
Katika dunia ya leo inayozidi kutegemea teknolojia, upatikanaji wa mtandao bora wa mawasiliano na wa uhakika si anasa, bali ni jambo muhimu linalochochea ukuaji wa uchumi sawa ilivyo kwa miundombinu mingine kama barabara, reli na umeme.
Hiyo ni kwa sababu kadri nchi zinavyowekeza katika mawasiliano ya kasi, ndivyo zinavyoongeza uwezo wa wananchi wake kushiriki katika shughuli za uzalishaji, biashara na ubunifu unaotegemea teknolojia.
Kwa Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea, mtandao wa uhakika umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kufungua fursa mpya za kiuchumi na kufuatia hilo, wafanyabiashara wanaweza kufikia masoko mapya.
Pia vijana wanaweza kuanzisha biashara za kidijitali, taasisi za elimu zinaweza kutoa mafunzo kwa kutumia mifumo ya mtandaoni huku sekta ya afya ikinufaika kupitia huduma za kidijitali zinazowafikia wananchi kwa haraka zaidi.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano una athari za moja kwa moja katika kuongeza tija, kuvutia uwekezaji na kuboresha ushindani wa uchumi.
Na hiyo ndiyo maana mataifa mengi sasa yanaweka kipaumbele katika upanuzi wa mitandao ya fibre optic na huduma za intaneti ya kasi kama sehemu ya mikakati ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na teknolojia.
Hilo limeifanya Tanzania nayo kusimama kidete kuhakikisha inapima huduma za mtandao zinazotolewa kwa wananchi kuanzia kupiga simu, ujumbe mfupi wa maandishi, intaneti katika kila miezi mitatu ili kuhakikisha watanzania wanapata kile wanachostahili.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika ripoti zake za robo mwaka imekuwa ikionyesha namna ubora wa mtandao ulivyo kwa watoa huduma mbalimbali huku ikiweka kiwango cha chini kinachopaswa kufikiwa na watoa huduma wote.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa vipimo vya ubora wa huduma hufanyika kwa kuzingatia vigezo vya ubora wa huduma na mbinu za vipimo zilizoainishwa kwenye Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Ubora wa Huduma), 2025.
Miongoni mwa vipimo hivyo ni upatikanaji wa mtandao, kasi ya intaneti, muda wa kuanzisha simu, ubora wa sauti, muda wa SMS kufika, simu zilizounganishwa, simu zilizokatika nk.
Matokeo ya upimaji wa ubora wa huduma za simu na Intaneti kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025 yanaonesha kuwa Mtandao wa Yas iliongoza kwa asilimia 98.5, ukifuatiwa na Vodacom kwa asilimia 98.0, Airtel ilikuwa na asilimia 92.6, TTCL ilikuwa na asilimia 91.8 na Halotel ilikuwa na asilimia 90.6.
Ofisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Mallya anasema kadri sekta ya mawasiliano inavyoendelea kukua, ushindani haupo tena kwenye bei pekee bali umehamia zaidi kwenye ubora wa huduma kwa mteja.
“Wateja wa leo wanahitaji zaidi ya upatikanaji wa mtandao tu. Wanahitaji mtandao wenye kasi na uhakika wa upatikanaji wake bila kusahau huduma bora na suluhisho zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku kwenye ambayo yanaendelea kubadilika kwenye ulimwengu huu wa kidijitali,” alisema Mallya.
Anasema kwao ubora wa huduma ni sehemu muhimu ya viashiria vya utendaji (KPIs) katika ngazi mbalimbali za kampuni. Tunapima na kufuatilia viwango vya ubora wa mtandao, kuridhika kwa wateja, muda wa utatuzi wa changamoto, pamoja na upatikanaji wa huduma.
Anasema kwa kufanya hivyo inawasaidia kama kampuni kuhakikisha kila idara inachangia katika kutoa uzoefu bora zaidi kwa wateja wetu na kuendeleza ushindani wa kampuni katika soko.
Kuhusu uongozi wao kwa ubora Mallya anasema Yas inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya mtandao ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora za sauti, data na huduma za kidijitali.
“Yas inajivunia kuwa na mtandao ulioenea nchi nzima kwa asilimia 96. Yas imewekeza zaidi ya trilioni 1 ikiwa na zaidi ya minara 4,800 ambapo kitakwimu ni minara 1,000 zaidi ya mtandao unaofuata,” anasema.
Anasema kampuni hiyo inayotawala soko la huduma za simu kwa asilimia 28.5 inatumia teknolojia za kisasa katika usimamizi wa mtandao, kuongeza uwezo wa vituo vya mawasiliano (sites), pamoja na kufanya maboresho ya mara kwa mara kulingana na mahitaji ya wateja yanavyoongezeka.
Kadhalika Mallya anasema wanafuatilia kwa karibu changamoto mbalimbali za wateja kupitia mifumo yetu na kuchukua hatua za haraka pale changamoto zinapobainika. Lengo letu ni kuhakikisha wateja wanapata mawasiliano yenye kasi, uhakika na yanayopatikana muda wote.
Wasemavyo wachumi
Akizungumzia suala hili, mtaalamu wa uchumi Oscar Mkude alisema mtandao ni sekta inayowezesha nyingine kwani kwenye shughuli za kiuchumi mawasiliano ni jambo la muhimu kuanzia kuwasiliana na wazalishaji hadi bidhaa inapofika sokoni.
“Mitandao ya simu katika upana wake ikiwamo katika jamii, kungekuwa hakuna mawasiliano ya haraka maana yake mambo yangekuwa yanachukua muda mrefu, watu wangekuwa wanalazimika kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufanikisha biashara na kungekuwa na uchelewaji wa huduma kulingana na hali ilivyo,” alisema.
Anasema kupitia mawasiliano bora kumekuwa na huduma mbalimbali ikiwamo malipo ya kidijitali ambayo ni uti wa mgongo ambapo imefanya baadhi ya miradi imekuwa ikifanyika kwa wakati kwa watu kuwa na uhakika wa kupata fedha zao kwa wakati kuanzia msambazaji hadi mtu wa mwisho.
“Vyote hivi vinawezesha shughuli za uchumi mbalimbali kufanyika kwa urahisi, kwa sasa mtandao unaposinyaa na shughuli za uchumi zinasinyaa,” alisema.
Anasema ili kufanikisha hilo ni vyema kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa za gharama nafuu ambazo watu wote wanaweza kumudu katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
“Ikiwa nafuu lakini pia mtandao huu ufike maeneo tofauti ya nchi, kuna baadhi ya maeneo nchini bado mtandao ni changamoto ambapo mtu analazimika kutumia muda mwingi kutafuta mtandao ili aweze kufanya mawasiliano anayohitaji au kuagiza bidhaa,” alisema.
Profesa Aurelia Kamuzora anasema mahali ambapo hakuna mtandao hawataweza kuendelea kwa sababu hawatakuwa na taarifa za uhakika ili wakauze mali zao katika masoko.
“Kama ni mkulima atakuwa na uhakika wa soko kwa sababu kila kitu anaweza kuona kupitia intaneti, ikikosekana mtu anaweza kudhani bidhaa zake hazina soko na zitamharibikia kumbe akiweza kwenda hatua chache mbele kuna soko zuri la bidhaa anazozalisha,” alisema.
Anasema ni vyema serikali kuhakikisha kila sehemu ambayo bado haijafikiwa na mtandao ili kuhakikisha watu wote wanaunganishwa ili waweze kufikia fursa mbalimbali kwa usawa bila kuwapo na kizuizi.
“Kuwapo kwa mtandao kijijini unafanya wao kuwa na uwezo wa kuiga vitu vinavyoweza kufanya soko la bidhaa au huduma iliyopo jijini Dar es Salaam kuchangamka kwani watataka kwenda na wakati, wasionekane kuwa nyuma,” alisema.
Hali ilivyo vijijini
Upelekaji wa mtandao wa uhakika haukuishia mijini pekee bali hadi maeneo ya vijijini Serikali ilijenga minara ili kuhakikisha wanakuwa na huduma za uhakika.
Aprili 10 mwaka huu, Serikali ilizindua minara 758 ya mawasiliano iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto za mtandao kwa zaidi ya wananchi milioni 8.5, hususan wanaoishi vijijini na katika maeneo ya mipakani.
Uzinduzi huo ulienda sambamba na kuunganisha huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika wilaya 85, jambo linaloashiria hatua mpya katika juhudi za Serikali za kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan alisema uwekezaji huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano kwa lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na kwa gharama nafuu.
Anasema kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutachochea ushiriki mpana wa wananchi katika uchumi wa kidijitali, sambamba na kufungua fursa mpya za ajira, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa.
“Mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani. Leo hii ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” alisema Rais Samia.
Mtaalamu wa Uchumi, Dk Lutengano Mwinuka anasema kwa kadri dunia inavyokwenda kasi katika mageuzi ya teknolojia ni vyema kuhakikisha maeneo ya vijijini yanafikiwa kikamilifu. “Hata ikishindikana kabisa mitandao yote kufika kwenye maeneo ya baadhi ya vijiji basi uwepo hata mtandao mmoja ili wasikose huduma kabisa kwani katika utekelezaji wa Dira 2050 unaoanza Julai Mosi mwaka huu unataja uchumi ujumuishi kama moja ya eneo la kufanyiwa kazi hivyo ni vyema kuhakikisha watu wote wanafikiwa kikamilifu,” alisema.
Anasema anatambua kuwa wakati mwingine suala la kupeleka mtandao hutegemeana na soko kwa sababu ni biashara lakini ni vyema kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.