
Moshi. Moshi mjini bado hakujapoa. Likitoka hili linakuja lile. Ndivyo unavyoweza kuelezea migogoro inayofukuta katika wilaya hiyo ikiwahusisha viongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hali inayotishia shughuli za maendeleo.
Safari hii, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amemvaa mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, akisema hasomi ilani ya CCM iliyomweka madarakani, kufuatia swali alilouliza bungeni hivi karibu kuhusu maeneo wa wazi kubadilishwa matumizi na manispaa hiyo.
Sakata hilo limeibuka ikiwa ni siku chache tangu kumalizika kwa mvutano wa kisiasa ndani ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini, uliodaiwa kusababishwa na uwepo wa makundi mawili, moja likimuunga mkono mbunge na lile lisilomuunga mkono.
Makundi hayo yamekuwa yakifitinisha viongozi wa CCM na Serikali, huku baadhi ya viongozi wa wilaya wakianza kujipanga mapema kuelekea uchaguzi wa ndani wa mwaka 2027, wakilenga nafasi za kisiasa zitakazowaniwa mwaka 2030.
Mvutano huo ulifikia hatua ya baadhi ya viongozi wa chama hicho, wakiwemo madiwani kudaiwa kuandika barua ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, jambo lililoibua mjadala mpana ndani ya chama na kuongeza ‘presha’ kwa uongozi wa wilaya na kitaifa.
Hali hiyo ilisababisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira kuweka kambi katika wilaya hiyo kusuluhisha mgogoro huo na kurejesha umoja ndani ya chama hicho.
Katika ziara hiyo mwanzoni mwa Juni, mwaka huu, Wasira alielekeza kuvunjwa kwa makundi yote ya WhatsApp ambayo ndiyo yamekuwa yakitumika kuchochea migogoro ndani ya chama hicho, akisisitiza kwamba chama hicho hakiendeshwi kwa malumbano ya mitandaoni.
Zikiwa zimepita wiki tatu tangu ziara ya Wasira, yameibuka mengine mapya baada ya mbunge kuwatuhumu bungeni viongozi wa Manispaa ya Moshi kubadilisha matumizi ya baadhi ya maeneo ya wazi ndani ya manispaa hiyo.
Madai ya mbunge
Katika mkutano wa bajeti uliohitimishwa hivi karibuni jijini Dodoma, mbunge huyo, wakati wa kipindi cha Maswali ya Papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, aliibua hoja kuhusu madai ya kubadilishwa kwa matumizi ya baadhi ya maeneo ya wazi ndani ya Manispaa ya Moshi.
Alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya viongozi wanaokiuka taratibu za matumizi ya ardhi.
Mbunge huyo aliiomba Serikali kutoa kauli kuhusu madai ya ukiukwaji wa matumizi ya maeneo ya Uhuru Park na Shanty Town.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, pale Moshi Mjini kuna eneo la wazi katikati ya mji linaitwa Uhuru Park. Eneo hilo lina zaidi ya miaka 50, lakini leo baadhi ya viongozi wameanza kujenga pale. Wanajenga vibanda vya biashara kama vile vinavyozunguka masoko ya katikati ya miji, jambo ambalo si zuri. Wananchi wengi wanamiminika katika ofisi ya mbunge wakilalamikia hali hiyo,” alihoji Shayo.
Aliongeza: “Vilevile, eneo la Shanty Town ambalo ni makazi ya watu, kuna ujenzi wa ukumbi wa sherehe unaoendelea. Ukumbi huo ukikamilika utasababisha kelele kwa wakazi wa eneo hilo. Aidha, kiwanja hicho ni eneo la wazi. Tunahitaji kauli ya Serikali kuhusu viongozi wanaokiuka matumizi sahihi ya maeneo ya wazi.”
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu aliiagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufuatilia na kuangalia madai hayo na kama yapo yafuate utaratibu.
