Wairani katika mji mkuu Tehran, majiji, miji na vijiji vyote nchini usiku wa kuamkia leo walikusanyika misikitini na katika vituo vya kidini na barabarani katika marasimu ya kuadhimisha Tasu’a, siku ya tisa ya mwezi Muharram, kuelekea kwenye Siku ya Ashura ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW).

Waombolezaji katika kona zote za Iran wametangaza kushikamana kwao na Ahlul Bait wa Mtume wetu Muhammad (SAW), mafundisho sahihi ya Uislamu na kutetea malengo ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib ya kupinga dhulma na kupambana na uonevu na upotoshaji.

Nara kuu katika maombolezo ya sasa ya Muharram ni kulaani mashambulizi na ukatili wa Marekani na Israel dhidi ya umma na mataifa ya Kiislamu, hususan Iran, Palestina na Lebanon na kula tena kiapo cha utiifu kwa ajili ya kudumisha mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW).

Kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu wa Muharram mamlaka za Iraq zimekuwa zikijitayarisha kwa ajili ya kupokea mamilioni ya mazuwari na Waislamu wanaoendelea kumiminika katika mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya Siku za Tasu’a na Ashura na kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (AS).

Marasimu ya Muharram hushika kasi zaidi tarehe 9 na 10 Mfunguo nne ambapo mamilioni ya Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia huwasili katika mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya maombolezo na kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na watu wengine wa familia ya Mtume. 

Karbala

Kilele cha maombolezo ya Muharram kitakuwa tarehe 10 siku inayojulikana kwa jila la Ashura ambapo Imam Hussein (AS) na watu wengine wa familia ya Mtume Muhammad na wafuasi wao waaminifu waliuawa kikatili baada ya mapambano ya kishujaa yaliyobakia hai katika historia ya wanadamu.

Imam Hussein (AS), akiwa pamoja na watu wengine wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) na masahaba zake waaminifu waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram katika mapambano ya siku ya Ashura dhidi ya utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Tehran inatoa salamu za rambirambi kwa Waislamu wote hususan Shia, wafuausi wa Ahlul Bait na wapenda haki kote duniani kwa mnasaba wa siku hii ya Tasu’a ya Imam Hussein (AS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *