Dar es Salaam. Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC 2025/2026 baada ya leo, Jumanne, Julai 30, 2026 kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Matokeo hayo yameifanya Yanga imalize kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 75, huku Simba iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC ikimaliza katika nafasi ya pili na pointi 73.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yamepachikwa na Prince Dube, Laurindo Depu na Maxi Nzengeli.

Rais wa TFF, Wallace Karia akikabidhi ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa nahodha wa Yanga, Bakar Mwamnteto. Picha na Michael Matemanga

Hata hivyo furaha ya ushindi ya Yanga katika mchezo huo, ilitikiswa katika dakika ya 43 baada ya Pacome Zouzoua kuchezewa rafu mbaya ambayo ilisababisha avunjike mguu wake wa kulia.

Mtibwa Sugar imeungana na KMC kushuka daraja wakati huo timu za Mbeya City na Tanzania Prisons zikibaki na kibarua cha kucheza mechi za mchujo (play off) ili zipambanie kubaki Ligi Kuu na timu nyingine zimefanikiwa kubaki katika ligi.

Baada ya kuongoza chati ya Ufungaji Bora kwa muda mrefu, kiungo wa Azam FC, Feisal Salum alijikuta akikosa tuzo ya Mfungaji Bora katika raundi ya mwisho ambapo nyota wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe.

Nduwumwe ambaye leo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha amefunga mabao matatu (hat trick) katika kichapo cha mabao 4-3 ambacho timu yake imekipata kutoka kwa Fountain Gate, amemaliza akiwa amefumania nyavu mara 17.

Hii ni mara ya pili kwa Feisal kukosa zawadi ya Ufungaji Bora katika raundi ya mwisho ya ligi ambapo mara ya kwanza ilikuwa katika msimu wa 2023/2024.

Haikuwa siku nzuri kwa Mtibwa Sugar ambayo msimu mmoja baada ya kurejea Ligi Kuu, imeshuka daraja.

Kichapo cha mabao 2-1 ilichokipata kutoka kwa Namungo FC kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi, kimeifanya Mtibwa Sugar kumaliza katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi na kuungana na KMC kushuka daraja.

Ikumbukwe KMC ilishuka daraja tangu mwezi uliopita.

MATOKEO YA MECHI ZA LEO

JKT Tanzania 0-3 Yanga

Simba 1-0 KMC

Coastal Union 2-1 Pamba Jiji

Fountain Gate 4-3 Singida BS

Mbeya City 0-0 TRA United

Mashujaa FC 0-1 Tanzania Prisons

Azam FC 2-0 Dodoma Jiji

Namungo 2-1 Mtibwa Sugar

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *