Wakati nyota wa Namungo, Fabrice Ngoy akiwa mchezaji wa tatu kufunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara, mambo manne yamebadilika ghafla.

Ngoy amefunga mabao hayo leo wakati akiiongoza timu yake kuikandamiza mabao 3-2 KMC ambayo imeshashuka daraja tayari.

Nyota huyo anaungana na watangulizi wake waliofanya hivyo ikiwa ni Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars na Methew Tegis wa Pamba Jiji.

Katika mechi nane zilizochezwa viwanja tofauti, mambo manne yamebadilisha upepo wa ligi na kufanya utamu na ugumu kuendelea katika hesabu za lalasalama zikibaki michezo miwili iliyobaki.

Ufungaji bora

Nduwumwe aliyeiongoza Singida Black Stars kuidungua Tanzania Prisons mabao 3-1 amemfikia aliyekuwa kinara wa mabao, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam wakifikisha mabao 14 wote.

Straika huyo amefunga mabao mawili leo dakika ya tatu na 40 huku lingine likifungwa na beki Kennedy Juma dakika ya 23 ilhali la kujifariji kwa Prisons likifungwa na Kelvin Sengati.

Hata hivyo, Ngoy amekoleza pia vita ya tuzo ya ufungaji bora akifikisha mabao 11 sawa na Tegis (Pamba Jiji), Allan Okelo wa Yanga na kufanya mechi mbili zilizobaki kuweza kushangaza zaidi msimu huu.

Top Four rasmi

Matokeo ya ushindi wa Singida BS dhidi ya Tanzania Prisons yameihakikishia nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 50 na kubakiza mechi mbili mkononi.

Pointi hizo zinaifanya timu hiyo kuwa na uhakika wa kucheza kimataifa mwakani kwani wapinzani wao waliopo nafasi ya tano, TRA United kwa pointi 42 hata wakishinda michezo yao miwili iliyobaki hawatafikia pointi za SBS.

Ubingwa bado

Ushindi wa Yanga leo dhidi ya Azam imeendelea kukaa kileleni ikiiacha Simba pointi mbili na kuendelea kusubiri matokeo ya dakika 180 zilizobaki.

Yanga ambayo inatetea taji lake la Ligi Kuu kwa msimu wa tano mfululizo tayari imeshapoteza makombe mawili msimu huu, ikiwa ni Muungano na kombe la shirikisho (CRDB) na sasa macho yao yapo Ligi Kuu.

Timu hiyo kongwe nchini leo ikicheza kwa ubora wake imeichakaza Azam 3-0 na kufikisha pointi 69 ikiwaacha watani zao Simba waliofikisha pointi 67 baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na kufanya vita kubaki vilevile.

Kushuka daraja

Mtifuano huko chini hali inazidi kuwa tete kwani matokeo ya ushindi wa Mbeya City ugenini dhidi ya Pamba Jiji yamebadili msimamo haswa kwa ndugu zao Tanzania Prisons.

City ikicheza CCM Kirumba jijini Mwanza, imeshinda mabao 2-0 dhidi ya wenyeji na kujinasua nafasi za mkiani kwa pointi 28 na kuiacha Prisons nafasi nafasi ya 15 huku Mtibwa Sugar wakishuka nafasi ya 14 kwa pointi zao 27.

Kwa sasa Tanzania Prisons itasubiri mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar kusaka pointi tatu kujinasua nafasi za chini sawa na wapinzani hao, mchezo ukipigwa uwanja wa Sokoine Mbeya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *