Tanga. Waziri wa Nishati, Deogratias Ndejembi amemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme cha Hale mkoani Tanga, kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliobaki wa mkataba bila kuomba kuongezewa.
Ndejembi amesema kukamilika kwa mradi huo kutarejesha uzalishaji wa megawati 21 za umeme, hatua itakayoongeza nguvu katika Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kaskazini ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka.
Mradi wa ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme cha Hale unagharimu Dola za Marekani 24.81 milioni, sawa na Sh64 bilioni.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa mitambo mipya pamoja na kituo cha kupooza umeme. Hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 83, huku Serikali ikitarajia mradi huo kukamilika ifikapo Julai 31, 2026.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo leo Juni 30, 2026, Waziri Ndejembi amesema Kituo cha Hale kilipoanza kufanya kazi baada ya uhuru, kilikuwa kinazalisha megawati 21, kiwango kilichokuwa kinatosheleza mahitaji ya taifa wakati huo ambapo matumizi ya umeme yalikuwa takribani megawati 36.
Mafundi wakiendelea na shuguli za ujenzi wa Kituo cha kusukuma mafuta hadi Chongoleani katika bandari ya Tanga.
Amesema kadri miaka ilivyoenda, mitambo ya kituo hicho, ambayo sasa ina zaidi ya miaka 60, ilichakaa na kusababisha uwezo wa uzalishaji kushuka kutoka megawati 21 hadi megawati nane pekee.
“Kutokana na uchakavu huo, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (Sida), ilitoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki. Serikali ya Tanzania imechangia asilimia 40 ya gharama za mradi huku Sweden kupitia Sida ikichangia asilimia 60 na kufanya jumla ya gharama kufikia Sh64 bilioni,” amesema Ndejembi.
Ameeleza kuwa fedha hizo zimetumika kufunga mitambo mipya ya kisasa yenye lengo la kurejesha uwezo wa kituo hicho kuzalisha megawati 21 kama ilivyokuwa awali.
Hata hivyo, Ndejembi amesema Serikali haijaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, kwani ulitakiwa kuwa umekamilika miezi 10 iliyopita.
“Mradi huu uko nyuma ya ratiba. Leo tumemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kabla ya Julai 31, 2026 ambao ndiyo mwisho wa mkataba wake. Hatutatoa nyongeza nyingine kwa sababu tayari aliongezewa Machi ili akamilishe kazi,” amesema.
Amebainisha kuwa jambo la kutia matumaini ni kwamba asilimia 98 ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi tayari vimewasili eneo la mradi na mafundi wanaendelea na kazi, hivyo matarajio ni kwamba uzalishaji wa megawati 21 utaanza baada ya mradi kukamilika.
Kwa mujibu wa Ndejembi, kuongezeka kwa umeme huo kutasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati katika mikoa ya Kaskazini, hususan Mkoa wa Tanga ambao kwa sasa unatumia takribani megawati 130 kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi na viwanda.
Amesema pamoja na kufunga mitambo mipya ya kuzalisha umeme, mradi huo unahusisha uwekaji wa transfoma kubwa yenye uwezo wa kupokea na kusambaza umeme mwingi pamoja na kubadilisha nyaya za zamani zilizowekwa mwaka 1964 ambazo uwezo wake wa kusafirisha nishati hiyo ulikuwa mdogo.
“Hatua hizi zitaimarisha Gridi ya Taifa na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa mikoa ya Kaskazini. Umeme si anasa, ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya sekta za afya, elimu, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji,” amesisitiza.
Kituo cha kusuka mafuta ghafi kilichopo Handeni Mkoani Tanga kikiwa kimefikia zaidi ya asilimia tisini ya ujenzi .Picha na Mbonea Herman
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji Umeme wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Timothy Mgaya amesema taasisi hiyo imepokea maelekezo ya Serikali na itaendelea kumsimamia mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi kwa mujibu wa masharti ya mkataba.
“Sisi kama Tanesco tumepokea maelekezo hayo na tutayafanyia kazi kikamilifu tutamsimamia mkandarasi kuhakikisha anatekeleza wajibu wake kwa wakati na endapo kutakuwa na ukiukwaji wa masharti ya mkataba, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa vifungu vya mkataba,” amesema Mgaya.