
Ripoti kutoka Ukanda wa Gaza zinasema kuwa chombo kimoja cha kuchimba vifusi (excavator) tu kinatumiwa kutafuta karibu miili ya watu 8,500 na mabaki yaliyo chini ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa na jeshi la Israel wakati wa vita vya mauaji ya kimbari katika eneo hilo.
Vikosi vya Ulinzi wa Raia, kwa msaada wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, vilianza tena shughuli za uokoaji Jumamosi vikiwa na uwezo mdogo sana, huku kukiwa na maonyo kwamba kuendelea kufanya kazi ya kutafuta maiti za wahanga wa vita vya Israel kwa kasi hii kunaweza kuchukua miaka mingi.
Operesheni ya kutafuta miili ya watu chini ya vifuusi vya nyumba za raia huko Gaza ilikuwa imesimamishwa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na uhaba wa mafuta na vifaa vizito vya shughuli hiyo.
Vita vya mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza, vilivyosita chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano Oktoba 10, 2025, vimeua shahidi Wapalestina 73,000 na wengine zaidi ya 173,000 walijeruhiwa. Majeshi ya Israel pia yamesababisha uharibifu mkubwa ulioathiri takriban 90% ya miundombinu ya raia, jambo ambalo limetatiza operesheni za kuopoa maelfu ya maiti zilizonaswa chini ya vifusi.
Timu za Ulinzi wa Raia zimeanza kazi kwa kutafuta miili ya mashahidi 8 chini ya vifusi vya nyumba ya familia ya Ghabboun katika kitongoji cha Sabra, ambayo ililipuliwa na Israel Oktoba 2025.
Msemaji wa Ulinzi wa Raia huko Gaza, Mahmoud Basal, ameiambia Anadolu kwamba shughuli za uopoaji zinaendelea polepole sana, kutokana na matatizo makubwa yanayotokana na ukosefu wa rasilimali na vifaa vizito.
Ameongeza kuwa takriban miili na mabaki 8,500 ya watu wa Gaza bado iko chini ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza, akieleza kuwa kuna vikwazo vingi vinavyozuia kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na uhaba wa vifaa na hatari zinazoweza kutokea uwanjani.
Amesema: “Kuendelea kufanya kazi kwa njia hii ya mwendo wa kinyonga kutachukua miaka mingi, kwani tunafanya kazi kwa kutumia chombo kimoja ambacho kinaweza kuharibika wakati wowote,” akibainisha kwamba ikiwa mashine nzito zitapatikana, “kipindi cha kazi hii hakitazidi miezi 3.”
kandokando ya shughuli za utafutaji wa miili ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Israel, mtoto Mohammed Riyad Ghabboun mwenye umri wa miaka 12 anasubiri kwa hamu kurejeshwa mabaki ya wanafamilia kadhaa aliowapoteza miezi minane iliyopita.
“Nina hisia mchanganyiko za hamu na huzuni wakati huu wa mchakato wa kutafuta miili ya wanafamilia wangu, ambao wametoweka kwa miezi minane,” anasema Ghabboun, ambaye alijeruhiwa na kutolewa kwenye kifusi cha nyumba yake baada ya shambulio la makombora la Israel.
Mtoto huyo ameliambia shirika la habari la Anadolu Agency kwamba: “Tangu wakati huo nimekuwa katika hali ya kutarajia na huzuni, na natumai kwamba nitaweza kuona miili yao na kuisitiri kwenye makaburi yao.”