
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema mapema Julai mwaka huu, ofisi yake itafanya mapitio ya kina kubaini taasisi za umma zinazotakiwa kukatiwa au kupunguziwa utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.
Aidha, amesema kwa kipindi cha miaka mitano, utegemezi wa ruzuku za Serikali kwa taasisi zisizo za kibiashara umepungua kwa wastani wa asilimia 12.8.
Mchechu amesema hayo leo, Jumanne, Juni 30, 2026, alipozungumza katika Siku ya Gawio, ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ni mgeni rasmi.
Amesema hilo wanatarajia kulifanya kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, kuhakikisha Serikali inazikatia au kuzipunguzia baadhi ya taasisi utegemezi, hasa kwenye fedha za mishahara na matumizi ya kawaida.
“Hili tunatarajia kwamba tutafanya mapema Julai kwa sababu tunafikiri pia hiki kipindi, kwa uchumi ulivyo na mambo yanavyoelekea, lazima twende katika hali ya kujifunga mkanda na kujitegemea zaidi ndani kuliko misaada,” amesema.
Mikopo inaongeza mitaji
Katika hatua nyingine, Mchechu amesema mikopo inayochukuliwa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hukuza mitaji ya mashirika ya umma na kuzalisha faida kwa nchi na wananchi.
Ametolea mfano mkopo uliotumika kujenga miradi kama Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP), akisema miradi hiyo inapokamilika, fedha hizo hugeuka kuwa mtaji wa kuwezesha mashirika ya umma.
Amesema wakati Rais Samia alipoingia madarakani, mtaji wa taasisi zote za umma ulikuwa Sh67 trilioni, lakini sasa umefikia Sh92 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 37.
Kiasi hicho cha ukuaji wa zaidi ya asilimia 20, amesema, ni mchanganyiko wa mambo mengi, ikiwemo mikopo ambayo Serikali inachukua kuwekeza kwenye mashirika, uzalishaji na kukua kwa mitaji.
“Hata huku tulipo, tunapojenga Reli ya Kisasa (SGR), sasa hivi ni mkopo, lakini SGR itakapokamilika, fedha yote itatumika kama mtaji ndani ya Shirika la Reli (TRC),” amesema.
Ameeleza kuwa vivyo hivyo hata kwa fedha za mkopo wa ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JHPP), na kwamba miradi yote itakapokamilika, mtaji utafikia Sh130 trilioni.