WAKATI Tanzania ikiendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yenye lengo la kujenga uchumi wa kisasa, wa ushindani na unaojali mazingira, wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa ongezeko la hewa ukaa na gesi nyingine chafu linaweza kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa vya maendeleo ya taifa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Ingawa Tanzania si miongoni mwa nchi zinazozalisha kiwango kikubwa cha hewa ukaa duniani, imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa yanayoathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na ongezeko la gesi hizo. Tayari, athari hizo zinaonekana kupitia vipindi virefu vya ukame, mafuriko ya mara kwa mara, kuongezeka kwa joto, kupungua kwa vyanzo vya maji na kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Hewa ukaa inayojulikana kitaalamu kama Carbon Dioxide (CO₂), ni gesi inayopatikana kwa kiwango kidogo katika angahewa na ni muhimu kwa maisha ya viumbe hai.Hata hivyo, inapoongezeka kupita kiasi, hujikusanya katika angahewa na kufanya kazi kama blanketi kubwa linalozuia joto la dunia kutoka kwa urahisi. Matokeo yake ni kuongezeka kwa joto duniani na kuvurugika kwa mifumo ya hali ya hewa.
Wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa chanzo kikubwa cha hewa ukaa nchini ni matumizi makubwa ya kuni na mkaa kwa shughuli za kupikia.Zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania inategemea nishati hiyo. Hali hiyo imeongeza kasi ya ukataji wa miti na kupunguza uwezo wa misitu kufyonza hewa ukaa. SOMA: Mabadiliko ya Kijani Yaanza Tanzania

Katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara, misitu mingi imeendelea kuvunwa kwa ajili ya kuzalisha mkaa unaosafirishwa kwenda Dar es Salaam na miji mingine mikubwa. Kila mti unaokatwa bila kupandwa mwingine hupunguza uwezo wa mazingira kufyonza hewa ukaa na kuongeza kiwango cha gesi hiyo angani.
Chanzo kingine kikubwa ni sekta ya usafiri. Ongezeko la magari, mabasi, malori na pikipiki zinazotumia petroli na dizeli limeendelea kuongeza utoaji wa hewa ukaa nchini. Katika mkoa wa Dar es Salaam, msongamano wa magari katika maeneo ya Ubungo, Kimara, Magomeni, Kariakoo na Posta huongeza muda wa magari kukaa yakiwaka, hali inayoongeza utoaji wa hewa chafu.
Shughuli za viwandani nazo zimeendelea kuwa chanzo muhimu cha hewa ukaa. Viwanda vya saruji, usindikaji wa vyuma, kemikali na bidhaa nyingine hutumia kiasi kikubwa cha nishati inayotokana na mafuta au makaa ya mawe. Kadhalika, taka zinazooza katika madampo huzalisha gesi chafu, hususan methane, ambayo ina uwezo mkubwa wa kuongeza joto duniani. Uchomaji wa misitu, moto wa porini na uchomaji wa mabaki ya mazao mashambani pia huongeza uzalishaji wa hewa ukaa.
Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC) unaonesha kuwa sekta za nishati, usafiri, matumizi ya ardhi, misitu na usimamizi wa taka ndizo zinazoongoza kwa kuchangia uzalishaji wa gesi chafu nchini. Serikali imeonya kuwa bila hatua za haraka, uzalishaji wa hewa ukaa utaendelea kuongezeka sambamba na ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa idadi ya watu, kupanuka kwa miji na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati.
Kutokana na ukubwa wa changamoto hiyo, serikali imeongeza uwekezaji katika sekta zinazohusiana moja kwa moja na udhibiti wa hewa ukaa na mabadiliko ya tabianchi. Katika mwaka wa fedha 2026/2027, serikali imepitisha bajeti ya takribani Sh trilioni 62.3 ikiwa ni bajeti ya kwanza ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Miongoni mwa maeneo yaliyopata kipaumbele ni uhifadhi wa mazingira, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuharakisha matumizi ya nishati safi. Aidha, zaidi ya Sh trilioni 2.5 zimetengwa kwa Wizara ya Nishati kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji na usambazaji wa umeme, kupanua miundombinu ya gesi asilia na kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
Serikali inaamini kuwa upatikanaji wa nishati safi utapunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao bado unatumiwa na zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania. Dar es Salaam ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na msongamano wa magari, shughuli za viwanda na ongezeko la taka. Katika miaka ya hivi karibuni, mkoa umeshuhudia mafuriko ya mara kwa mara katika maeneo ya Jangwani, Kigogo na Bonde la Mto Msimbazi.

Mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na Simiyu imeendelea kukumbwa na vipindi virefu vya ukame na kupungua kwa mvua, hali iliyoathiri kilimo na ufugaji. Katika mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara, kupanda kwa kina cha bahari na mmomonyoko wa fukwe ni changamoto kubwa. Kilimanjaro na Arusha pia imeendelea kushuhudia mabadiliko ya mifumo ya mvua na kupungua kwa baadhi ya vyanzo vya maji.
Tukiangalia jinsi nchi jirani za Afrika Mashariki zinavyokabiliana na tatizo hili la hewa ukaa, Kenya imeendelea kukumbwa na ukame mkubwa uliosababisha mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa chakula. Serikali ya nchi hiyo imewekeza katika nishati ya upepo na jotoardhi ili kupunguza utegemezi wa mafuta yanayochangia hewa ukaa.
Uganda imeshuhudia mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, huku ukataji wa misitu ukiongeza athari za mabadiliko ya tabianchi. Rwanda imekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika sera za uchumi wa kijani, ikijikita katika usafi wa mazingira na kupunguza matumizi ya plastiki. Hata hivyo, nchi hiyo bado inakabiliwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inamiliki Msitu wa Bonde la Congo unaotajwa kuwa miongoni mwa mapafu makubwa ya dunia kutokana na uwezo wake wa kufyonza hewa ukaa. Hata hivyo, ukataji wa miti na shughuli za kibinadamu zinaendelea kutishia uhai wa misitu hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni anasema:“Mabadiliko ya tabianchi si changamoto ya kesho, ni changamoto ya leo inayohitaji hatua za haraka na ushirikiano wa kila mdau”. Kwa upande wake, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), linasisitiza kuwa mazingira yetu ni uhai hivyo kuyahifadhi ni kulinda afya, uchumi na ustawi wa taifa.
Wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa bila hatua za haraka, gharama za mafuriko, ukame, kupungua kwa uzalishaji wa mazao na uharibifu wa miundombinu zinaweza kuligharimu taifa mabilioni ya shilingi kila mwaka. Kwa mujibu wa wataalamu hao, mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayatategemea ukuaji wa uchumi pekee bali pia uwezo wa taifa wa kulinda mazingira yake.
Vita dhidi ya hewa ukaa si jukumu la serikali pekee bali ni wajibu wa kila Mtanzania anayehitaji kuona taifa lenye hewa safi, maji salama, kilimo chenye tija na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.