Manyara. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amempa siku 14 mkandarasi anayejenga barabara ya Mbulu – Hydom kufikisha vifaa vyote vya ujenzi vinavyohitajika katika eneo la mradi kama mkataba unavyoeleza. 

Ulega alitoa maagizo hayo jana Jumanne, Juni 30, 2030 wakati alipokuwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo kampuni ya Jiangxi Geo Engineering ya China inayojenga kipande cha Labay – Hydom chenye urefu wa kilomita 25 kwa lami.

Wakati akitaka kupewa taarifa na mkandarasi, waziri huyo alielezwa asilimia takribani asilimia 50 ya vifaa tayari vipo eneo la tukio, taarifa ambayo Ulega alisema haikuwa ya ukweli kwa sababu nyaraka zinaonyesha ni asilimia 33 tu ya vifaa ndiyo vimefika katika eneo la mradi.

“Nyaraka zinaonyesha vifaa vilivyopo hapa ni asilimia 33 tu. Nakuagiza kwamba nataka kuona vifaa vyote vinavyohitajika vinafika hapa katika muda wa wiki mbili kutoka sasa. Hayo ndiyo masharti ya mkataba na ni muhimu kufuatwa, “ alisema.

Waziri huyo alisema barabara hiyo ni ya muhimu kwa sababu ndiyo inaunganisha mikoa mitano ambayo ni Arusha, Manyara, Simiyu, Singida na Shinyanga na unatekelezwa kwa taratibu wa Sanifu Jenga (Design and Build).

Ulega aliendelea kuwasisitiza watendaji na wasimamizi wa mradi kusimamia ubora wa ujenzi wa barabara ili iweze kudumu na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

“Haipendezi kuona barabara iliyojengwa ndani ya mwaka mmoja ina mashimo hiyo inatokana na kujengwa chini ya kiwango. Suala la ubora halina mjadala na sitalivumilia nitawachukulia hatua kwa wote watakaoshindwa kusimamia hilo,” alisema Ulega.

Ulega alisema suala la ubora wa barabara halihitaji mjadala hivyo watendaji wanaosimamia na  kukagua miradi wazingatie ubora na ufanisi katika kila hatua ya ujenzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *