Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza rasmi kwa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maandalizi yake yamegeuka kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi kwani mafundi, wapambaji na vibarua wameendelea kuvuna fursa za ajira za muda.
Mwananchi imefika katika viwanja hivyo leo Jumatano, Juni 24, 2026 na kushuhudia mafundi seremala, wachomeleaji, wapaka rangi, wapambaji wa mabanda na mafundi wa mifumo ya umeme wakiendelea na kazi za mwisho ikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kuanza rasmi maonyesho hayo.
Mbali na mafundi, wananchi hususan vijana wanaotafuta ajira za muda waliendelea kufika viwanjani hapo kutafuta nafasi za kazi zinazotokana na maandalizi ya maonesho hayo.
Maonyesho haya yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, yataadhimishwa kwa upekee wa Jubilei ya Dhahabu ikiwa ni miaka 50 tangu kuanzishwa kwake huku yakigeuka kwa jukwaa kuu la biashara nchini
“Kwa kipindi hiki kazi huwa nyingi sana. Kadri wamiliki wa mabanda wanavyotaka maeneo yao yavutie zaidi, ndivyo mahitaji ya mapambo yanavyoongezeka na bei zake kuwa juu,” amesema Martha Malumbano, mpambaji wa mabanda na mkazi wa Sinza.
Amesema gharama za upambaji hutegemea mahitaji ya mteja, ukubwa wa banda na aina ya mwonekano anaoutaka.
Mmoja wa mafundi akiendelea na maandalizi ya ukarabati wa mabanda katika viwanja vya Mwakimu Julius Nyerere ikiwa ni siku tatu kabla ya kuanza kwa maonyesho hayo Juni 28 mwaka huj
“Bei inategemea namna mtu anavyotaka banda lake liwe. Ukitaka kitu cha kawaida gharama huwa ndogo lakini ukitaka banda la kuvutia lenye maua mengi, taa na mapambo ya kisasa gharama zinaongezeka. Hata ua moja mezani haliwezi kuwa sawa na banda lililopambwa kila kona,” amesema.
Martha amesema kwao kipindi cha Sabasaba ni moja ya nyakati muhimu zaidi za kutafuta kipato kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma zao.
“Tunapofika kipindi hiki mara nyingi tunaanza kuwasiliana na wateja wetu wa zamani mapema. Kazi zinakuwa za uhakika na mara nyingi tunashindwa hata kukamilisha mahitaji yote kwa wakati mmoja,” amesema.
Shughuli hizo za maandalizi zinaenda sambamba na ongezeko la idadi ya washiriki wanaotarajiwa kushiriki maonesho ya mwaka huu yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Takwimu za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) zinaonyesha kuwa hadi sasa waonyeshaji 3,752 wamejiandikisha na usajili unaendelea ukilinganishwa na waonyeshaji 3,670 waliokuwapo mwaka jana.
Kwa upande wa ushiriki wa kimataifa, hadi sasa nchi 23 zimethibitisha kushiriki maonesho hayo, huku matarajio yakiwa ni kuona idadi hiyo ikiongezeka katika siku za mwisho za maandalizi.
Hiyo ni kwa sababu baadhi ya nchi ikiwemo Burundi, zimekuwa na utaratibu wa kuwasili baada ya maonesho kuanza rasmi, wakati Kenya nayo ikiwa tayari imeonyesha nia ya kushiriki mwaka huu.
“Tumekuja kutafuta kazi, si jambo jipya lakini nimekuwa nikifanya hivi kwa mwaka wa tatu sasa kwani muda ambao maonyesho haya yanafanyika tunakuwa tumefunga chuo,” amesema Mariana Mushi mkazi wa Keko.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis akizungumzia maandalizi ya sabasaba leo Juni 24, 2026 jijini Dar es Salaam.
Miaka 50 ya Sabasaba
Akizungumza miaka 50 ya maonyesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis amesema si jambo dogo kwani maonyesho hayo yameendelea kuunganisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi kwa miongo mitano mfululizo.
Amesema ili kuweka utofauti na maonyesho yaliyowahi kutangulia kaulimbiu kuu ya maonyesho hayo yatakuwa na kaulimbiu ndogo zinazolenga kuhamasisha biashara za kimataifa na matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika biashara.
“Moja ya kaulimbiu hizo ni ‘Bidhaa za Tanzania Kimataifa Zaidi’, inayolenga kuhimiza upatikanaji wa masoko ya kimataifa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini. Kaulimbiu nyingine ni ‘Biashara ya Kitanzania Kidijitali Zaidi’, inayoendana na juhudi za za kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma na shughuli za biashara,” amesema.
Kwa mujibu wake, maandalizi ya maonyesho hayo yamekamilika na washiriki wataanza kupatiwa maelekezo rasmi kupitia semina maalum itakayofanyika Juni 26.
Latifa amesema semina hiyo ni muhimu kwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuwa itatoa taarifa muhimu kuhusu taratibu za maonesho, huduma zinazopatikana ndani ya viwanja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa maonesho.
Katika kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu, TanTrade imeandaa matukio mbalimbali ya kipekee yatakayoanza Juni 27 kwa matembezi maalum yatakayohusisha viongozi wa Serikali, washiriki wa maonesho, wadau wa biashara na wananchi.
Baadaye usiku wa Juni 27 kutakuwa na onyesho maalum la fataki litakaloashiria kuanza rasmi kwa maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba kabla ya ufunguzi Juni 28 mwaka huu.
Mbali na shughuli hizo, TanTrade imesema imeendelea kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Shirikisho la Sekta Binafsi (TPSF) na taasisi nyingine ili kuhakikisha mikutano na majadiliano ya biashara yanayofanyika wakati wa maonesho yanazalisha matokeo yenye tija kwa washiriki.
“Lengo letu si kufanya sherehe pekee. Tunataka kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani na wa nje, kuwajengea mitandao ya kibiashara na kuwafungulia masoko mapya,” amesema Latifa.
Upekee mwingine wa maonesho ya mwaka huu utakuwa usiku maalum wa Jubilei ya Dhahabu utakaofanyika Julai 6, ambapo kutakuwa na maonesho ya historia ya Sabasaba tangu kuanzishwa kwake.