Jumapili, Juni 21, 2026, siku ya kwanza ya mazungumzo ya utekelezaji wa vipengele 14 vya makubaliano ya kumaliza vita baina ya Iran na Marekani, vipengele viwili muhimu tayari vilikuwa vimeshavunjwa. Iran walitangaza kuufunga tena Mlango Bahari wa Hormuz.

Kipengele namba tano, kati ya 14, kinataka Iran wafungue Mlango Bahari wa Hormuz kwa siku 60, na kuruhusu meli zipite Ghuba ya Uajemi hadi Bahari ya Oman, kwenda na kurudi, kipindi mazungumzo ya kumaliza vita yakiendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema kuwa wamefunga Mlango Bahari wa Hormuz kwa sababu Israel ilifanya mashambulizi Lebanon.

Katika hati ya makubaliano baina ya Marekani na Iran, kipengele cha kwanza kabisa, kwa msisitizo, kimebainisha kuondolewa kwa uvamizi wa kijeshi Lebanon, na kuheshimiwa kwa mamlaka ya kidola ya nchi hiyo.

Nani ameivamia Lebanon? Jibu ni Israel. Februari 28, 2026, Marekani kwa ushirikiano na Israel, walianzisha mashambulizi dhidi ya Iran. Mpango wao ulikuwa kubadili utawala wa Iran. Leo inatimia miezi mitatu na siku 27, tangu walipoanzisha mashambulizi hayo, Marekani na Israel hawazungumzi tena lugha moja.

Kwa nini hawazungumzi lugha moja? Jibu ni kupishana kwa masilahi ya kisiasa. Marekani wanataka vita iishe, kuendelea ni hatari kisiasa kwa Rais Donald Trump. Israel wanataka vita iendelee, kukoma kwa vita ni hatari kisiasa kwa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu.

Israel tayari walishaweka wazi msimamo wao wa kutoafiki makubaliano baina ya Marekani na Iran. Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, alitoa taarifa kwa umma akiyaita “makubaliano ya Marekani na Iran” kuwa “makubaliano ya Trump.”

Alisema: “Makubaliano ya Trump hayatufungi sisi. Israel siyo sehemu ya makubaliano hayo. Israel itaendelea kufanya uamuzi wake wa kulinda raia wake.” Wakati huohuo, Netanyahu alisema kuwa yeye haiongozi Israel kwa maelekezo ya Trump. Kila mmoja anawajibika kwa nchi yake.

Mpaka hapo, kikwazo namba moja ni masilahi ya kila upande. Kwa hali ilipofikia, Trump amekuwa tayari kutojali masilahi ya Israel tena. Anajali ya kwake. Lazima vita iishe kwa ajili ya usalama wake wa kisiasa na dunia. Vita dhidi ya Iran imeleta mtikisiko mkubwa wa kiuchumi duniani. Iran imeipigisha magoti dunia kwa kufunga Mlango Bahari wa Hormuz, hivyo kusababisha nishati za mafuta na gesi kupanda bei, vilevile kuadimika.

Kisha, Iran ikageuza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa chanzo chake kipya cha mapato. Inatoza fedha meli zinazopita Hormuz, tena ikizingatia zile zisizo na masilahi ya moja kwa moja na Marekani pamoja na Israel. Bei ya mafuta kupanda, kumepandisha gharama za maisha ulimwenguni. Marekani pia imeathirika.

Uchaguzi wa nusu muhula Marekani utafanyika Novemba 3, 2026. Ni miezi minne na siku 10 kutoka sasa. Uchaguzi Mkuu Israel unatarajiwa kufanyika Oktoba 27, 2026. Ni miezi minne na siku tatu kutoka sasa. Kwa Israel, uchaguzi unaweza kufanyika mapema zaidi, baada ya Bunge la 25 ya Israel (Twenty Fifth Knesset), kupiga kura kutaka uchaguzi uharakishwe.

Trump anataka awe amemalizana na Iran kabla ya uchaguzi wa nusu muhula. Kumalizana na Iran kijeshi, imeonekana ni vigumu.

Ni sababu sasa ya kukumbatia mazungumzo, ili kumalizana na Iran kidiplomasia. Hofu ya Trump ipo wazi, na ameshaisema, kwamba endapo chama chake, Republican, kitashindwa kwenye uchaguzi wa nusu muhula, wapinzani wao, Democrats, wataanza mchakato wa kumng’oa madarakani. Ni hofu, ni presha!

Netanyahu tayari ameshatangaza nia yake ya kuomba ridhaa ya kuendelea kuwa Waziri Mkuu wa Israel baada ya uchaguzi ujao. Hata hivyo, presha ya kuangushwa ni kubwa.

Kinachoweza kumponya ni mwendelezo wa vita ili uchaguzi usifanyike. Makubaliano ya Marekani na Iran, yanampa wakati mgumu kisiasa. Zaidi, hali ikiwa hivi, chama chake, Likud, kitaanguka vibaya kwenye uchaguzi.

Lebanon ni shida

Iran imeingia kwenye meza ya mazungumzo wakiamini wao ndiyo wenye karata ya uamuzi. Tangu awali, walisema kuwa Marekani na Israel walianzisha vita, ila wao ndiyo wataamua jinsi ya kuimaliza.

Kuthibitisha hilo, waliweka sharti kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano lazima yajumuishe Lebanon. Iran inataka oparesheni zote za kijeshi za Israel nchini Lebanon, zikome.

Katika hati ya makubaliano (MoU), iliyosainiwa na Trump, pamoja na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, Juni 17, 2026, suala la Lebanon ni agenda iliyokubaliwa.

Hata hivyo, Israel kuonesha hawaungi mkono makubaliano hayo, walifanya mashambulizi Lebanon, hivyo Iran nayo ikafunga Mlango Bahari wa Hormuz.

Israel kuiacha Lebanon kirahisi ni ngumu. Mgogoro wa Lebanon na Israel upo kabla ya dola ya Mapinduzi ya Kiislam Iran.

Chanzo chake ni Israel kuanza kupokea mashambulizi ya Wapalestina kutokea Kusini ya Lebanon. Mwaka 1978, Israel iliivamia Lebanon, ilifanya hivyo kwa mara nyingine mwaka 1982, na kuidhibiti Kusini ya Lebanon mpaka mwaka 2000.

Baada ya Israel kuiachia Lebanon, ilianza kupokea mashambulizi kutoka kwa kikundi cha wapiganaji cha Hezbollah. Baada ya mgogoro wa muda wa mrefu, uliokolea zaidi mwaka 2023, ilipofika mwaka 2024, Israel iliivamia tena Lebanon.

Israel wanaamini kuwa kuikalia Lebanon ni muhimu na lazima kwa usalama wao, vinginevyo mashambulizi dhidi yao yataendelea.

Sasa, kitendo cha Trump kusaini hati ya kumaliza vita na Iran, halafu makubaliano hayo kuhusisha Lebanon, bila Israel kushirikishwa, kimekuwa mgongano mkubwa wa kimasilahi.

Israel wanaamini lazima walishikilie eneo la Kusini ya Lebanon, vinginevyo watapokea vipigo mfululizo kutoka kwa vikundi vya mujahidina, hasa Hezbollah.

Kuonesha kuwa Israel hawatanii kuhusu Lebanon, walishafanya mashambulizi mengine hata baada ya hati ya makubaliano kusainiwa baina ya Trump na Pezeshkian.

Huo ni ujumbe wa wazi kwamba Israel haikubaliani na makubaliano ya Marekani na Iran. Na kweli, Netanyahu hapokei maelekezo kutoka kwa Trump.

Iran nayo masilahi yao kwa Lebanon wanayapa kipaumbele. Kwanza, baada ya Israel kuishambulia Lebanon baada ya hati ya makubaliano kusainiwa, waliahirisha kuhudhuria mkutano wa Uswisi, ambao awali ulitakiwa kufanyika Juni 19, 2026. Kisha ukafanyika Juni 21 na 22, 2026.

Hezbollah ni mtoto wa Iran. Kikundi hicho kilianzishwa chini ya ufadhili wa Kiongozi Mkuu (Rahbar), wa kwanza wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini.

Kikundi hicho kimekuwa kikifanya kazi tatu muhimu, kulinda masilahi ya Iran Mashariki ya Kati, kuwatetea Wapalestina, ambayo ndiyo agenda kuu ya kuanzishwa kwake, vilevile kuipigania Lebanon, ambayo ndiyo ardhi yao ya nyumbani.

Kilio cha Hezbollah na serikali ya Lebanon, ni vikosi vya Israel kuondoka Kusini ya Lebanon, na mipaka yake kuheshimiwa kama dola huru.

Iran inaona kuwa kuweka masharti yenye kuwalenga wao moja kwa moja peke yake ni ubinafsi, usaliti, na kutowazingatia washirika wao wa mapambano. Ni kwa msingi huo, Iran inataka Lebanon iachwe.

Zipo sababu nyingine za kidini, kijiografia, kisiasa na kitamaduni, ambazo Iran wanazizingatia kwa umuhimi mkubwa, kiasi kwamba wapo tayari kuendelea na vita ambayo inawapa hasara kubwa, kuliko kuruhusu Lebanon iendelee kukaliwa na Israel.

Kuhusu mazungumzo ya Uswisi, upande wa Iran, ujumbe wa mazungumzo uliongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Ghalibaf, akiambatana na Araghchi, pamoja na maofisa wengine.

Marekani, kiongozi wa mazungumzo ni Makamu wa Rais, JD Vance, aliyeambata na Mjumbe Maalum wa Misheni za Amani, Steve Wotkoff, mshauri wa Trump, Jared Kushner, na maofisa wengine.

Jumatatu, Juni 22, 2026, mazungumzo ya awali ya Uswisi yalimalizika. Taarifa ya Vance kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa viongozi wakuu waliondoka, lakini kazi ya majadiliano iliachwa kwa wataalamu wa pande zote mbili.

Ubabe ni changamoto

Ukiacha suala la mgongano wa masilahi kwa pande zote, pembe ya pili katika pembe tatu za mkwamo wa mwafaka ni ubabe wa Marekani. Trump anaamini kuwa kwa vile Marekani ndiyo imekuwa mlinzi mkuu wa Israel, kwa hiyo Netanyahu na serikali yake wanatakiwa kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi.

Mathalan, Trump aliamua kumpuuza Netanyahu na kuendesha majadiliano na Iran, chini ya upatanishi wa Qatar, Saudi Arabia na Pakistan. Kisha, akatamba kuwa Netanyahu humsikiliza yeye. Matokeo yake suala la Lebanon limekuwa mfupa mgumu kuelekea kufanikisha mwafaka.

Laiti Trump angeacha ubabe na kumshirikisha Netanyahu hatua kwa hatua, pengine hali isingekuwa ya wasiwasi kama ilivyo sasa. Kinyume chake, alijipa uhakika kwamba angemlazimisha Netanyahu kuondoa majeshi yake Lebanon na angetii. Hilo limekuwa gumu.

Vance amekuwa akitembea na kusherehesha kinachotoka kwa bosi wake, Trump. Baada ya kikao cha Uswisi, Vance aliionya Israel kuwa Marekani ndiyo mshirika wao pekee aliyebaki, hivyo hawapaswi kuchezea uhusiano uliopo kwa sasa.

Maswali ni mengi; je, Israel itakubali kunywea kwa Marekani na kusamehe masilahi yao ndani ya Kusini ya Lebanon? Netanyahu atakubali kumtii Trump na chama chake kishindwe kwenye uchaguzi?

Trump na Netanyahu wapo tayari kuvunja uhusiano wa kihistoria baina ya Marekani na Israel kwa sababu ya masharti ya Iran? Trump atakubali kupoteza karata kwenye uchaguzi wa nusu muhula kwa sababu ya Israel? Uhusiano wa Israel na Marekani ukivunjika ni doa kubwa jeusi la kihistoria kwa Trump.

Mwendelezo wa ubabe wa Trump, upo pia dhidi ya Iran. Kila mara inapotokea kutokuelewana, badala ya kujikita kwenye mazungumzo, na kusikilizana, yeye hutoa vitisho vya kuishambulia Iran kijeshi.

Misimamo ya Iran

Haijalishi inapata madhara kiasi gani, lakini Iran imekuwa na msimamo mkali katika kulinda kile ambacho wanakisimamia. Eneo hili linakamilisha pembe ya tatu katika pembe tatu za mkwamo wa mwafaka wa Iran na Marekani.

Trump ni mbabe, Iran wana misimamo isiyoyumba. Nchi hiyo imeshapokea vipigo vingi ndani ya miaka 40. Uvamizi wa Iraq na vita ya miaka nane, vikwazo vya kiuchumi, vinavyofanya nchi hiyo ishindwe kufanya biashara ya rasilimali zake kwa nafasi, pamoja na hivyo, nchi hiyo haijawahi kusalimu amri.

Mashambulizi ya makombora yaliyotua Tehran na kuua viongozi wake wa juu, akiwemo aliyekuwa Kiongozi Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, uharibifu mkubwa wa miundombinu, lakini bado ilisimama na kujibu mapigo, na kamwe haijawahi kukubali kuweka mikono juu wala nyuma. Ni pembe tatu za mkwamo, bila matumizi bora ya busara zitaugharimu mwafaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *