
ILIPOISHIA
Maneno ya Wakwetu yalimfariji James akashusha pumzi.
“Sasa itabaki kesi ya kugonga mtu” alisema.
“Kesi za trafiki ni za faini. Nitalipa kiasi chochote kitakachotakiwa. Usiwe na wasiwasi. Ila mtu aliyegongwa hajulikani yuko wapi”
“Kwanini?”
“Polisi walishughulika zaidi na kesi hii ya kujeruhi kwa risasi, wakaipuuza ile. Leo ndiyo wameikumbuka lakini hawana hakika mtu aliyegongwa bado yuko hospitali au amesharuhusiwa”
“Vyovyote itakavyokuwa, sina wasiwasi na kesi za trafiki”
SASA ENDELEA…
“Sawa. Kesho wakikupeleka mahakamani utakiri kosa na utatozwa faini hapo hapo.”
“Na Majaliwa naye yuko wapi?”
“Amekimbia nyumbani tangu ile juzi. Sijui yuko wapi.”
“Amekimbia nini sasa?”
“Amekimbia kesi. Si unajua yeye hana leseni ya kuendesha gari.”
“Ukimpigia simu anasema yuko wapi?”
“Simu yake haipatikani.”
“Angerudi nyumbani tu kuliko kuishi juu juu.”
“Labda akipata habari kuwa kesi imekwisha, ndiyo atarudi.”
“Kumbe Masumbuko ni muoga sana!”
James alicheka.
Walipofika nyumbani, Wakwetu alimweleza mke wake yaliyotokea.
“Walipogundua kuwa James siye aliyehusika walikubali kumpa dhamana. Kesho tunatakiwa turudi tena.”
“Kwa hiyo hata kama Majaliwa atarudi hatakuwa na hatia tena?” Sharifa alimuuliza.
“Aliyetuhumiwa ni James. Majaliwa akirudi hatakuwa na hatia kwa upande wa polisi, lakini kwa upande wangu atakuwa na hatia.”
“Hatia ya nini?”
“Kwani kitendo alichonifanyia umekiona ni kizuri?”
“Ni mwanao yule, utamfanyaje sasa?”
“Hapo atakapokuja ndiyo nitajua la kumfanya. Na nataka aje na arudishe ile bastola.”
“Mimi nafikiri umsamehe kwa sababu ni mwanao.”
“Ameiba bastola yangu, gari langu na kwenda kumpiga mtu risasi. Kama angemuua unafikiri nini kingetokea?”
“Ni kweli amefanya kitendo cha hatari, lakini wewe kama mzazi muweke chini umweleze asirudie tena kosa kama hilo.”
“Kubwa ambalo mimi nataka anieleze ni kwanini alimpiga risasi yule kijana.”
Siku iliyofuata Wakwetu na James walikwenda kituo cha polisi cha Msimbazi. Walikutana na Inspekta Amour aliyewaambia kwamba majeruhi aliyekuwa amelazwa hospitalini baada ya kugongwa na gari aliruhusiwa kutoka hospitalini tangu jana na aliondoka bila kwenda kuripoti polisi.
“Tunamsubiri yeye. Kama atafika hapa leo au kesho ndiyo tutaweza kulifikisha suala hilo mahakamani. Kwa hiyo mnaweza kwenda, mje tena kesho,” Inspekta huyo aliwaambia.
“Sawa. Tutakuja kesho,” Wakwetu alimwambia na kuondoka na James.
Walipotoka kituo cha polisi walikwenda Hospitali ya Bombo kumjulia hali kijana aliyedaiwa kupigwa risasi na Majaliwa. Walimkuta amehamishwa katika wodi ya kawaida baada ya kuondolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
“Ana nafuu sana,” muuguzi waliyemkuta akimpa tembe za kumeza aliwaambia.
Wakwetu na James walimwona. Kijana huyo alionyesha wazi kuwa alikuwa amepata nafuu.
“Unajisikiaje mwanangu?” Wakwetu alimuuliza.
“Najisikia vizuri kidogo,” kijana huyo alimwambia kwa sauti ya chini.
“Nimefurahi kusikia sauti yako na ukiniambia wewe mwenyewe kuwa unajisikia vizuri. Tangu jana nilikuwa nakuja kukutazama. Leo nimeona una nafuu kidogo.”
Kijana akabaki kumtazama Wakwetu bila kusema lolote jingine.
“Ugua pole, nitakutembelea tena kesho.”
Wakati Wakwetu anamuaga kijana huyo, Inspekta Amour aliyekuwa amefuatana na daktari walitokea.
“Imekuwa vyema nimewakuta hapa,” Inspekta Amour akamwambia Wakwetu.
“Nimekuja kumjulia hali majeruhi kwa sababu niliahidi kumsaidia. Si unakumbuka?”
“Nilidhani kwa vile kijana wako hakutambuliwa, utabatilisha ahadi yako.”
“Hapana, siwezi kufanya hivyo. Mimi ni mtu mzima bwana.”
“Umezungumza maneno ya kiungwana. Je, mmemkuta hali yake?”
“Kwa sasa hajambo kidogo.”
Inspekta Amour akamtazama kijana huyo.
“Kijana, unajisikiaje?”
“Nashukuru, najisikia vizuri kidogo.”
Amour akamtazama daktari.
“Dokta, naweza kuzungumza naye mawili matatu?”
“Bado anahitaji utulivu. Hatujaruhusu azungumze na watu. Unaweza tu kumsalimia,” daktari alimjibu.
“Nilitaka kumuuliza swali moja tu kwa leo.”
“Kama ni swali moja unaweza kumuuliza.”
“Si swali gumu, ni swali rahisi ambalo anaweza kulijibu bila wasiwasi,” Inspekta alisema na kumwita James.
“Hebu njoo hapa mbele, kijana mwenzako akuone.”
James akasogea mbele ya Masumbuko.
“Unamfahamu huyu kijana mwenzako?” Inspekta akamuuliza Masumbuko.
Masumbuko alimtazama James kisha akatikisa kichwa.
“Simfahamu,” alisema.
“Unamfahamu kijana aliyekujeruhi kwa risasi kama ukimwona?”
“Nikimwona nitamfahamu.”
Inspekta akamtazama daktari.
“Samahani dokta, nitamuuliza swali jingine ambalo ni muhimu pia.”
“Muulize swali la mwisho.”
“Sawa,” Inspekta akamtazama Masumbuko. “Unaweza kuniambia ulikuwa unafahamiana na yule kijana aliyekupiga risasi?”
“Sifahamiani naye.”
“Je, mlikuwa na ugomvi wowote?”
“Hatukuwa na ugomvi.”
“Alikupiga risasi bure tu?”
“Alipoingia mle chumbani aliniuliza, ‘Wewe ndiye Masumbuko?’ Nilipomjibu ni mimi, alitoa bastola na kunifyatulia risasi.”
“Alikufyatulia risasi tu na kuondoka?”
Masumbuko alionekana kuishiwa nguvu na kushindwa kujibu maswali. Akakunja uso na kufumba macho.
“Basi endelea kupumzika. Nitakuja kukuhoji utakapopata nafuu vizuri.”
Masumbuko akamkubalia kwa kichwa.
Inspekta alimuaga. Wakwetu na James pia walimuaga na kutoka kwa pamoja.
Wakwetu alikuwa amepata fikra nyingi kutokana na maswali ambayo Inspekta Amour alimuuliza Masumbuko.
Wakati wanatoka nje ya hospitali alikuwa akijiuliza, kijana yule ni nani, anatoka wapi na Majaliwa alimjuaje?
“Kama Majaliwa angekuwepo, kila kitu kingeeleweka. Angenieleza ni kwanini amempiga risasi yule kijana,” Wakwetu alijiambia.
Akaendelea kujiambia, ni lazima kutakuwa na sababu, tena sababu kubwa. Majaliwa asingeiba bastola yake na kwenda kumpiga risasi mtu asiyemfahamu.
Wakwetu alipofika nyumbani kwake alimweleza Sharifa maelezo waliyopewa kituo cha polisi na jinsi walivyokwenda Hospitali ya Bombo kumjulia hali kijana aliyepigwa risasi na Majaliwa.
“Yule kijana anasema hamfahamu Majaliwa, lakini ninaamini Majaliwa atakuwa anamfahamu.”
“Kwanini?” Sharifa akamuuliza.
“Kwa sababu Majaliwa si kichaa, hawezi kuiba bastola yangu na kwenda kumpiga risasi mtu asiyemfahamu na asiye na kosa naye.”
“Wakati mwingine ni mambo ya kitoto tu. Pengine wamechukuliana wasichana wakawekeana visasi.”
“Unakosea. Nimekwambia yule kijana amesema hafahamiani na Majaliwa. Hao wasichana watachukulianaje kama hawafahamiani?”
“Pengine anaficha. Usiamini kila anachokisema. Haiwezekani mtu aje kupiga risasi bure bure tu. Lazima wanafahamiana.”
“Yule kijana amesema kweli. Sioni sababu ya yeye kusema uongo. Yeye ndiye aliyeumizwa.”
“Mimi siamini.”
“Mke wangu una mawazo tofauti.”
“Majaliwa atakuja kukueleza ukweli.”
“Yuko wapi sasa?”
“Atakuja tu, hapa ni kwao. Uoga wake ukiisha atakuja tu. Hawezi kukimbia milele.”
Siku ile nayo ikapita. Asubuhi ya siku iliyofuata Wakwetu na James walikwenda tena kituo cha polisi kama walivyoambiwa na Inspekta Amour.
Walipofika James alikamatwa na kupelekwa mahakamani ambako alisomewa shtaka la kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha ajali na kujeruhi.
Alikiri makosa yote na hapo hapo alitozwa faini ya makosa mawili, la kuendesha kwa uzembe na kusababisha ajali. Hakimu akaeleza kuwa atatoa adhabu ya kosa la kujeruhi pindi mtu aliyejeruhiwa atakapowasilishwa mahakamani.
Wakwetu alilipa faini ya makosa mawili. Kosa la kuendesha kwa uzembe lilitozwa shilingi laki mbili na kosa la kusababisha ajali lilitozwa shilingi laki tatu.
Upande wa mashtaka uliahidi kumfikisha mtu aliyejeruhiwa siku iliyofuata na James alitakiwa afike siku hiyo.
Baada ya shauri hilo kuishia hapo, Wakwetu alikwenda tena hospitalini kumjulia hali Masumbuko. Aliruhusiwa kusalimiana naye tu. Baada ya kusalimiana naye, Wakwetu alimpa shilingi laki moja ili zimsaidie kwa matumizi madogo madogo kisha akamuaga na kuondoka.
Alipotoka hospitalini, Wakwetu alikwenda kazini kwake. Mchana akarudi nyumbani. Mara tu alipoingia ndani, Sharifa alimpa mfuko uliokuwa na kitu ndani.