Tamko la kuzuia mikutano ya hadhara ni jaribu la utawala wa sheria

Mjadala mzito unaendelea katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kuhusiana na tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi ya kuzuia kwa muda, mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.

Ukifuatilia mijadala hiyo inayohusisha baadhi ya viongozi wa kisiasa, wa dini,  wanaharakati, wanasheria, na hata wananchi wa kawaida, utapata hitimisho moja kubwa tu kwamba tamko hilo na jaribu katika utawala wa sheria.

Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa, maana ya utawala wa sheria ni kwamba hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia rais wa nchi mpaka mimi mnyonge niliye hapa mtaa wa Relini kata ya Bomambuzi.

Kwa maneno mengine, kuanzia Dola ya nchi mpaka kaya iliyopo kwenye kijiji kidogo kabisa ambacho jina lake halijulikani isipokuwa wenyeji wake. Kwa ufupi ni kwamba kila chombo cha Dola, taasisi, mtu anawajibika kwa sheria.

Ukisoma mjadala utagundua kuwa hakuna mtu anayepinga sababu za kuchukua hatua hiyo ambazo ni uwepo wa tishio la usalama kuelekea Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (77), lakini hoja ni je, aliyelitoa ana mamlaka hayo kisheria?.

Mwaka 1765, Jaji mkuu wa Uingereza, Lord Camden akizungumzia watawala kufuata sheria alisema “lf it is the law, it will be found in our books. lf it is not to be found there, it is not law,” kwa tafsiri yangu ni kwamba kama ni sheria basi ni lazima tuione kwenye vitabu vya sheria, na kama haipo, basi hiyo sio sheria.

Tujiulize, tamko la Waziri Katambi la kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa nchi nzima, ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Katiba yetu ya mwaka 1977 na sheria zetu yeye amepewa nguvu hiyo na sheria gani?

Ibara ya 20(1) ya Katiba hiyo inasema kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani.

Ukisoma Ibara ndogo ya (3) inasema Bunge linaweza kutunga sheria inayoweka masharti yatakayohakikisha kuwa vyama vya siasa vinazingatia mipaka na vigezo vilivyowekwa kuhusu uhuru na haki ya watu kushirikiana na kujumuika.

Ni kutokana na takwa hilo la Kikatiba, Bunge letu lilitunga Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 na ikafanyiwa marekebisho kadri haja ilivyojitokeza.

Sasa ukisoma kifungu cha 23(1) cha sheria hiyo kinasema kila chama cha siasa kilicho na usajili wa muda au usajili wa kudumu kitakuwa na haki ya kufanya na kuhutubia mikutano ya hadhara kwa ajili ya kujitangaza na kuomba wanachama.

Kifungu kidogo cha (4) kinasema endapo kinataka kufanya mkutano au maandamano, kinatakiwa si chini ya saa 48 kabla ya mkutano au maandamano kiwasilishe taarifa ya maandishi kwa Ofisa wa Polisi anayesimamia eneo hilo.

Ikiwa mkutano au maandamano yaliyotolewa taarifa yanaashiria uvunjifu wa amani au kuathiri usalama wa umma katika eneo hilo, Ofisa huyo ambaye mara nyingi ni mkuu wa polisi wa wilaya, atazuia kufanyika kwa mkutano.

Maudhui ya kifungu hicho pia yapo pia katika kifungu cha 43(1) cha Sheria ya Polisi na Polisu Wsaidizi na suala hilo la kuzuia mikutano ni la OCD.Waziri mwenye dhamana wala IGP hatajwi, Polisi kuzuia mikutano kwa tamko la Waziri Katambi ni kinyume cha sheria.

Sasa kulingana na sheria yetu hiyo, hakuna mahali Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi anaingia, isipokuwa ni Ofisa wa Polisi, ndio maana nimetangulia kusema utawala wa Sheria upo katika majaribu makubwa juu ya kauli ya Katambi.

Agizo la kuzuia mkutano wa hadhara linapaswa kutolewa na mkuu wa polisi wilaya tena kwa maandishi kwa chama cha siasa au mtu aliyewasilisha ombi hilo. Zuio hilo lingeweza kutolewa na Kamanda wa Polisi (RPC) mmoja mmoja katika eneo lake.

Ni lazima tukubaliane kuwa nchi hii haiongozwi kwa matamko bali kwa kufuata sheria, kwa hiyo tamko la Waziri Katambi halina miguu ya kusimamia kwa sababu hana mamlaka hayo lakini linaathiri haki za kikatiba za mamilioni ya Watanzania.

Bahati mbaya sana, mara tu baada ya tamko hilo, OCD wa Urambo alitekeleza agizo hilo na kufuta mikutano ya Chadema akisema amefanya hivyo kutokana na maelekezo ya Serikali (Katambi) na sio tena vitisho vya usalama eneo lake.

Ni jambo la hatari sana kwa waziri kuwa na mamlaka ya kupoka haki za Kikatiba za wananchi kujumuika pamoja na kutoa mawazo yao tena waziri anatoa tamko la kuzuia mikutano nchi nzima kana kwamba kuna hatari ya nchi kuingia vitani.

Hata kama tungekuwa tunaingia vitani, ni Rais pekee mwenye mamlaka ya kutoa tangazo la kusitisha shughuli ambazo zipo kwa mujibu wa Katiba.

Tamko hili la waziri Katambi halina tofauti na lililotolewa na Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli (marehemu) mwaka 2016 ambalo lililaaniwa na kupingwa vikali na wapenda demokrasia, leo tunarudi kulekule.

Kwa nini Serikali na Jeshi la Polisi wasihangaike na hicho kikundi cha watu kinachodaiwa kinataka kuvuruga amani Julai 7 (ambao ni wajibu wa Polisi), na badala yake, inatoa amri zinazovunja Katiba ya nchi na haki ya raia wema.

Jeshi letu la Polisi limekuwa na intelijensia imara sana, ninachoshauri mimi, agizo la waziri Katambi lifutwe, halafu ma-OCD kwa kuzingatia sheria ile ya vyama vya siasa na PGO, ndio wafanye maamuzi maeneo yao, sio kwa nchi nzima.

Lakini, Jeshi la Polisi liimarishe ulinzi siku hiyo ya sabasaba, na vyama vya siasa kwa busara na uzalendo vifute mikutano ya hadhara kwa siku hiyo ili kuvipa vyombo vya usalama, kazi rahisi na nyepesi ya kulinda raia na mali zao.

Mbona kulipokuwa na tishio la kufanyika kwa maandamano Desemba 9, 2025 siku ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru Jeshi letu la Polisi liliweza kudhibiti hali ya usalama, leo linashindwa nini kuimarisha doria siku hiyo ya Sabasaba.

Nimefurahishwa sana na uamuzi wa Chama ACT Wazalendo, kuamua kwenda mahakamani kupata tafsiri ya kisheria juu ya tamko hilo la Waziri Katambi na uhalali wa kisheria wa tamko hilo, japo njia hiyo inaweza kuwa ni ndefu.

Kwa sababu kama alivyosema Jaji Lord Camden, kama sheria (tamko) haliko katika vitabu vyetu vya sheria basi hiyo sio sheria, kwa sababu nguvu ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano wamepewa ma-OCD sio kwa amri ya jumla.

Viongozi wetu ni lazima wawe wanajiuliza kabla ya kutenda kuwa unachofanya kipo kwenye sheria? Kama kipo basi itaangaliwa iwapo kweli sheria hiyo imezingatiwa. lwapo hakuna sheria, basi hata udhuru wa kujitetea haupo.

Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua na katika kila uamuzi wanaochukua, basi kama Tangazo la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linavyosema, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.

Nguvu kubwa inayotumika kuzuia mikutano ya hadhara ingetumika kutatua changamoto zinazoibua hasira na chuki za visasi ambazo ni pamoja na kuendelea kwa matukio ya utekaji na kupotea kwa watu na kukandamiza haki.

Ninatamani kipindi hiki tukitumie kutafuta majawabu ya lini mchakato wa kuandika Katiba mpya ambayo ni shirikishi utaanza ili kupatikana pia kwa chombo huru cha uchaguzi kwani siku 1,580 kufikia uchaguzi mkuu 2030 haziko mbali.

Muhimu sana, Katiba yetu iwe na Ibara inalinda ukuu wa Katiba, na iweke adhabu kwa kiongozi au mtu yeyote atakayevunja ibara yoyote ile kama ilivyo kwa ya Ghana ya mwaka 1992 ambayo inachuliwa kama moja ya Katiba bora.

Hiki ni kipindi cha kutafuta majawabu ya namna ya kuendesha chaguzi zetu kwa haki kwamba mgombea anayechaguliwa na wananchi ndiye anatangazwa na haki ionekane katika mchakato wote kuanzia kampeni, upigaji kura na matokeo.

Ni kipindi cha kutafuta majawabu ya ukamataji holela (arbitrary arrest) unaofanywa na baadhi ya polisi, tutafute majawabu ya watuhumiwa kushikiliwa vituo vya siri vya polisi na kwa muda mrefu na pia haki ya kuwasiliana na ndugu.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *