua kesi za uhaini lakini baadaye Rais akaelekeza waachiwe.

Baadaye Rais aliunda Tume ya Jaji Chande iliyowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ambayo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti hiyo, imeeleza watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Hata hivyo, kabla tume hiyo ya kijinai haijaapishwa kuanza jukumu hilo, mwanaharakati Buberwa na mwenzake Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, walikwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.

Katika shauri hilo waombaji hao wanaiomba Mahakama hiyo, itengue uamuzi huo wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.

Sababu za kuipinga tume

Buberwa na Mabugo wanapinga uamuzi wa Rais wa uteuzi wa makamishna hao wakidai kuwa, Rais amefanya nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria na ni kinyume cha sheria.

Pia, wanadai uteuzi hauna msingi wa kimantiki, unakwenda kinyume na matarajio halali ya waombaji na ya wananchi kwa jumla, unahusisha matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari na unapingana na masharti ya Katiba.

Katika hati ya maelezo na kiapo chao cha pamoja, waombaji hao wanadai kuwa, awali kufuatia matukio hayo Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa nchini na kuwafungulia kesi za uhaini lakini baadaye Rais akaelekeza waachiwe, kisha akaunda Tume ya Jaji Chande.

Tume hiyo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti ya uchunguzi wa matukio hayo ilipendekeza kuundwa kwa tume nyingine ya kuchunguza ujinai wakati na baada ya uchaguzi; na Rais akaahidi kuunda tume hiyo.

Hata hivyo, Buberwa na Mabugo wanadai kuwa,  kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32(R:E 2023) Rais hana mamlaka ya kuunda tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.

Wanabainisha kuwa, kwa mujibu wa sheria hiyo, Kifungu cha 21(1) (a) na (b), Rais baada ya kupokea na kuisoma ripoti ya Jaji Chande, alipaswa kuelekeza wale waliotajwa katika ripoti hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia, wanadai kuwa Rais hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza matukio ya kijinai bali hilo ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wanafafanua kuwa, DPP ndiye pekee amepewa mamlaka Kikatiba na kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Mashtaka Sura ya 430 (Marejeo ya mwaka 2023) ikiwamo kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai bila kujali sheria nyingine zozote nchini.

Wanadai kuwa, kama Rais baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande anaona kuna haja ya kuchunguza zaidi, anatakiwa kumuagiza DPP kuliagiza Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.

Pia, wanadai kuwa kitendo cha Rais kuunda tume kuchunguza matukio wakati aliamuru watuhumiwa waachiwe bila Mahakama kutoa uamuzi wowote kuhusu uhusika wao, unakosa mantiki wa kisheria na ni kitendo cha kibaguzi kinachopingana na ibara ya 13 (1) ya Katiba ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *