KIUNGO wa Charles M’Mombwa wa Taifa Stars ametambulishwa kwenye kikosi cha Zabbar St. Patrick inayoshiriki Ligi Kuu Malta baada ya kuachana na Floriana aliyoisaidia kutwaa ubingwa, lakini uhamisho wake umeingia kwenye utata wa kimkataba.

Hali hiyo inakuja baada ya Floriana FC kutoa taarifa rasmi ikikanusha kuachana na kiungo huyo, ikisisitiza bado ni mchezaji wao halali kwa mujibu wa mkataba unaotambulika na Chama cha Soka Malta (MFA), licha ya Zabbar St. Patrick kumtambulisha kama usajili wao mpya.

M’Mombwa aliitumikia Floriana kwa msimu mmoja akicheza mechi 32 na kufunga mabao matatu yaliyochangia ubingwa wa timu hiyo, ambayo sasa itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).

MMOMB 01

Licha ya hali hiyo, klabu yake mpya Zabbar St. Patrick ilimtambulisha na kuandika: “Charles analeta ubora, uzoefu na nidhamu kubwa ya kazi. Tunaamini atakuwa nyongeza muhimu katika kikosi chetu,” ilisema sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

M’Mombwa, 28, anajiunga na Zabbar akiwa na uzoefu mkubwa wa kucheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali, baada ya kuwa sehemu ya kikosi cha Floriana kilichokuwa na msimu mzuri Ligi Kuu ya Malta.

Uhamisho huo unaonekana kuwa hatua nyingine muhimu katika safari ya nyota huyo ambaye ameendelea kujiimarisha barani Ulaya.

Kwa sasa M’Mombwa anakadiriwa kuwa na thamani ya Euro 400,000 (zaidi ya Sh1.2 bilioni), jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wa Tanzania wenye thamani kubwa wanaocheza nje ya nchi.

MMOMB 02

Hata hivyo, uhamisho wake umekumbwa na utata mkubwa baada ya Floriana FC kutoa taarifa rasmi ikikanusha kuachana na kiungo huyo, ikisisitiza kuwa bado ni mchezaji wao halali kwa mujibu wa mkataba unaotambulika na Chama cha Soka Malta (MFA).

Kwa mujibu wa klabu hiyo, M’Mombwa alisaini nyongeza ya mkataba mapema mwaka huu ambayo ilisajiliwa rasmi na MFA mwezi Februari 2026, hivyo kuendelea kumfunga kimkataba licha ya hatua yake ya sasa ya kuhamia Zabbar St. Patrick.

Floriana FC imeeleza kuwa mchezaji huyo alikuwa sehemu ya maandalizi ya msimu mpya, aliripoti kambini na kushiriki mazoezi pamoja na mechi za kirafiki, kabla ya kuwasilisha ombi la kuachwa klabuni, hatua ambayo wameitaja kama ukiukwaji wa makubaliano ya kazi.

“Charles M’Mombwa bado ana mkataba halali wa ajira na klabu hii ambao unaendelea kutumika kikamilifu,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Floriana FC, ambayo pia iliongeza kuna klabu nyingine na wahusika wa tatu wanaodaiwa kumshawishi mchezaji huyo kuvunja mkataba wake.

Licha ya hali hiyo kuendelea, M’Mombwa hajatoa kauli yoyote hadi sasa, na Mwanaspoti ilifanya jitihada za kumtafuta yeye pamoja na watu wake wa karibu, lakini juhudi hizo ziliingia mchanga.

M’Mombwa aliyezaliwa DR Congo na kukulia Tanzania kabla ya kuhamia Australia ambako alikuza kipaji chake cha soka.

MMOMB 01

Kiungo huyo alianza kukuza kipaji chake katika akademi ya Central Coast Mariners kabla ya kupanda hadi timu ya wakubwa na baadaye kujiunga na Macarthur FC, ambako alicheza zaidi ya mechi 70 katika Ligi Kuu ya Australia (A-League).

Pia aliwahi kuitumikia Newcastle Jets kabla ya kuhamia Malta mwaka 2025 ambako alipata nafasi ya kucheza mashindano ya Ulaya kupitia UEFA Conference League.

Kwenye timu ya Taifa, kiungo huyo ameichezea Tanzania mechi 19 na kufunga mabao manne. Mechi yake ya kwanza mwaka 2023 aliandika historia kwa kufunga bao la ushindi kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya Niger katika hatua za kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Tangu hapo ameendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Tanzania katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, AFCON na mechi mbalimbali za kirafiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *