Paris, Ufaransa. Chuo cha Dhow Countries Music Academy (DCMA) cha Zanzibar kimeandika historia baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya 21 ya UNESCO-Sharjah Prize for Arab Culture. Katika hafla iliyofanyika jana, Juni 24,2026 kwenye Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa.

DCMA kimetunukiwa tuzo hiyo kwa kutambuliwa mchango wake katika kuhifadhi, kufundisha na kuendeleza urithi wa muziki wa taarab pamoja na tamaduni za ukanda wa Bahari ya Hindi na Kiarabu.

Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya chuo na mwakilishi wake, Haldah Am Al-Kanaan. DCMA ni taasisi inayojihusisha na ufundishaji wa ala za asili na mitindo ya muziki wa jadi ikiwemo taarab, kidumbak na ngoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Profesa Khaled El-Enany, alikipongeza chuo hicho kwa juhudi zake za kuhifadhi na kuendeleza urithi wa muziki wa Kiarabu na Kiswahili. Alisema chuo hicho kimetambuliwa kutokana na uwezo wake wa kutumia muziki kama nyenzo ya kuunganisha tamaduni mbalimbali duniani.

Kwa upande wa uongozi wa DCMA ulisema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa Zanzibar na Tanzania, na kwamba itatoa hamasa ya kuendelea kulinda na kuendeleza urithi wa taarab na muziki wa jadi kwa vizazi vijavyo.

Tuzo ya UNESCO-Sharjah Prize for Arab Culture ilianzishwa mwaka 1998 kwa ushirikiano kati ya UNESCO na Serikali ya Sharjah, Umoja wa Falme za Kiarabu. Na hutolewa kila mwaka kwa watu binafsi au taasisi zinazotoa mchango wa kipekee katika kuendeleza na kutangaza utamaduni wa Kiarabu duniani.

Katika toleo la mwaka huu, DCMA ilitangazwa mshindi pamoja na mwanamuziki na mjasiriamali wa utamaduni kutoka Morocco, Brahim El Mazned.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *