Dar es Salaam. Moja ya changamoto zinazowakumba watu maarufu ni jamii inayowazunguka kuwawekea viwango tofauti na ubinadamu. Hivyo ikitokea wakipitia changamoto huonekana kama wanaigiza, jambo ambalo baadhi yao linawanyima haki ya kupata msaada.
Katika mahojiano ya Mwananchi na msanii wa Bongo Fleva, Sharifu Said Juma ‘Jay Melody’, anasema maisha ya wasanii au watu maarufu yanahitaji akili kubwa na hekima ya kuishi na jamii ili kuepuka kuchukuliwa kama wapenda starehe na kushindwa kujiwekeza.
Anasema ingawa bado hajatokewa na changamoto hiyo kutokana na aina ya maisha yake. Lakini anaona kwa wasanii wenzake ambao hukosolewa vibaya na kuonekana wanaendekeza starehe badala ya kujiwekea akiba.
“Binafsi naficha sana maisha yangu binafsi na naishi kawaida sana na jamii, hivyo wananiona ni yule yule ingawa wakati mwingine hawaamini kama naweza nikakosa,” anasema na kuongeza:
“Wakati mwingine maisha ambayo wanatuona nayo siyo yale wanayoyafikiria. Mfano naweza nikanunua raba kali nikapiga picha nikajiposti, baadaye nikapata shida wataanza kusema wanajionyesha maisha makubwa halafu wanataka tuwasaidie sisi.
“Ukikaa mchafu au huvai vizuri pia watasema msanii gani hajielewi na hajui kuvaa. Ukipanda bodaboda au usafiri wa umma watasema naye huyu kuimba kote kumbe hana lolote. Ndiyo maana nasisitiza tunahitaji kuishi kwa hekima.”
Anasema hivi karibuni amepitia changamoto ya kuumwa, lakini aliamua kukaa kimya ili kujiuguza.
“Unaweza ukatunza kiasi cha pesa lakini ukaumwa na kikaisha, hakuna atakayejua kwamba ulikuwa unatunza. Hiyo ni kati ya changamoto kubwa wanayopitia wengi wao.”
Anasema kuna wakati kama binadamu anakuwa anatamani kununua vitu vinavyouzwa mitaani, lakini jicho la jamii linakuwa tofauti, hivyo anachokifanya ni kuagiza mtu kufanikisha hilo.
“Wapo wasanii wengi wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo baada ya kuona wanakataliwa na jamii, hilo limenifunza sana kuishi maisha ya kawaida licha ya wao kuniweka juu,” anasema.
Amewahi kudhulumiwa
Anasema mwaka 2025 alikwenda kufanya shoo London, baada ya kumaliza hakulipwa pesa na msimamizi wa tukio hilo.
“Upo nje hauna mtu wa kukutetea unaona tu bora urudi nchini kwako ili usije ukakumbwa na matatizo mengine.”
Ukiachana na hilo, changamoto nyingine anaieleza: “Kuna hasara ambazo tunaingia ni vile watu hawajui tunapitia nini kuandaa wimbo, kufanya video hadi inatoka. Kuna wakati mwingine tunapata hasara kubwa sana.”
Anaongeza: “Kuna wakati mwingine producer ni mshkaji wako anakwambia wimbo umefutika, utafanyaje? Inabidi uache tu. Mfano wimbo wangu wa Nakupenda baada ya kutengeneza video iliharibika ilibidi irudiwe kushutiwa upya, hapo unakuwa umekula hasara zaidi ya Sh.10 milioni. Changamoto zote hizo hakuna anayejua; ukionekana mitandaoni au kwenye runinga wanaona una raha na hauna shida.”
Aliikimbia kazi hii
Anasema mwaka 2016 kabla ya kuanza kuingia kwenye usanii 2017 aliwahi kufanya biashara ya kuuza nguo kwa mtindo wa mnada. Lakini moyoni mwake alikuwa anahisi anafanya jambo lisilo sahihi, akaamua kuachana na kazi hiyo.
“Nguo zilikuwa za watu, hivyo tulikuwa tunachukuliwa kikundi watu na kupandishwa kwenye gari, kisha tukifika eneo la kufanyia mnada ambalo lilikuwa Gongo la Mboto tunashushwa, yule anayeuza tunajifanya hatukuwa naye na kwenda kuzinunua nguo, hivyo tunawavutia watu wengine kuja kununua nguo hizo,” anasema Jay Melody na kuongeza:
“Kitu ambacho kwa upande wangu hakikuwa sawa. Kuna wakati nguo zilikuwa zinapakwa mafuta ili zionekane bora wakati siyo, au nguo ya Sh1,000 mtu anauziwa Sh6,000 hadi 10,000. Nilikuwa nikirudi nyumbani nikihisi nahukumiwa, nikaachana na ishu hiyo na kujikita kwenye muziki.”
Changamoto nyingine anayokumbana nayo ni wakati wa kwenda kuswali msikitini, baadhi ya watu humchukulia kama anaigiza au kujionyesha, kutokana na kazi yake ya muziki, jambo ambalo wakati mwingine humlazimu avae kofia ili asijulikane.
“Jambo lingine msanii inabidi aingie kwenye mahusiano na msanii mwenzake. Mfano unapanda steji anakuja mtu kucheza na wewe, ukiwa na mtu ambaye haelewi inakuwa ngumu kutoa maelezo kila siku. Ila akiwa msanii anajua ipo siku na yeye yatamkuta. Wakati mwingine ni ngumu kupata upendo halisi,” anasema.
Anataja vitu anavyojizuia kuvifanya ni hasira na kuongea kupitiliza, badala yake anapenda kusikiliza zaidi ili kujua mawazo ya watu mtaani.
“Nimejifunza vitu vingi mtaani, kila mtu ana mawazo yake. Pia nazingatia vitabu vya dini vinasema nini. Ndiyo maana hata stejini nikipanda naepuka kufanya vitu vilivyopitiliza ambavyo vinakuwa siyo sawa kijamii, kwani nakuwa natazamwa na wengi wanaoweza kuiga mfano kutoka kwangu.”
Utunzi wa nyimbo
Anasema anaandika nyimbo kutokana na matukio tofauti ya maisha, kisha hupata wazo la kuandika na amekuwa akipokelewa vizuri na mashabiki wake.
“Kuna wakati naweza nikaona jamii inataka nini, lakini pia naangalia soko linataka nini kutokana na ushindani uliopo.”
Kuhusu ushabiki wa mpira wa miguu anasema: “Kiukweli kwa hapa Bongo mimi ni shabiki maandazi. Simba ikishinda nashabikia, Yanga ikishinda nashabikia, sipendi maumivu. Ndiyo maana kila mchezaji mzuri napenda kumuangalia akicheza.”