Meya amjibu mbunge
Akizungumzia hoja hiyo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amesema ilani ya CCM ya 2025-2030 inazungumzia maeneo hayo kuhusu ujenzi wa maduka kuzunguka eneo la Uhuru Park na ukumbi katika eneo la Shant Town kama sehemu ya kitega uchumi kwa manispaa hiyo na hivyo hayajabadilishwa matumizi.
“Swali la mbunge limenihuzunisha sana kwa sababu limenifanya nikatafakari mambo mengi sana. Kama ilani ya CCM ambayo yeye kainadi katika kampeni zake na hii ilani amesimama nayo katika majukwaa yote wakati anaomba kura kwa wananchi kupata ridhaa, labda kama ana chama chake kingine.
“Ilani ya chama chetu imesema kwamba ujenzi wa maduka kuzunguka eneo la Uhuru Park lakini kujenga ukumbi wa nje katika eneo la Shanty Town,” amesema Kidumo.
Aidha, meya huyo amesema eneo la Uhuru Park tayari kuna vibanda ambavyo vipo ndani ya eneo hilo kwa muda mrefu, hivyo wanachokifanya kwa sasa ni kujenga uzio (maduka) kuzunguka eneo hilo, pembeni ya hifadhi ya barabara ili kuendelea kulilinda eneo hilo.
“Sisi tunachokifanya tumejenga ukuta ili kulilinda lile eneo lakini mbele kwenye hifadhi ya barabara tuweke maduka na hii itatusaidia kupata mapato na Serikali yetu inatupima kwa kukusanya mapato,” amesema Kidumo.
Ameongeza: “Hakuna chochote ambacho tumekifanya cha tofauti kwenye haya maeneo lakini akijitokeza mwekezaji pale eneo la Shanty Town tunamkaribisha maana hatujafanya chochote, aje awekeze tupate mapato maana eneo lipo tu na linalimwa maharage. Tupo tayari mwekezaji yeyote ambaye atajiskia kuja kufanya uwekezaji pale tunamkaribisha.”
Meya huyo amesema: “Ukiona kiongozi ambaye tunajenga nyumba moja anaenda kuzungumza mambo kama haya inasikitisha. Sasa naanza kumwelewa Profesa Assad, juzi wakati anahojiwa alisema haya maneno…tuna viongozi wengi ambao hawasomi makabrasha.
“Nilitegemea angetupongeza kwa sababu tumeanza kutekeleza ilani ya chama chetu, labda huenda ana ilani yake tofauti na hii tunayoitekeleza sisi,” amesema Kidumo.
Alipotafutwa kuzungumzia kauli hiyo ya meya, mbunge huyo amesema hawezi kumjibu meya kwa kuwa tayari alishatoa hoja yake kwa waziri mkuu bungeni Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji, Franscis Shio amesema maeneo hayo yana hatimiliki ya halmashauri na matumizi yake ni kwa ajili ya biashara, ili kukuza mapato ya halmashauri.
“Kinachofanyika eneo la Uhuru Park ni kutengeneza uzio kuzunguka lile eneo na ni mpango wa muda mrefu, maana kule ndani kuna vibanda kama 39 ambavyo vilishajengwa siku nyngi. Tunachokifanya tunaboresha lile eneo na kuweka utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka lakini kupata mapato,” amesema Shio.
CCM yatia neno
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kulikuwa na utaratibu wa kuendeleza eneo la Uhuru Park kwa kujenga vibanda vya biashara ili kuongeza mapato ya Manispaa ya Moshi.
“Kuhusu Uhuru Park, hakuna jambo lolote linalofanyika katika Manispaa ya Moshi bila kufuata utaratibu. Ndani ya Ilani ya CCM, pamoja na ilani ya Mkoa wa Kilimanjaro, ukiangalia kipengele kinachohusu Moshi, utagundua kuwa kulikuwa na utaratibu wa kujenga vibanda au kutekeleza mradi utakaosaidia Manispaa kupata mapato zaidi,” amesema Boisafi.