Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump aliingiza zaidi ya dola bilioni moja kupitia shughuli zinazohusiana na sarafu za kidijitali mwaka jana, kwa mujibu wa ripoti yake ya lazima ya mwaka 2025 ya kutangaza mali zake.
Katika ripoti hiyo yenye kurasa 927, Trump amesema alipata dola milioni 635 kutokana na mrabaha wa sarafu ya kidijitali ya Trump meme coin, ambayo thamani yake imeshuka kwa kiasi kikubwa tangu ilipozinduliwa siku tatu kabla ya kuapishwa kwake.
Pia amesema alipata zaidi ya dola milioni 500 kutoka World Liberty Financial, kampuni ya sarafu za kidijitali iliyoanzishwa na wanawe pamoja na watoto wa mjumbe wake maalum wa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.
Mbali na hilo, Trump alipata mamilioni ya dola kupitia biashara za mali isiyohamishika na bidhaa zinazobeba jina la Trump.
Hata hivyo, Ikulu ya White House imekanusha kuwa Trump ananufaika kifedha kutokana na urais wake.
Mapato yaliyoorodheshwa katika ripoti hii mpya ni makubwa zaidi kuliko yale aliyotangaza mwaka 2024, aliposema alikuwa ameingiza zaidi ya dola milioni 600.
White House pia ilikanusha kuwapo kwa mgongano wa maslahi, ikisema Trump alihamishia biashara zake kwenye mfuko wa amana unaosimamiwa na wanawe.
Naibu msemaji wa White House, Anna Kelly, amesema rais huyo ameifanya Marekani kuwa “kitovu cha dunia cha sarafu za kidijitali.”