Dar es Salaam. Kutokana na fani yake, Baba Levo alionekana kama anayetekenya watu mbavu zao. Hatuwezi kubishana, ni kweli alikuwa akichekesha. Lakini alikuwa akimchekesha mtu aliyenasa kwenye mtego wake mwenyewe.
Labda mtu huyo alikuwa akimtamanisha simba wa sabasaba kwa mshikaki, kwa uchu simba akaurukia na kwa bahati mbaya akaondoka na mkono mzima. Sasa kituko hicho umsimulie mhanga wa tukio hilo.
Umeshawahi kumwona mtu akiugulia kwa kubana kicheko? Iko hivi: mtu anaweza kukichekesha kikundi cha watu. Lakini kumbe miongoni mwa watu hao, yumo anayehusika moja kwa moja na kichekesho hicho.
Yaani yeye ndiye anayechekwa. Sasa kwa kuwa umati wote unacheka, na yeye atajilazimisha kucheka. Lakini tofauti ni kwamba kicheko chake kinaweza kuambatana na machozi.
Usishangae. Kicheko halisi huanzia kwenye misuli ya tumbo, hupanda kifuani na kutokea mdomoni. Lakini kicheko cha maumivu huzuiwa tumboni.
Wanaochekea tumboni huwa wanazuia kucheka mambo yanayowahuzunisha. Lakini wakizidiwa, kicheko hupanda kwa maumivu makubwa. Ni sawa na mtu aliyezuia kikohozi kwa muda mrefu, lakini ghafla kikamponyoka. Usitake nitoe mfano wa hewa chafu!
Sasa wakati “Rais wa Machawa” akiendelea kutoa hoja zake, sura za wapokeaji zilikuwa zikionesha hali ya “ustake nicheke”, au “tunacheka lakini basi tu…”
Hasa pale alipoyaeleza ya wanaume kusomesha wanawake kwa matarajio ya uenza, ama kusingiziwa watoto. Alibainisha kuwa ugomvi baina ya mume na mke unaweza kuibua neno kutoka kwa mama kama “kwanza watoto hawa si wako!”
Sijui kwa nini wanawake hawataki. Wakati msemaji akieleza, wabunge hasa wanawake walikuwa wakishindwa kuyapokea mazito hayo. Lilikuwa kama jiwe lililotupwa gizani, kilio cha mlalamikaji itaashiria kupigwa na jiwe hilo.
Waheshimiwa wakahanikiza kutoa taarifa juu ya kile alichokuwa akikisema, hata hivyo Mwenyekiti ambaye ni mwanamke mwenzao aliwazuia kwa kuwaasa wavumilie maumivu ya sindano, kwani ndio tiba.
Bingwa akaja na kubwa zaidi: Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imejikita katika kumtetea mwanamke kwa kuinamisha mzani.
Elimu inasambazwa kupitia vipindi vya redio na TV, lakini vinaporushwa hewani ni kama vinawafundisha wanawake jinsi ya kupambana na waume zao. Huu unakuwa mwanzo wa ndoa na mahusiano kuparaganyika.
Hakuna mtoto wa kiume aliye mnyonge kwenye himaya yake. Chukua mfano wa mbwa koko, unaweza kumfukuza kote lakini si kwenye uwanja wake. Ieleweke kuwa mtoto wa kiume huwa karibu na mama yake kwa sababu anajisikia kumlinda.
Anatiwa uchungu na mateso ya baba mlevi, au wanaume wakatili dhidi ya mama yake. Ndiyo maana mwanaume humwambii kitu juu ya mama, mkewe na bintiye.
Kila mtoto wa kiume huwa na kawaida ya kujenga himaya thabiti ili kulinda utawala wake. Mambo haya ni urithi wa dunia, ambapo ustaarabu wa mwanaume ni kuondoka kwenye himaya ya baba na kuanzisha ya kwake.
Kadhalika yapo hata kwa wanyama wa mwituni na wa kufugwa. Wengine kama majogoo huamini kuwa hahitajiki jogoo mwingine wakati yeye anatimiza majukumu.
Mheshimiwa huyo msanii alikumbusha kuwa mwanaume anaoa mwanamke kulingana na jinsi anavyopenda. Yupo anayeoa mwanamke mfanyakazi wa kusaidiana naye majukumu, au mama wa nyumbani wa kulea watoto.
Ananikumbusha kuwa mamwinyi walioa idadi kubwa ya wanawake kama raslimali watu. Hawa ndio waliohodhi ardhi na kuzalisha mali kupitia kilimo.
Wakati hoja ilielekea kutamatika, waheshimiwa wabunge walionekana kuipokea kwa sura tofauti. Najaribu kuvuta sura za wezi watatu waliokwenda kuiba dukani kwa mwarabu usiku.
Wa kwanza alipenyeza mkono wake dirishani, mwarabu aliyekuwa ndani akakata kiganja cha mwizi! Upesi mwizi alichomoa mkono na kuuficha mgongoni. Akamwelekeza kwa macho mwizi wa pili, kuwa yeye amefanikiwa na sasa ni zamu yake.
Wa pili naye akapoteza kiganja kwa mtindo ule ule, akafanya kama wa kwanza kumuashiria wa tatu amalizie. Mwizi wa tatu alipoingiza mkono na kukutana na ajali ile, hakustahimili. Alipiga yowe:
“Mama mkono wangu!” Palepale wezi wale wawili walimcheka na kumwonesha mikono yao, “hata sisi yametukuta!” Hapo najaribu kujumlisha vicheko vyao na maumivu ya kukatwa viganja, tena kwa jambia.
Lakini mwisho wa siku mada ilihitimishwa kwa funzo kuu: Unapofundisha kuepuka unyanyasaji wa kijinsia, ni lazima uwafundishe wahusika kuutambua na kuuepuka.
Zipo sehemu ambazo mtoto wa kike akiimba “Nauli yake nakula lakini siendi…” ataonekana shujaa, lakini wa kiume angeimba jinsi alivyomkomoa baada ya kumnasa aliyekula nauli yake, angefungiwa na BASATA na kisha Wizara ingelikuja na hatua kubwa zaidi.
Ipo dhana kuwa wakati wa kuhangaika na mtoto wa kiume umekwisha. Au pengine wanaona jinsi wanaume walivyoweza kujisimamia kwa muda mrefu, sasa wanaona baada ya nchi yetu kupata akinamama wengi kwenye nafasi za uongozi, umefika wakati wa kukumbuka neno “kutesa kwa zamu”.
Wanasahau kuwa hata mwanaume anahitaji ulinzi, pengine zaidi ya mwanamke kwa sababu yeye ni kiongozi wa familia. Yeye ndiye anayemchukua mwanamke kutoka kwa wazazi wake, ndiye anayeanzisha familia na akailea na kuitunza ikiwa mabegani mwake. Labda wanaume wengine wanapotea, si kigezo cha kumshusha kila mwanaume.