DODOMA: MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka walipakodi na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika matembezi na Mbio za Shukrani kwa Mlipakodi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tuzo kwa Mlipakodi Bora na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa TRA, tukio hilo linatarajiwa kufanyika Juni 27,mwaka huu na limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa walipakodi katika kuchochea maendeleo ya taifa kupitia ulipaji wa kodi, huku likitumika pia kuhamasisha wananchi kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kikodi kwa hiari.

Matembezi na mbio hizo zinatarajiwa kuanza saa 12:00 asubuhi na kuwakutanisha walipakodi, wadau wa kodi, taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi katika kuadhimisha mchango wa kodi kwa maendeleo ya Tanzania.
TRA imeeleza kuwa maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Miaka 30 ya TRA, Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea kwa Taifa Letu.”
TRA imebainisha kuwa ushiriki wa wananchi katika tukio hilo utakuwa sehemu ya kuendeleza utamaduni wa ulipaji kodi na kuonesha mshikamano katika safari ya kujenga taifa lenye maendeleo na uchumi imara unaotegemea rasilimali zake za ndani.