Musoma. Serikali kuu imetoa zaidi ya Sh422.3 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 315 ya maendeleo mkoani Mara katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Fedha hizo zinalenga kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za kijamii na kiuchumi katika wilaya sita za mkoa huo, ikiwemo afya, elimu, maji, miundombinu na nishati.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara jana Alhamisi Juni 25, 2026, Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi, amesema miradi hiyo inalenga kuboresha huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya mkoa.

Amesema hadi kufikia Mei 2026 utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 87.5, huku baadhi ikiwa imekamilika na kuanza kutoa huduma.

Kwa mujibu wa Kanali Mtambi, kati ya fedha zilizotengwa, mkoa huo tayari umepokea zaidi ya Sh241.7 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Tunaendelea kupokea fedha, lakini habari njema ni kwamba kati ya miradi 315, miradi 120 imekamilika kwa asilimia 100 na mingine zaidi ya 50 imefikia asilimia 90 ya utekelezaji,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kikao cha Halamshauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara. Picha na Beldina Nyakeke

Ameeleza kuwa katika sekta ya afya, miradi 48 yenye thamani ya zaidi ya Sh8.8 bilioni inatekelezwa, ikihusisha ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba za watumishi na ununuzi wa vifaa tiba.

Katika sekta ya elimu, amesema miradi 120 yenye thamani ya zaidi ya Sh26.8 bilioni inatekelezwa, ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na miundombinu mingine.

“Katika sekta ya barabara tunatekeleza miradi 53 yenye thamani ya zaidi ya Sh224.8 bilioni. Hii inahusisha barabara za kimkakati ambazo zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mkoa na wananchi wake,” amesema.

Aidha, amesema sekta ya maji ina miradi 13 yenye thamani ya zaidi ya Sh42 bilioni, huku sekta ya nishati ikiwa na miradi 10 yenye thamani ya Sh115 bilioni inayolenga kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ikiwemo vitongoji.

Kanali Mtambi amesema miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za kijamii na kuinua uchumi wa wananchi, akitolea mfano mradi wa uwanja wa ndege ambao umefikia hatua ya kuruhusu ndege kuanza kutua na kuruka.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa CCM mkoani humo wameeleza changamoto zinazoendelea kuwepo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Christopher Siagi, amepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi, lakini amesema upatikanaji wa maji bado ni changamoto katika wilaya hiyo.

Amesema hali hiyo inahitaji kuangaliwa kwa umakini kutokana na uwepo wa chuo kikuu katika eneo hilo ambacho kinatarajiwa kupokea idadi kubwa ya wanafunzi ifikapo Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Ngicho, ameomba Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara wilayani humo akisema hali ya baadhi ya barabara si nzuri na imekuwa ikichangia ajali.

Naye Robert Zembela amesema maandalizi ya miundombinu ya elimu yanapaswa kuzingatia ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028 kutokana na mabadiliko ya sera ya elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *