Dar es Salaam. Wananchi wenye changamoto ya kupata huduma za matibabu ya kibingwa wanatarajiwa kunufaika na kambi maalumu za matibabu na upasuaji zitakazofanyika Julai mwaka huu, baada ya Stanbic Bank Tanzania kutoa Sh20 milioni kusaidia utekelezaji wa mpango huo.
Mchango huo umetolewa kwa Mpango wa Kambi za Matibabu na Upasuaji wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), ukiwa na lengo la kupanua upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wanaohitaji matibabu maalumu.
Kambi hizo zinatarajiwa kufanyika katika vituo teule vya afya nchini Malawi pamoja na mikoa ya Arusha na Mtwara nchini Tanzania, ambapo wataalamu wa afya watatoa huduma za kibingwa na upasuaji bila malipo kwa wananchi.
Hundi ya ufadhili huo ilikabidhiwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, kwa Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dk Ntuli Angyelile Kapologwe.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rwegasira amesema benki hiyo inaamini kuwa maendeleo ya jamii yanategemea ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.
“Ufadhili huu unaonesha dhamira yetu ya kuendelea kuwekeza katika sekta muhimu kama afya, ambayo ni msingi wa ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Kapologwe alisema ushirikiano huo utasaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaokabiliwa na changamoto ya kupata huduma za kibingwa.
Amesema ECSA-HC inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
“Afya ni msingi wa maendeleo ya jamii na uchumi. Ushirikiano huu unatuwezesha kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma za kibingwa,” amesema.
Stanbic Bank Tanzania imeeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2025 hadi 2026 imechangia zaidi ya Sh230 milioni katika miradi mbalimbali ya afya na maendeleo ya jamii.
Mchango huo umetolewa wakati benki hiyo ikiadhimisha miaka 30 ya huduma zake nchini Tanzania, ambapo imekuwa ikieleza kuendelea kushiriki katika miradi ya kijamii kupitia sekta za afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi.