
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali taarifa ya pamoja ya Marekani na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P-GCC), ikiitaja kuwa ni “ya kuingilia mambo ya wengine, isiyo ya kuwajibika, na ya kichochezi,” huku ikizionya nchi za eneo hilo dhidi ya kuendelea kushirikiana kwa misimamo ya uadui na Washington.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa, Iran ilijibu kwa ukali taarifa ya pamoja iliyotolewa tarehe 25 Juni 2026, na kuyatupilia mbali madai ya Washington kuhusu “azma ya kudumu ya Marekani” kwa ajili ya usalama wa nchi za Ghuba ya Uajemi, ikisema kuwa hayo si chochote ila “maneno ya kisiasa yasiyoakisi uhalisia, bali yanayopindua ukweli.”
Wizara hiyo ilisisitiza kwamba uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo umeendelea kuwa mzigo kwa wananchi wa mataifa ya eneo hilo, na kwamba ndio miongoni mwa sababu kuu zinazochochea ukosefu wa usalama.
Wizara hiyo imeashiria uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kuanzia tarehe 28 Februari hadi 8 Aprili, ambapo Marekani ilitumia vituo vya kijeshi vilivyoko katika nchi za Ghuba ya Uajemi kutekeleza mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika vita hivyo, baadhi ya nchi za pwani ya Ghuba ya Uajemi ziliruhusu Marekani kutumia ardhi yao na anga zao dhidi ya Iran. Iran ilijibu kwa mawimbi 100 ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya ngome za Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo. Iran sasa inataka fidia kutoka kwa mataifa matano ya Kiarabu kwa kuwezesha mashambulizi hayo haramu ambayo yalipelekea kuuawa shahidi Kiongozi Muadhamu, makamanda wa kijeshi, wanasiasa, wasomi na raia wa kawaida wakiwemo watoto wa shule.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema hatua ya Marekani kutumia ardhi ya nchi za Kiarabu kuishambulia Iran ni jambo linalobainisha wazi kwamba Washington haijali usalama wa mataifa ya eneo hilo wala mahusiano yao baina yao.
Wizara hiyo ilizikumbusha nchi wanachama wa baraza hilo la Kiarabu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kanuni ya ujirani mwema. Pia ilizihimiza “kuzuia matumizi yoyote ya ardhi na miundombinu yao na upande wa tatu kwa ajili ya kupanga, kuandaa, kuunga mkono, na kutekeleza vitendo visivyo halali, vikiwemo mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Iran pia imekosoa kurudiwa kwa “uongo mkubwa” uliobuniwa na Marekani na “utawala wa Kizayuni unaotekeleza mauaji ya kimbari” kuhusu programu ya nyuklia ya amani ya Iran. Badala ya kurudia vitisho vya Magharibi, wizara hiyo ilizishauri serikali za Ghuba ya Uajemi kujiunga na mpango wa Iran wa kuifanya Asia Magharibi kuwa eneo lisilo na silaha za nyuklia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madai ya kukaririwa ya “vitisho vinavyotoka Iran” ni chombo tu cha kampeni ya muda mrefu ya Chuki dhidi ya Iran au“Iranophobia” iliyoandaliwa na Marekani na utawala wa Kizayuni. Iran imesema kampeni hiyo ya Marekani inafuata ile mbinu ya kibeberu “gawanya utawale” ambayo imezinasa nchi za Ghuba ya Uajemi katika mashindano hatari na yasiyo na mwisho ya silaha, na kuligeuza eneo hilo kuwa ghala kubwa la silaha.
Muhimu zaidi, wizara hiyo ilisisitiza kwamba “amani na usalama wa kudumu katika eneo hili vinaweza kupatikana tu kwa kujenga uaminifu na ushirikiano wa pande zote kati ya nchi za eneo hili, bila kuwepo uingiliaji wa Marekani wenye uharibifu.”
Kuhusu namna makundi ya kupigania ukombozi Palestina na Lebanon yanavyotajwa, wizara hiyo ilieleza masikitiko makubwa juu ya msimamo wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi wa kwenda sambamba na Marekani na Isarel katika kuyaita makundi hayo kuwa “makundi ya niaba ya Iran.”
Badala yake, ilisema kwamba “chombo pekee cha uwakala katika eneo hili ni utawala wa Kizayuni,” ikisisitiza kuwa mapambano dhidi ya uvamizi na ubaguzi wa kimfumo ni halali chini ya sheria za kimataifa.
Taarifa hiyo pia iligusia Lango Bahari la Hormuz lenye umuhimu wa kimkakati, ikiweka lawama za moja kwa moja kwa hali ya karibuni ya ukosefu wa usalama baharini juu ya Marekani, utawala wa Kizayuni, na mataifa ya eneo yaliyosaidia kampeni yao ya kijeshi.
Tehran inasisitiza tena kwamba mlango huo wa bahari umo ndani ya maji ya eneo la Iran na Oman, na kwamba usimamizi wa meli utazingatia kikamilifu Kifungu cha 5 cha Hati ya Makubaliano ya tarehe 18 Juni, iliyomaliza vita vya hivi karibuni.
Hati hiyo ya makubaliano ya tarehe 18 Juni, iliyotiwa saini kwa njia ya mbali na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian pamoja na Donald Trump, ilitaka kusitishwa kwa kudumu kwa mapigano, kuondolewa kwa hatua kwa hatua kwa vikwazo, na kurejeshwa kwa usafiri wa kibiashara kupitia mlango huo wa bahari.
Hatimaye, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imezihimiza nchi za P-GCC kujifunza kutokana na vita vya karibuni walivyolazimishwa kuvikabili, na kufanya marekebisho katika mtazamo wao wa kiusalama, ikisisitiza tena kwamba: “Usalama wa pamoja unaweza kupatikana tu kwa ushirikiano wa nchi zote za eneo hili bila kuingiliwa na nguvu za kigeni.”