YANGA imebeba bingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tano mfululizo, baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 3-0, ikijihakikishia ufalme huo siku ya mwisho ya kufunga msimu ikikusanya pointi 75.

Ilihitaji sare tu Yanga kubeba ubingwa huo baada ya kutofautiana na Simba pointi mbili, lakini ikaibuka na ushindi huo mkubwa na kuiacha Simba kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 73.

Wenyeji JKT waliuanza mchezo huo kwa kujenga hali ya kujiamini wakitumia dakika moja na nusu kucheza pasi fupifupi kwenye eneo lao huku Yanga ikiwasubiri kuvuka kuja kwao.

Yanga ikafika vizuri lango la JKT dakika ya tano krosi nzuri ya beki wa kulia Yao Kouassi ikashindwa kufika kwa Laurindo Aurelio ‘Depu’ akitaka kufunga kwa mtindo wa ‘acrobatic’.

Dakika ya nane Yanga ikafanikiwa kufungua mlango wa mabao kupitia mshambuliaji Prince Dube.

Achana na bao hilo, kazi nzuri utasifia kilichofanywa na kiungo Maxi Nzengeli ambaye aliupokonya mpira karibu na katikati ya uwanja kisha kuwatoka wachezaji wanne wa JKT, akatengeneza pasi safi ya mwisho iliyomaliziwa na Dube.

Yanga ikatengeneza nafasi nyingine nzuri dakika ya 17 ikitumia upande wa kushoto, krosi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ inatua eneo zuri kwa Depu, lakini kichwa alichopiga, mpira ukapaa.

Wageni wakafanya shambulizi lingine zuri dakika ya 22, Pacome Zouzoua akaunasa mpira sehemu nzuri na kukimbia nao lakini akajaribu kumpiga chenga kipa Ramadhan Chalamanda aliyeugusa mpira na kushindwa kufunga lakini shuti lake alipojaribu kufunga kwa mara ya pili likapaa.

Yanga ikapata pigo dakika ya 45 baada ya Pacome kupata jeraha la kifundo chake cha mguu wa kushoto alipochezewa vibaya na beki Hassan Wahabi.

Wakati Pacome akisaidiwa na madaktari baada ya kuumia, wachezaji wa timu zote walionekana kuumizwa na tukio hilo wakijiziba uso na kusikitika.

Tukio hilo awali mwamuzi Katanga Hussein alionyesha kadi ya njano lakini baada ya taharuki na kuangalia hali ya Pacome akaifuta kadi hiyo na kuonyesha nyekundu kwa Wahabi.

Pacome baada ya tukio hilo, alipandishwa kwenye gari la wagonjwa na kuwahishwa hospitali huku viongozi wa Yanga, Rais Hersi Said, Makamu wake Arafat Haji na wajumbe Alexander Ngai wakiimfuata kwenye gari na kumfariji kabla ya kuondoka.

Mchezo huo ukaenda mapumziko Yanga ikiongoza kwa bao 1-0.

CHOPA YAWARUDISHA MCHEZONI YANGA

Baada ya tukio la Pacome, mashabiki wengi uwanjani walionekana kuwa na nyuso za huzuni wakilaumu kwa namna kiungo huyo alivyoumizwa.

Hata hivyo, ile chopa iliyokuwa imebeba kombe ikaanza kuzunguka uwanjani hapo na mashabiki kubadilika na kushangilia, hali iliyobadilisha uwanja kurudi kwenye furaha dakika chache kabla ya kuanza kwa kipindi cha pili.

Yanga ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 50 likifungwa na Maxi akimalizia krosi safi ya chini kutoka kwa Allan Okello.

TSHABALALA AINUA KITI KAMA KOMBE

Wakati Yanga wakishangilia bao hilo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alionekana kuinua kiti cha plastiki kilichokuwa pembeni ya uwanja mithili ya kuinua kombe huku akishangiliwa na mashabiki.

Yanga ikapata bao la tatu dakika ya 68 likifungwa na Depu, akimaliza vizuri alipopokea pasi, kisha kuvua jezi yake na kuifuata ile ya Pacome na kuinyoosha juu kwa mashabiki ikiwa ni ishara ya kumtakia apone haraka.

YANGA MABAO 10 VS JKT

Ushindi huo wa Yanga wa mabao 3-0 yanaifanya timu hiyo kuifunga JKT kwa jumla ya mabao 10-0 ndani ya msimu mmoja katika mechi tatu za mashindano tofauti.

Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 lakini timu hizo zikakutana tena kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB na Yanga ilishinda 2-0 hapohapo Isamuhyo, leo ikaruhusu tena mabao 3-0 na kufanya jumla kufungwa mabao 10-0.

KMC YAAGA NA KIPIGO

Simba imehitimisha msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara ikimaliza nafasi ya pili baada ya kuifunga KMC bao 1-0 ambayo imeaga rasmi kwa kipigo kufuatia kuwa timu ya kwanza kushuka, kabla ya kuungana na Mtibwa Sugar.

Bao la Simba lilifungwa dakika ya 55 kwa penalti kupitia Inno Jospin Loemba baada ya Antony Mligo kufanyiwa madhambi ndani ya boksi.

Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkali, licha ya Simba kushambulia mara kwa mara, lakini walikutana na ugumu wa vizuizi vya wachezaji wa KMC ambao walikuwa wanajaa ndani ya 18 na kuhakikisha wanaondoa hatari zilizokuwa zinawakabili.

Kwa KMC ilikuwa mechi ya kuhitimisha safari ya Ligi Kuu na kwenda kuanza chalenji mpya ya Ligi ya NBC Championship msimu ujao wa 2026-2027.

KMC haikuwa na msimu mzuri katika mechi 30 ilizocheza, imeshinda mbili, sare tatu na kupoteza 25. Imeruhusu mabao 53, yenyewe ikifunga mabao 16 na kukusanya pointi 9.

AZAM YAMALIZA KIBABE

Mabao mawili yaliyofungwa na Jean-Jacques Ngita dakika ya 66 na Nathaniel Chilambo dakika ya 89 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, yameifanya Azam kumaliza kibabe msimu ikiwa nafasi ya tatu na pointi 62.

Azam katika mechi hiyo ilifanya mabadiliko makubwa takribani wachezaji sita walianza kikosini, Fuentes Mendoza na Adolf Mtasingwa waliingia baada ya kukaa nje muda mrefu wakiuguza majeraha.

Kiungo James Akaminko ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa akianzia benchi leo alianza akichukua nafasi ya Himid Mao ambaye alikuwa jukwaani akishuhudia mchezo huo.

Vilevile wachezaji watatu muhimu wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Lusajo Mwaikenda na Idd Nado wote wakianzia benchi.

MTIBWA YARUDI CHAMPIONSHIP

Kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, wenyeji Namungo wameishusha daraja Mtibwa kwa kichapo cha mabao 2-1, matokeo ambayo yameifanya Mtibwa kumaliza nafasi ya 15 na kushuka daraja moja kwa moja ikiungana na KMC. Mtibwa ilipanda daraja msimu huu na sasa inarejea ilipotoka kwenda kujipanga upya.

Mabao ya Geoffrey Luzendaze dakika ya 33 na Jacob Masawe dakika ya 85, yalitosha kuishusha Mtibwa ambayo ilianza kufunga kupitia Ismail Mhesa dakika ya pili. Mtibwa imemaliza na pointi 27.

PLAYOFF NI DABI YA MBEYA

Tanzania Prisons na Mbeya City, zimemaliza nafasi ya 13 na 14 ambapo sasa zinalazimika kwenda kucheza mtoano ‘playoff’ kupambania kubaki ligi kuu.

Playoff hiyo itakuwa na mvuto wa aina yake kwani itapigwa Dabi ya Mbeya, mshindi atabaki ligi kuu, atakayepoteza anakwenda kucheza na mmoja kutoka Championship.

Prisons imemaliza nafasi 13 ikikusanya pointi 32 baada ya kuifunga Mashujaa bao 1-0 kupitia Lulihoshi Heritier dakika ya 90 kwa penalti, huku Mbeya City ikimaliza nafasi ya 14 ikitoka 0-0 dhidi ya TRA United.

Matokeo ya mechi zingine ni Fountain Gate 4-3 Singida Black Stars na Coastal Union 2-1 Pamba Jiji.

NDUWUMWE ALIVYOMPIKU FEI

Wakati tukiingia raundi ya mwisho, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam alikuwa kinara wa mabao akifunga 15, nyuma yake Mosi Nduwumwe wa Singida Black Stars na Allan Okello wa Yanga kila mmoja akiwa na 14. Lakini dakika tisini, hali ikabadilika.

Nduwumwe alifunga mabao matatu ‘hat trick’ katika kichapo cha 4-3 dhidi ya Fountain Gate na kumfanya kumaliza kinara wa ufungaji wa ligi hiyo akiwa na 17 na alianza kucheza baada ya dirisha dogo la Januari 2026 kufunguliwa.

Hiyo ni hat trick ya pili kwake na ya tano msimu huu.  Zingine zikifungwa na Mathew Tegis wa Pamba Jiji na Fabrice Ngoy kutoka Namungo na Okello.

Wakati Nduwumwe alipokuwa akipambania tuzo hiyo katika mechi ya mwisho, Fei Toto alianzia benchi na kuingia baadaye katika mechi ambayo Azam ilishinda 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Hii ni mara ya pili Fei Toto anakosa tuzo ya ufungaji bora katika Ligi Kuu Bara akimaliza nafasi ya pili baada ya 2023-2024 alipomaliza na mabao 19, nyuma ya kinara Stephane Aziz Ki aliyefunga 21.

Wakati huohuo, Djigui Diarra wa Yanga, amemaliza kuwa kipa kinara wa clean sheet akiwa nazo 17, huku kiungo wa Simba, Elie Mpanzu akiwa kinara wa asisti akipiga 10.

WAANDISHI: KHATIMU NAHEKA, NEVUMBA ABUBAKAR, OLIPA ASSA NA VICTORIA MELKIAD

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *