MABAO matatu (Hat-Trick), aliyofunga mshambuliaji wa Namungo FC, Mkongomani Fabrice Ngoy katika ushindi wa timu hiyo wa 3-2, dhidi ya KMC FC, umempa mzuka baada ya kupitia kipindi kigumu cha kutokufunga.

Mshambuliaji huyo alifunga mabao hayo na kufikisha 11 ya Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kuandamwa na ukame tangu alipoifungia Namungo katika sare ya bao 1-1, dhidi ya Singida Black Stars, Februari 26, 2026.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoy alisema ni fahari kwake kuongezea idadi hiyo ya mabao katika Ligi Kuu Bara, licha ya kukiri kupitia kipindi kigumu katika mechi zilizopita, jambo alilolichukua kama fursa ya kuzidi kuendelea kupambana.

“Furaha ya mshambuliaji ni kuona unafunga hata kama sio kila mechi kwa sababu hakuna anayeweza kufanya hivyo, kukaa kwa muda mrefu ni jambo lililoniumiza zaidi ingawa, kwangu niliamini muda sahihi ukifika nitaendelea kufunga,” alisema Ngoy.

Hat-Trick hiyo ni ya kwanza kwa nyota huyo tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara, ingawa kwa msimu huu ni ya tatu, baada ya Mrundi Mossi Nduwumwe anayecheza Singida Black Stars na Mkenya Mathew Momanyi wa Pamba Jiji kufunga pia.

Nyota huyo ameaminiwa na Kocha, Juma Mgunda licha ya uwepo wa washambuliaji wengine wakiongozwa na mkongomani mwenzake, Heritier Makambo aliyetoka TRA United zamani Tabora United na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, aliyetokea kikosi cha TMA FC.

Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.

Mshambuliaji huyo alitua hapa nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia na msimu wa 2023-2024, alifunga bao moja tu la Ligi Kuu Bara, huku 2024-2025, akifunga mawili na msimu wa 2025-2026, amefunga 11.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *