Pemba. Serikali ya Canada imesema itaendelea kushirikiana na Serikali za Tanzania katika sekta  mbalimbali, ikiwemo uchumi wa buluu kwa utoaji wa vitendea kazi kwa wajasiriamali ili kukuza uchumi wao.

Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns ametoa kauli hiyo leo Juni 30, 2026 kwenye hafla ya ugawaji wa vitendea kazi kwa vikundi vya wajasiriamali, baada ya ufunguzi wa kituo cha mafunzo eneo la Chamanangwe, Wilaya ya Wete mkoani Kaskazini Pemba.

Amesema vifaa vilivyokabidhiwa kwa vikundi 12 vya ushirika Kisiwani Pemba ni boti maalumu na mashine zake, viatu, meza za ofisi, viatu maalumu, kompyuta mpakato na kompyuta za mezani.

Vingine ni makoti maalumu ya uokozi, waya za kuanikia dagaa na mwani, vioo vya kuzamia, majembe pamoja na uzinduzi wa kituo cha mafunzo cha wajasiriamali vyote vikiwa na thamani ya Sh270 milioni.

“Serikali ya Canada inaendelea kuwahidi ushirikiano huu kwenye sekta mbalimbali ikiwemo uchumi wa buluu na utakuwa endelevu pamoja na maeneo mingine,” amesema.

Amesema ushirikiano huo utawasaidia wajasiriamali waliojikita kwenye eneo hilo la uchumi wa bahari hasa wanawake na vijana, ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakuhusishwa moja kwa moja.

Amesema Zanzibar na baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara iliyozungukwa na bahari, wakati umefika manufaa yake yawanufaishe makundi yote hasa wanawake.

Katika hatua nyingine, Balozi huyo amewataka wajasiriamali hao, kuhakikisha vifaa hivyo ikiwemo boti maalumu, wanavitumia kwa lengo la kukuza pato lao.

“Vifaa hivi tulivyovikabidhi kwenu ni heshima kubwa kwa viongozi wa Tanzania ambao wamekuja na sera ya uchumi wa buluu, sasa mwelekeo wenu uwe wa maana sana,” amesisitiza.

Awali, Mkurugenzi wa Mradi wa Resea, Andreanne Martel-Mi amesema ni jambo la faraja kuona Serikali ya Canada imetekeleza kwa vitendo ahadi yake katika kuwawezesha wajasiriamali kukuza kipato chao.

“Kama inavyoeleweka kuwa wanawake ndio kundi ambalo liliachwa nyuma kwenye sekta kadhaa, ikiwemo ya bahari lakini kwa hili lililofanywa na wenzetu wa Canada, matunda yanakuja kwa haraka,” amefafanua.

Katika hatua nyingine, amesema vikundi hivyo kwa sasa vimekuwa kiuchumi, na kama vile kukabidhiwa kwa vifaa hivyo, vinakwenda kujitegemea.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdalla Rashid Ali amewataka wajasiriamali waliokabidhiwa vifaa hivyo, kwanza kuvithamini na kisha kuhakikisha vinazaa matunda.

“Kwa hakika wenzetu wa jumuiya ya Inclusion wamefanya jambo jema, kuwapata wafadhili wa serikali ya Canada na sasa kuwagawia vifaa hivi,” amefafanua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Ruzuku wa Wanawake Tanzania (WFTT), Rose Marandu amesifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Canada, kwa kuunga mkono wajasiriamali kufikia malengo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *