
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imepanga Julai 10, 2026 kusikiliza shauri la kupinga uteuzi wa makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,.
Mahakama hiyo imepanga tarehe hiyo wakati shauri hilo lilipotajwa kwa mara ya kwanza leo Jumanne, Juni 23, 2026, kwa njia ya mtandao huku Serikali ikiomba kupewa muda mfupi kuwasilisha majibu ya maandishi, dhidi madai ya walalamikaji kabla ya tarehe ya usikilizwaji.
Shauri hilo la mapitio ya kimahakama limefunguliwa na mwanaharakati Bubelwa Ephraim Bubelwa na mwenzake Joseph Daudi Mabugo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, na makamisha wake watatu.
Makamishna hao wa tume hiyo ambao pia ni walalamikiwa katika shauri hilo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Wakati shauri hilo ambalo linasikilizwa na Jaji Wilbert Chuma, lilipotajwa leo, kiongozi wa jopo la mawakili wa walalamikiwa wote, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola ameieleza mahakama kuwa walipokea wito wa mahakama kuhudhuria mwenendo wa shauri hilo jana Juni 22, 2026.
Hata hivyo, ameieleza mahakama walikuwa hawajapewa nyaraka halisi za shauri hilo na akaomba wapewe nyaraka halisi za shauri hilo na akiomba siku tano tu za kiwasilisha majibu hayo badala ya siku 14.
“Kwa asili ya shauri hili tunazo siku 14, lakini tunaomba siku tano tu kuwasilisha majibu yetu ya maandishi dhidi ya hati ya maelezo (ya walalamikaji) pamoja na kiapo kinzani,” amesema wakili Kalokola.
Kwa upande wake, mmoja wa mawakili wa walalamikaji, Hekima Mwasipu ameomba baada ya walalamikiwa kuwasilisha majibu ya maandishi na kiapo kinzani dhidi ya madai hayo, nao wapewe siku tano kuwasilisha majibu dhidi ya kiapo kinzani cha walalamikiwa.
Japo Serikali ilipinga ombi hilo, Mahakama imekubalina na hoja za kiongozi wa jopo la mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki kuwa walichokiomba kinaruhusiwa kwenye kanuni.
Hata hivyo, Jaji Chuma ameonya katika majibu ya kiapo hicho kinzani mawakili wa walalamikaji wasiibue mambo mapya ambayo hayakuwepo tangu hatua ya awali ya ombi la kibali cha kufungua shauri hilo.
Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na uteuzi wa mwenyekiti makamishna wake ulitangazwa Mei 18, 2026.
Rais Samia ameunda tume kufuatia mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Kisha Rais aliunda Tume ya Jaji Chande ambayo iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ambayo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti hiyo, watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa, idadi ambayo alisema inaweza kuwa zaidi, ndipo baadaya akaunda tume hii ya Jaji Lila.
Hata hivyo kabla tume hiyo haijaapishwa kuanza jukumu hilo, Buberwa na mwenzake Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, wamekwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.
Katika shauri hilo waombaji hao wanaiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.
Sababu za kuomba kuipinga tume hiyo ni kwamba walalamikaji hao wanadai kwa uteuzi huo Rais amefanya nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria.
Pia wanadai uteuzi hauna msingi wa kimantiki, unakwenda kinyume na matarajio halali ya waombaji na ya wananchi kwa ujumla, unahusisha matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari na unapingana na masharti ya Katiba.