Wanariadha kukutana Kibaha mashindano ya taifaWanariadha kukutana Kibaha mashindano ya taifa

ARUSHA: JUMLA ya wanariadha 650 kutoka Tanzania Bara na Visiwani wanatarajiwa kukutana kwa siku mbili, Julai 3 na 4 mwaka huu, katika Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani, kushiriki Mashindano ya Taifa ya Riadha.

Mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka, mwaka huu yatafanyika katika viwanja vya Shule ya Filbert Bayi, Kibaha, yakilenga kuibua na kukuza vipaji vya mchezo wa riadha ili kuwaandaa vijana hao kushindana katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na gazeti hili, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogart Stephen, alisema wanariadha wote kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa sita ya Visiwani wamethibitisha kushiriki mashindano hayo.

Stephen alisema shirikisho hilo limejipanga kuhakikisha linaibua vipaji vipya kwa vijana ili waweze kuchukua nafasi za wanariadha wakongwe wanaotamba kwa sasa, akiwemo Alphonce Simbu na wengine.

Alisema maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika kwa kiasi kikubwa, na kilichobaki ni kwa wanariadha pamoja na makocha kufika Kibaha kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo ya taifa.

Rais huyo wa RT aliongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wake, mchezo wa riadha utaendelea kufanya vizuri kitaifa na kimataifa, kutokana na shirikisho hilo kuongozwa na viongozi wenye uelewa wa mchezo huo na wanaolenga kukuza vipaji vya vijana.

“Tunaungana na Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni, Paul Makonda, ambaye amekuwa akisisitiza uibuaji wa vipaji kwa watoto katika mchezo wa riadha, na sisi tumejipanga kuhakikisha lengo hilo linafikiwa kwa asilimia mia moja,” alisema Stephen.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Riadha Mkoa wa Arusha, Gerard Babu, alisema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuhakikisha unafanya vizuri katika mashindano hayo ya kitaifa ili kuendeleza sifa ya Mkoa wa Arusha.

Babu alisema Arusha ina vipaji vingi vinavyostahili kuonyeshwa katika mashindano hayo na vinatarajiwa kuwa tishio katika siku zijazo, huku wakijipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *