Leo ni tarehe 9 Muharram 1448 Hijria sawa na Juni 24 mwaka 2026.

Leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ni siku ya Tasua’ yaani tarehe tisa Mfunguo Nne Muharram.

Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong’ona na Mola wake.

Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ”Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.” Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao.

Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi, lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.   ****

Siku kama ya leo miaka 214 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar.

Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow.

Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi waliwashambulia askari wa Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao.

Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812. **

Katika siku kama ya leo miaka 183 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.    ****

Na siku kama ya leo miaka 51 iliyopita Mirza Ahmad Ashtiani, mmoja wa wasomi wa sheria za Kiislamu, wanafalsafa na wanasayansi mashuhuri wa kisasa wa Iran, alifariki dunia.

Alizaliwa Tehran yapata mwaka 1300 Hijria Qamaria katika familia ya wasomi ya Mirza Hassan Ashtiani, mujtahid mashuhuri wa enzi ya Qajar. Baada ya kusoma sayansi ya kidini na kiakili kwa wasomi mashuhuri kama vile Mirza Hashem Rashti, Mirza Hassan Kermanshahi, na Sayyid Mohammad Yazdi, alianza kufundisha elimu za Kiislamu katika shule za Sepahsalar na kisha akatumia muda kusoma, kufundisha, na kufanya utafiti katika vyuo vikuu vya Qum na Najaf al Ashraf.

Baada ya kurudi Iran, Ashtiani alitambuliwa kuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu za kiakili na nakili wa zama hizo. Alikuwa hodari katika falsafa, irfani, fiqhi, hisabati na tiba za kijadi, na amelea na kufundisha wanafunzi mashuhuri kama Allamah Hassan Hassanzadeh Amoli, Sayyid Jalaluddin Ashtiani na Sayyid Abbas Tabatabaei.

Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu na risala zaidi ya sitini katika nyanja za falsafa, irfani, teolojia, na maarifa ya Kiislamu.

Mwanachuoni huyu mchamungu  aliyejitolea maisha yake kuelimisha, kuandika vitabu na kuongoza watu kidini, hatimaye alifariki dunia mjini Tehran tarehe 3 Tir mwaka 1354 Hijria Shamsia.

Mwili wake ulizikwa katika Haram ya Hadhrat Abdul Adhim al Hassani katika eneo la Rei lililoko kandokando ya jiji la Tehran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *