Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO na nchi wanachama wake, zikiwemo Italia na Romania, ambazo Katibu Mkuu wa NATO amekiri waziwazi nafasi yao katika kutekeleza mashambulizi haramu na ya kihalifu dhidi ya Iran, zinapaswa kuwajibishwa kwa aina yoyote ya ushirikiano katika uhalifu uliofanywa na Marekani na Israeli dhidi ya Iran.

Esmail Baghaei ameashiria kauli ya Katibu Mkuu wa NATO katika mahojiano na Fox News kuhusu nafasi ya NATO katika kuunga mkono mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, pamoja na kuitaja Italia na Romania kama nchi mbili zilizotoa msaada mkubwa katika operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran, na kuandika kwenye mtandao wa X: “Kukiri wazi Katibu Mkuu wa NATO kuhusu ushirikiano na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni katika kutekeleza shambulio la kivamizi dhidi ya Iran ni kukiri ushiriki wa moja kwa moja wa shirika hilo katika kutenda uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi huru mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Uvamizi huo umekuwa ukiukaji mkubwa wa kanuni za lazima za sheria za kimataifa na misingi ya msingi ya hati ya Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, NATO na kila nchi mwanachama wake iliyoshiriki katika kufanya maamuzi haya lazima iwajibike kwa matokeo yote yaliyotokana na vita hivi vya kivamizi.

Bwana Baghaei amesema, Katibu Mkuu wa NATO amezitaja waziwazi Italia na Romania kuwa nchi zilizoshirikiana katika kutekeleza uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran. Nchi hizi mbili, pamoja na nchi nyingine yoyote ya Ulaya iliyosaidia uvamizi huo wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, zinapaswa kutoa maelezo kwa wananchi wao na kwa dunia nzima kuhusu sababu zilizozifanya kuamua kushirikiana na wavamizi dhidi ya Iran, na kwa nini walishiriki katika kutenda uhalifu mkubwa na wa kutisha dhidi ya wananchi wa Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *