
Dar es Salaam. Moja ya mambo yaliyoua bendi nyingi za zamani ilikuwa ni ziara za bendi. Hapa nieleze baadhi ya mikasa iliyosababisha vifo vya baadhi ya bendi.
Kwa vile bendi zilikuwa zikitegemea viingilio kwenye maonyesho yao, bendi zililazimika kufanya maonyesho mengi.
Ratiba za bendi kwa ujumla zilianza Jumanne saa nne asubuhi. Kila mwanamuziki alilazimika kuwepo kwenye eno la mazoezi kufikia saa hiyo, na kulikuwa na daftari la kuratibu uchelewaji.
Siku hizo za Jumanne baadhi ya bendi zilianza kwa kuangalia mema na mabaya yaliyotokea katika wiki iliyopita. Hapo zilijadiriwa nyimbo mpya ambazo zilionekana kutokukubaliwa na mashabiki.
Walijadiliwa wanamuziki walio vunja sheria mbalimbali, kama vile kuchelewa jukwaani wakati nyimbo imeanza, ulevi, pengine kama muhusika hakuvaa sare wakati onyesho lilikuwa na ulazima wa kuvaa sare na kadhalika. Baada ya vikao vya aina hiyo, mazoezi yaliendelea.
Mazoezi ya bendi yalikuwa yakifanyika Jumanne na Jumatano, japokuwa kama ilikuwa ni wakati wa kutayarisha nyimbo za kurekodi, mazoezi yaliweza kufanyika mpaka Ijumaa.
Kwa wiki zile ambazo hakukuwa na mazoezi, maonyesho yalikuwa yakifanyika kila siku kuanzia Jumatano hadi Jumapili, Jumatatu kwa kawaida ilikuwa siku ya mapumziko.
Mazoezi hayakuwa ya mchezo, bendi ilitakiwa kuwa na nyimbo nzuri ili watu washawishike kuifuata na kulipa kiingilio. Mashabiki walikuwa na upenzi mkubwa wa bendi, haikuwa ajabu bendi kuwa na onyesho Kinondoni lakini ukakuta mshabiki ametoka Ukonga kwa taxi kuja kupata burudani ambayo pia atalipia kiingilio.
Walikuweko hata mashabiki ambao walisindikiza bendi kama zilikuwa na maonyesho miji ya karibu kama Bagamoyo na Morogoro. Na hata huko walilipa kiingilio.
Dar es Salaam kulikuwa na ushindani mkubwa kwani katika siku nilizozitaja kulikuwa na bendi zaidi ya thelathini zinafanya maonyesho kila siku. Kila bendi ilijitahidi kupiga muziki mzuri kuliko nyingine, kinyume cha hapo ni njaa kwa wanamuziki wake.
Bendi zilikuwa zikipata kipato kizuri sana zilipoenda kupiga nje ya Dar es Salaam, kule kulikojulikana kama mikoani.
RTD ilikuwa na utaratibu wa kurusha nyimbo mpya zilizorekodiwa katika studio zake katika kipindi kilichoitwa Misakato. Kwa vile radio ilikuwa moja tu, kipindi cha Misakato kilisikika nchi nzima. Bendi nyingi zilianza kufanya ziara baada ya kipindi cha misakato.
Bendi zilizokuwa chini ya mashirika, au taasisi mbalimbali zilikuwa na mipango mizuri ya ziara. Kwanza ratiba zao zilipangwa vizuri, zilieleza mwanzo na mwisho wa ziara. Wanamuziki walipewa posho zao za safari nzima kabla ya safari.
Kwa ujumla kwa wanamuziki wa bendi hizi, safari lilikuwa jambo lililokuwa na manufaa kifedha, hata kama maonyesho yao hayakuingiza fedha.
Shida kubwa ilikuwa kwa bendi za watu binafsi. Kwa kuwa wenye bendi wengi hawakuwa na mtaji mkubwa wa kuweza kugawa posho kwa wanamuziki wao, bendi zilipotaka kufanya ziara zilijitahidi kukusanya fedha ya kuanzia safari tu.
Mara nyingi matayarisho yao yalikuwa ni nauli za wanamuziki kufikia kituo cha kwanza, fedha za kusafirisha vyombo na pengine posho ya siku moja au mbili.
Safari hizi zilikuwa zikijulikana siku ya kuondoka tu, lakini siku ya kurudi ilikuwa ni majaliwa. Bendi hizi zilikuwa zikitegemea kufanya maonyesho na kutokana na mapato hayo, wanamuziki waweze kuishi na pia kuendelea na safari.
Tatizo lilianza pale ambapo hayakupatikana mapato ya kutosha. Hapo ndipo bendi ililazimika kukwama. Bendi nyingine zilijikuta zikikaa hata mwezi mmoja katika mji mmoja, na kujaribu kupiga kukusanya chochote kuendela na safari, japo kupata nauli ya kwenda mji unaofuata kujaribu tena bahati.
Mambo yalipozidi ndipo kutimka kwa wanamuziki kulianza, kila mtu akijitahidi binafsi kurudi nyumbani.
Kama ungeweza kukutana na wenye nyumba za kulala za zamani watakuhadithia walivyolazimika kukubali kupokea spika au amplifaya kama malipo ya malazi ya wanamuziki waliokwama.
Bendi nyingi zilikuwa na meneja ambaye kazi yake ilikuwa kutangulia wiki moja au mbili kabla ya ziara kufanya mipango. Akisha ondoka njia pekee ya haraka ya mawasiliano ilikuwa kwa simu.
Simu za zamani zilikuwa ni za mezani hivyo ilikuwa lazima mtaarifiane ni muda gani meneja atapiga simu ili aweko mtu wa kupokea simu hiyo, la sivyo kulikuwa nashida kubwa ya mawasiliano kati ya bendi na mtu aliyetangulia.
Kukosekana kwa mawasiliano kulisababisha bendi ikajikuta imetua kwenye mji ambao ilitarajia meneja angekuwa amefanya mipango na kukuta hakuna mipango yoyote, hapo njaa hunyemelea bendi.
Bendi maarufu kulala ukumbini, au kituo cha basi au treni halikuwa jambo geni.
Nakumbuka bendi moja iliyokufa kwa kuwa kulikuweko makubaliano kati ya wanamuziki waliokuwa wakisafiri na mwenye bendi, kuwa kila wiki atatoa posho kwa familia za wanamuziki waliosafiri.
Bendi ilisafiri salama na ziara ilikuwa na faida kubwa kwa mwenye bendi, hatimaye bendi ikarudi, tatizo kila moja akakuta familia yake ikiwa katika hali mbaya kwani ‘tajiri’ hakutimiza ahadi yake ya kutunza familia.
Kundi kubwa la wanamuziki likahama bendi hiyo, wengine wakajiunga na bendi mpya iliyokuja kuitwa Dar es Salaam International Orchestra.
Jambo jingine lililosababisha bendi kufa, lilikuwa wafanyabiashara mkoani kukodi bendi. Bendi zilipokodiwa, aliyekodisha alifanya biashara mbili katika onyesho, aliendelea na biashara yake ya kuuza vinywaji na pia alikusanya kiingilio kwa waliokuja kucheza na kusikiliza muziki.
Tatizo lilikuwa linatokea pale biashara inapokuwa mbaya, au kwa uwezo wa Mungu, mvua kubwa inanyesha siku ya aonyesho ambalo gharama kubwa ya kulitayarisha imeshafanyika, hili pia lilikuwa linaifikisha bendi kukwama.